Dar es Salaam. Wakati mchakato wa kumtafuta
mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM ukiwa umekamilika, ni dhahiri kwamba
baadhi ya vigogo waliokuwa na matumaini makubwa ya kuukwaa, sasa
wanaugulia maumivu huku wengine wakiwa wameshautangazia umma kutoendelea
na ubunge.
Licha ya kuwa siasa ni pata potea, kwa wanasiasa
vijana huenda mchakato huo ukawa ni mwanzo wa safari ya kuelekea kwenye
kilele cha mafanikio na kwa baadhi ya vigogo huenda ukawa ndiyo mwanzo
wa kuelekea kustaafu siasa.
Edward Lowassa, Frederick Sumaye, Dk Mohammed
Gharib Bilal, Stephen Wasira, Mizengo Pinda, Samuel Sitta na Profesa
Mark Mwandosya ni makada waliojitokeza kujaribu bahati yao ya kuteuliwa
kugombea urais, lakini ni dhahiri kuwa sasa watakuwa wanaanza kujiwekea
mazingira ya kuachana na siasa.
Wote hawakumudu kuingia kwenye orodha ya wagombea
watano waliopelekwa kwenye Halmashauri Kuu kwa ajili ya kuchujwa hadi
kubakia watatu ambao hupelekwa kwenye Mkutano Mkuu kwa ajili ya kumpata
mgombea urais wa CCM.
Kwa mujibu wa utaratibu wa CCM wa kumuachia mteule
agombee kwa vipindi viwili iwapo anashinda uchaguzi wa Rais, makada hao
sasa watalazimika kusubiri hadi mwaka 2025 ili kujaribu tena bahati
yao, jambo ambalo linaonekana halitakuwa rahisi.
“Nyakati za kisiasa zinabadilika haraka sana.
Miaka 10 ijayo siyo mchezo,” alisema Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria
Tanzania (OUT), Hamad Salim alipohojiwa na Mwananchi kuhusu mustakabali
wa makada waliokosa nafasi ya kupeperusha bendera ya CCM kwenye Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba 25.
“Kwa kipindi hicho, mambo mengi yatabadilika,
wanasiasa waliogombea kipindi hiki hawawezi kuwa kwenye umaarufu wa
sasa, wanaweza kupanda chati au kushuka.
“Pia, kuna suala la umri wazee kama Dk Bilal au
Sumaye miaka 10 ijayo kupanda jukwaani na kushuka mara kwa mara itakuwa
shida kidogo. Wanasiasa wengi waliokuwamo kwenye kinyang’anyiro hicho ni
wazee na ule siyo umri wa kushinda majukwaani.”
Licha ya sifa za mgombea kutozungumzia umri wa juu
bali wa chini ambao ni kuanzia miaka 40, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, Richard Mbunda alishauri baadhi ya vigogo walioshindwa
kupumzika kupisha damu changa za mabadiliko.
Alisema: “Siasa nchini hazitabiriki na ni za
kipekee kwani unaweza ukawa maarufu usichagulike na siku zinavyokwenda
ukapoteza umaarufu huo.
“Kwa hali ya sasa, Bilal, Pinda, Lowassa, Sitta
tayari walishakamata nafasi za juu nchini na umri wao umeshasogea. Bila
shaka ni muda muafaka kupisha wengine… wameshaitumikia nchi vya kutosha
na wana marupurupu ya kutosha baada ya kustaafu. Ni bora wawaachie
vijana walete mabadiliko,” alisema Mbunda.
Alisema makada hao ni washauri wazuri iwapo
wataachana na siasa za kushindana. Alisema hata kwa wale ambao umri
unawaruhusu, haitakuwa vizuri kuwapa vyeo vidogo kama vya ubalozi na kwa
maana hiyo alisema safari yao kisiasa, imefikia ukingoni.
Post a Comment Blogger Facebook