Dar es Salaam. Baada ya tetesi za muda mrefu,
hatimaye Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi ), Moses Machali amejiunga
na Chama cha ACT - Wazalendo.
Naibu Katibu Mkuu wa ACT - Wazalendo, Msafiri
Mtemelwa alisema hayo jana alipokuwa akimtambulisha kwa waandishi wa
habari, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitengo cha Vijana wa NCCR - Mageuzi,
Deo Meck ambaye naye amejiunga na chama hicho.
Machali ambaye hakuwapo kwenye utambulisho huo,
alithibitisha kwa simu jana kujiunga na chama hicho kipya kinachoongozwa
na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na kusema atatoa
ya moyoni Julai 21 katika mkutano utakaofanyika kwenye Uwanja wa
Kiganamo, Kasulu Mjini. “Nitakuwa na Zitto na wabunge wengine ambao
siwataji kwa sasa,” alisema Machali. awali, Mtemelwa alisema Machali
amejiunga na chama hicho na kwamba kinachosubiriwa ni utaratibu maalumu
wa kumtambulisha kwa wananchi.
“Siyo Machali pekee ambaye amekuwa akihusishwa
kuhamia katika chama hiki, bado kuna wabunge kama wanne, nao wakati
wowote watatambulishwa kwa wananchi. Staili yetu kwa hawa wabunge ni
kuwapokea na kuwatambulisha katika majimbo yao, mbele ya wapigakura,”
alisema Mtemelwa.
Alisema kuhamia katika chama hicho kwa wabunge na
vijana wengi kutoka upinzani ni mwendelezo wake wa kupokea wananchi wa
sehemu mbalimbali wanaotaka demokrasia ya kweli. Meck ambaye
alikabidhiwa kadi ya uanachama jana hiyohiyo, alisema ameamua kuhamia
ACT kwa sababu vyama alivyopita havikuwa na demokrasia na mabadiliko ya
kweli.
Alisema baadhi ya vyama vya siasa havijajikita
katika kutoa elimu kwa wanachama wake na kwamba ACT imedhamiria
kuirudisha nchi katika misingi iliyowekwa na waasisi wa Taifa.
“ACT kipo tofauti na vyama vingine, leo (jana )
nimejiunga na nimepewa vielelezo ambavyo ni kama mwongozo kwa kile
kinachofanywa,” alisema Meck. Mbali na mwanachama huyo, pia aliyewahi
kuwa mlinzi wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) Khalid Kagenzi naye alionekana katika ofisi hizo.
Alipoulizwa na waandishi wa habari kama amehamia
alijibu: “Ni haki ya kila Mtanzania kujiunga na chama chochote cha siasa
anachokitaka. Bado sijachukua kadi yangu ya uanachama,” alisema
Kagenzi.
Post a Comment Blogger Facebook