Dar es Salaam. Mgombea urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mechi ya ufunguzi wa mashindano ya
Kombe la Kagame kati ya Yanga na Gor Mahia.
Dk Magufuli aliyepitishwa na mkutano mkuu wa chama
hicho, Jumatatu mjini Dodoma amepewa heshima hiyo ikiwa ni kutambua
mchango wake katika maendeleo wakati akiwa waziri.
Hilo litakuwa kusanyiko la kwanza kwa mwanasiasa
huyo ambaye hakuwahi kujiainisha kwenye ushabiki wa soka, hasa kwa klabu
kubwa, Simba na Yanga.
Wakati hayo yakiendelea, Shirikisho la Soka Tanzamia (TFF) limeahidi kuweka ulinzi maalumu wakati wa mashindano hayo.
Shirikisho hilo limeahidi usalama na ulinzi wakati wakati wote mashindano hayo kwa mashabiki na timu zote zitakazoshiriki.
Hakikisho hilo la TFF limekuja siku chache
kufuatia kuibuka kwa matukio ya uhalifu jijini Dar es Salaam
yanayohusisha uvamizi wa vituo vya polisi kwenye maeneo kadhaa.
Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na TFF ni
kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vimeombwa kutoa
ulinzi maalumu kwa timu zote zitakazoshiriki mashindano hayo.
Ulinzi huo kwa timu utahusisha misafara, hoteli
zote ambako timu hizo zitafikia huku mikakati kiulinzi, ikiwa pia kwa
mashabiki kwenye viwanja vitakavyotumika, Karume na Taifa.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa TFF,
Baraka Kizuguto alisema kuwa pamoja na vyombo vyote vya ulinzi na
usalama, pia wameweka mikakati kabambe ya kuhakikisha hakuna matukio ya
aina yoyote yanayoweza kuvuruga au kuhatarisha amani kipindi chote cha
michezo hiyo.
“Tunawahakikishia wapenzi wa soka na Watanzania
kwa jumla kuwa kutakuwa na usalama wa kutosha kwani vyombo husika tayari
vimeshachukua hatua madhubuti ili kuhakikisha kuwa hakuna aina yoyote
ya uvunjifu wa amani na ulinzi utakuwa ni wa uhakika, hivyo mashabiki
wasiwe na wasiwasi,” alisema Kizuguto.
Katika hatua nyingine, Alhamisi kutakuwa na
mtihani maalumu kwa waamuzi, Cooper Test ambako wale wakatakaofuzu ndiyo
watachezesha mashindano hayo
Post a Comment Blogger Facebook