Arusha. Mgombea urais kwa
tiketi ya Chadema na Ukawa, Edward Lowassa jana kwa mara ya kwanza
alikumbana na joto la upinzani baada ya msafara wake kushambuliwa na
mabomu ya polisi.
Tukio hilo, ambalo
lilifanyika mbele ya msafara wa Lowassa, lilitokea jana eneo la Daraja
la Nduruma katika Jiji la Arusha na kusababisha umati wa watu
kutawanyika na wengine kutelekeza magari yao.
Wakati
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akimkaribisha kwenye chama hicho
wakati wa mkutano mkuu alimwambia; “Mzee huku inabidi uwe unafanya
mazoezi kidogo, kuna mabomu huku.”
Lowassa alikumbwa na
kadhia hiyo, akiwa njiani na mgombea mwenza, Juma Duni Haji na viongozi
wengine wa Ukawa, wakitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro
(KIA), huku wakiwa wamesindikizwa na umati wa watu na magari.
Tamko la polisi
Kamanda
wa polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema kuwa polisi
walilazimika kupiga mabomu ya machozi ili kutawanya watu waliokuwa
wakiwarushia mawe polisi na wengine kufunga barabara.
“Kwa
hali ile, tungefanya nini? Wanatupa mawe kwa polisi na wamefunga
barabara na kuzuia magari mengine yasipite…ikumbukwe kulikuwa hakuna
kibali cha maandamano na hata kingekuja, matamko ya kuzuia maandamano
yameshatolewa,” alisema Sabas.
Katika tukio hilo, idadi
kubwa ya polisi walikuwa kwenye magari na silaha mbalimbali ambao
baadaye walianza kurusha mabomu kutawanya watu na magari kwa eneo la
daraja hilo.
Hata hivyo, katika tukio hilo, lililotokea
saa nane mchana hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa na kutokana na nguvu
hiyo ya polisi watu walitawanyika, na barabara hiyo ya Arusha- Moshi
ilifunguka baada ya kutopitika kwa saa tano kuanzia saa nne asubuhi.
Ukawa walaani kupigwa mabomu
Akizungumza
katika mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Tindigani, Mbunge wa jimbo
la Arusha, Godbless Lema alisema wamesikitishwa na kitendo cha polisi
kumpiga mabomu Lowassa na msafara wake.
“Tunajua polisi
wamepata maelekezo na sasa wanataka kuwatisha wananchi, lakini tunasema
leo ndiyo mwisho hatutakubali tena kunyanyaswa,” alisema Lema.
Kuwasili Lowassa
Lowassa
aliwasili KIA saa 3:20 asubuhi akiwa ameongozana na viongozi wa Ukawa,
Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa NLD,
Emmanuel Makaidi, Kaimu Mwenyekiti wa CUF taifa, Twaha Taslima na
viongozi wengine.
Kwenye Uwanja wa KIA, shughuli mbali
mbali zilisimama katika eneo la kushuka viongozi mashuhuri (VIP), ambapo
mawaziri kadhaa walikuwa katika eneo hilo.
Baadhi ya
viongozi hao ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
Profesa Mussa Juma Hassadi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Dk Mary Nagu,
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tzeba.
Baada ya
Lowassa kutua KIA, alikwenda moja kwa moja kwenye Hoteli ya KIA Lodge na
mgombea mwenza wake, Juma Duni Haji kwa mapumziko mafupi.
Baada
ya kupumzika saa 5:30 msafara ulianza kuelekea uwanja wa Tindigani
Kimandolu na ulifika saa tisa na kukutana uwanja ukiwa tayari umefurika
maelfu ya watu.
Akihutubia mkutano huo Lowassa
alitahadharisha viongozi wa polisi, kuacha kutumia nguvu kupita kiasi,
kwani anaweza kuwafikisha Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) iliyopo
The Hague nchini Uholanzi.
Lowassa alisema alikuwa akiiamini polisi, lakini alichokiona jana cha kupigwa mabomu ni jambo baya.
Kuhusu
suala la Babu Seya aliyefungwa kifungo cha maisha gerezani alisema
atafuatiliwa kwa kutumia suala la utawala bora kwa kuangalia vyombo vya
sheria na hatua zingine zitafuatwa.
Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe alisema wanachama wanaojiunga sasa wana haki sawa
na mwasisi wa chama hiki Edwin Mtei mwenye kadi namba moja.
Alisema
mara baada ya wanachama wapya kujiunga, kwa kipindi cha wiki moja
nilipokea matusi mengi kuliko niliyowahi kutukanwa baada ya kupokea
wanachama wapya.
Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Taslima
alisema kuna watu ambao wamejenga desturi ya kuwabeza watu wanapohama
vyama kwa hiari kwa kuwaita oili chafu au makapi anavunja Katiba.
Alisema
Ibara ya 20 ya Katiba ya mwaka 1977 inasema kila mtu yeyote ambaye ni
Mtanzania, yuko huru kujiunga na mtu yeyote, chombo chochote, taasisi
yoyote atakayopenda na hatazuiliwa.
Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema; “Mabomu yamepigwa katika mkutano wa
Chadema, watu wakafa Arusha, Arusha tunayoitegemea kwa uchumi leo hii
zaidi ya asilimia 19 ya pato ya taifa linatokana na utalii, lakini leo
(jana) tunaingia Arusha alipozaliwa Lowassa tunapigwa mabomu, ukweli
utatuweka huru.
source; gazeti la Mwananchi
source; gazeti la Mwananchi
Post a Comment Blogger Facebook