Jeshi nchini Nigeria limewaokoa watu 178 waliokuwa wakishikiliwa mateka na kundi la Boko Haram, wakiwemo watoto zaidi ya 100 katika jimbo la Kaskazini la Borno.
Msemaji wa Jeshi hilo Kanali Tukur Gasau amesema kati ya watu hao walikuwa watoto 101, wanawake 67 na wanaume 10.
Katika Operesheni hiyo ya uokoaji iliyofanyika katika eneo karibu na Aulari takriban kilometa 70 kusini mwa Maiduguri ambao ni mji mkubwa kaskazini mwa Nigeria, Kamanda mmoja wa kundi la Boko Haram pia alikamatwa.
Miezi ya hivi karibuni Jeshi la Nigeria limetangaza kuwaokoa mamia ya watu waliokuwa wakishikiliwa mateka na kundi la Boko Haram, haswa katika eneo sugu la msitu wa Sambisa, ambao ni ngome kubwa ya wapiganaji hao wa kiislam.
Kundi la Boko Haram limewaua raia takriban 5,500 nchini Nigeria tangu mwaka 2014.
Mpaka sasa zaidi ya wanafunzi wasichana 200 wa Chibok hawajulikani walipo, ikiwa ni mwaka mmoja umepita tangu walipotekwa shuleni kwao kaskazini mwa Nigeria, ambapo wengi kati ya waliotekwa ni wakristu.
Mwezi Oktoba mwaka jana serikali ya Nigeria ilisema imefikia makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa wanafunzi hao, lakini kundi la Boko Haram limekanusha madai hayo.
Post a Comment Blogger Facebook