Chande Abdallah na Deogratius Mongela
Mshtuko! Bi harusi Agnes Omari (26) amezua kizaazaa baada ya kudaiwa kupandisha mashetani kanisani wakati akivishwa pete ya ndoa, hali iliyosababisha tendo la kufungishwa ndoa kusimama kwa muda kwa ajili ya kutafuta msaada wa maombi.
Akizungumza na Ijumaa Wikienda, bwana harusi, Arnold Martin alisema sakata hilo lilijiri hivi karibuni kwenye Kanisa Katoliki la Parokia ya Mbagala-Zakhem jijini Dar.
Alisema kwamba, alipata taarifa usiku wa kuamkia siku ya ndoa kutoka kwa msimamizi wa bi harusi kuwa mchumba’ke amepandisha mashetani, tatizo ambalo hakuwa nalo katika kipindi chote walichoishi pamoja.
Kutokana na tatizo hilo, Arnold alisema alivunja utaratibu na kwenda kumuona mchumba’ke huyo na kumkuta akijigaragaza huku akipiga makelele na kuzungumza lugha za ajabu.
“Kulipokucha, hali yake ilionekana kuwa nzuri kiasi kwamba majira ya saa 3:00 asubuhi, aliondoka na msimamizi wake kwa ajili ya kubadilisha gauni la harusi maeneo ya Mbagala-Kizuiani baada ya lile la awali kuonekana kumbana huku na mimi nikijiandaa kwenda saluni,” alisema Arnold.
Baada ya kutoka na msimamizi wake huyo, haukupita muda mrefu akapigiwa simu kuwa hali hiyo imejirudia, akamfuata na kumbeba kwenye gari lake kisha kumkimbiza katika Parokia ya Mbagala-Zakhem kwa ajili ya msaada wa maombi na kutoa taarifa kwa paroko kuhusu hali ya mchumba’ke huyo.
Bi harusi huyo aliombewa lakini wakati akimvisha pete ya ndoa kanisani hapo hali hiyo ilijirudia ndipo alipohamishiwa katika Kanisa la Nabii Yaspi lililopo Buza-Kipera jijini Dar ambapo wakiwa huko, walikutana na wachungaji ambao waliwaombea na hali ikatulia.
“Hali hiyo ilijirudia tena wakati tukipiga picha palepale kanisani akaanza tena kupandisha mashetani, akaombewa lakini hali ilizidi kuwa mbaya, wakaja watu wa Karismatiki nao ikashindikana ikabidi tufunge safari tena kuelekea kulekule kwa Nabii Yaspi ambako aliombewa, akapona.
“Wakati tukiingia ukumbini, hali hiyo ilijirudia tena ambapo sherehe nzima iliharibika na kuwa majonzi hivyo kila mtu akaondoka kimyakimya.
“Bi harusi aliondoka na ndugu zake usiku ule hadi kesho yake nilipoambiwa amerudia hali yake ya kawaida ila kinachonishangaza nilipoenda pale nyumbani kwao alikuwa akionesha kama vile hanifahamu kabisa pamoja na kwamba nilifunga naye ndoa,” alisema Arnold ambaye alidai kuwa anatarajia kurudi tena kwa Nabii Yaspi ili kumaliza tatizo hilo.
Post a Comment Blogger Facebook