JESHI
la Polisi mkoani Dodoma linamshikilia mkazi wa Katesh katika wilaya ya
Kiteto mkoani Manyara, Mohammed Abdallah (35), baada ya kukutwa akitoa
huduma za kidaktari ambazo hana utaalamu wake.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema Abdallah alikamatwa
Agosti 12, mwaka huu saa tisa mchana katika kijiji cha Nyerere kata ya
Hogoro tarafa ya Zoissa wilaya ya Kongwa, akiwa tayari ametoa huduma ya
matibabu kwa wagonjwa zaidi ya 20.
Kabla
ya kukamatwa kwake, Kamanda Misime alisema Polisi ilipata taarifa za
siri na kuzifanyia kazi, ambapo mtuhumiwa alikamatwa katika nyumba
isiyostahili kufanyiwa shughuli za matibabu mali ya Sikitu Magomba.
Kamanda
Misime alisema baada ya mtuhumiwa kukamatwa katika nyumba hiyo
alikopanga, alipopekuliwa, alikutwa na dawa mbalimbali zenye nembo ya
Bohari ya Madawa (MSD), mifuko tisa ya dripu za ujazo wa milimita 500,
ambazo kwa kawaida haziruhusiwi kuuzwa, sindano na baadhi ya vifaa tiba
vinavyodhaniwa vilipatikana kwa njia isiyo halali.
Baada
ya kuhojiwa, kwa mujibu wa Kamanda Misime, mtuhumiwa alikiri kutenda
kosa hilo na kuongeza kwamba hana taaluma yoyote ya utabibu na elimu
yake ni darasa la saba. Kamanda Misime alisema uchunguzi zaidi
unaendelea na ukikamilika, mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani.
Alitoa
mwito kwa wananchi kuwa makini na kuhakikisha wanatibiwa kwenye
zahanati, vituo vya afya na hospitali zinazofahamika, ili kuepuka
madhara dhidi ya tiba bandia.
Pia
alitaka wananchi kufichua madaktari feki, ili wachukuliwe hatua za
kisheria, kwani wanapotibiwa na mtu ambaye hana utaalamu, kwanza
huwatapona na pili watapata madhara ambayo yanaweza kuwa ya kudumu na
pengine kupoteza maisha
Post a Comment Blogger Facebook