Dar es Salaam. Chama cha
Wananchi (CUF) kimesema uamuzi wa Jeshi la Polisi kuzuia misafara ya
wagombea urais wakati wa kuchukua na kurejesha fomu batili, kinyume na
Katiba ya nchi na sheria ya vyama vya siasa, na unalenga “kuionea huruma
CCM” baada ya kufunikwa na vyama vinavyounda Ukawa.
Polisi
imepiga marufuku misafara hiyo kwa maelezo kuwa imesababisha usumbufu
kwa wakazi na kusimamisha shughuli nyingine za kila siku.
Naibu
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Abdulrahman Kaniki alitangaza uamuzi
huo juzi baada ya watu wengi kujitokeza kumsindikiza mgombea urais wa
CCM, Dk John Pombe Magufuli na baadaye wengi zaidi kujitokeza wakati
mgombea wa Chadema, Edward Lowassa alipokuwa akienda kuchukua fomu Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Jana naibu katibu mkuu wa
CUF, Magdalena Sakaya alisema chama hicho kitaendelea kufanya maandamano
na mikutano ya hadhara kama kawaida.
Alidai kauli ya
polisi ni agizo la CCM baada ya kuona Watanzania wanajitokeza kwa wingi
kwenye shughuli za kisiasa zinazofanywa na kwa pamoja na vyama
vinavyounda Ukawa ambavyo ni Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF.
“Tumesikitishwa
na kauli ya polisi. Nadhani wanacheza na amani na utulivu wa nchi yetu.
Maandamano ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania na imeelezwa katika
ibara ya 18(a) na 20 ya Katiba ya Jamhuri ya muungano,” alisema Sakaya.
Alisema
hata sheria ya vyama vya siasa, ibara ya 11 imefafanua kuhusu
maandamano na kusisitiza kuwa kampeni haziwezi kufanywa kimyakimya.
“Huwezi kuzuia maandamano na mikusanyiko katika shughuli za kisiasa,” alisema.
“Kwa
sasa vyama vya upinzani vina wapenzi, mashabiki na wanachama wengi.
Hizi ni njama za CCM kuzuia maandamano maana… katika mikutano yao watu
ni wachache mno. Sisi (Ukawa) mikutano na maandamano yetu ina utulivu
mkubwa. Polisi wasiwe na wasiwasi,” alisema. Alisema Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2005 watu walipoteza maisha kutokana na kauli kama hizo za kuzuia
maandamano na mikusanyiko.
“Hii ni ishara kuwa polisi
watatumia nguvu nyingi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Wanataka
kulazimisha bao la mkono. Wanatakiwa kulinda usalama wa wananchi katika
mikutano na si kuizuia. Wasome katiba na sheria kwanza, si kuzuia tu
kila jambo,” alisema.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi
kuhusu msimamo wa CUF, kaimu mkuu huyo wa polisi alitaka atafutwe
msemaji wa jeshi hilo, Advera Bulimba ambaye alisisitiza kuwa amri hiyo
inalenga kuimarisha usalama wa nchi na wananchi.
“Mambo
yaliyojitokeza katika maandamano si sawa maana mwananchi walishindwa
kufika katika shughuli zao. Tunaangalia usalama wa nchi kwanza.
Tutafanya mkutano na kuwashirikisha wanasiasa ili kutafuta namna bora ya
kufanya mambo yao bila kuathiri shughuli nyingine,” alisema.
“Hatutangazi
ugomvi wala malumbano na vyama, tunataka siasa kufanyika wakati huohuo
watu wengine wasiathirike. Amani ya nchi haitaki ushabiki na inamhusu
kila mmoja wetu.”
Wakati polisi inazungumzia maandamano
kuwa yalisumbua wananchi wengine, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mathias Chikawe na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova, walipongeza msafara wa Lowassa kwenda kuchukua fomu NEC,
wakisema kama wataendelea hivyo, Uchaguzi Mkuu utafanyika kwa amani.
Na Gazeti la mwananchi
Na Gazeti la mwananchi
Post a Comment Blogger Facebook