KIUNGO anayeweza kucheza nafasi zote za ulinzi, Erasto Edward Nyoni yuko mbioni kujiunga na mabingwa wa Tanzania, Yanga baada ya kumaliza mkataba wake Azam FC
Nyoni yupo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayojiandaa kwa mchezo na Rwanda Jumamosi Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza kuwania tiketi ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), michuano inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee – na Yanga wanatarajia kumalizana naye kabisa baada ya mechi hiyo.
“Mazungumzo na Nyoni yamekwenda vizuri na wakati wowote tunaweza kumalizana naye, pengine baada ya mechi tu dhidi ya Rwanda,”kimesema chanzo kutoka Yanga.
Benchi la Ufundi la Yanga, chini ya Kocha Mkuu, Mzambia George Lwandamina kwa kushirikiana na Sekretarieti chini ya Katibu Mkuu, Charles Boniface Mkwasa ambaye kitaaluma ni kocha kwa pamoja wamejiridhisha Nyoni ni mchezaji ambaye wanamuhitaji kikosini.
Na hiyo ni kwa sababu huyo ni ‘kiraka’ anayeweza kucheza nafasi yoyote ya ulinzi kuanzia kiungo wa ulinzi – lakini uzoefu na weledi wake kisoka ni vitu vingine vinavyomuunganisha na Yanga katika siku za mwishoni za maisha yake ya uwanjani
Post a Comment Blogger Facebook