0
Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Mh.Dkt John Pombe Magufuli akiwasalimia wananchi alipokuwa akiwasili jijini Mwanza.
SHUGHULI mbalimbali katika maeneo ya Barabara Kuu itokayo Uwanja wa Ndege wa Mwanza hadi mjini katikati, jana zilisimama kwa muda wa saa moja, huku wakazi wa jiji hilo wakishiriki kumpokea mgombea mteule wa urais wa CCM, Dk John Magufuli.
Mapokezi hayo ambayo yameacha historia ya pekee jijini hapa, yalianzia katika uwanja huo saa 8:00 mchana alipowasili akiongozana na mkewe Janeth Magufuli, Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Rajabu Luhavi.
Uwanjani, mgombea huyo alipokewa na mamia ya wana CCM, viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali kutoka mkoani hapa na mikoa ya jirani ya Kanda ya Ziwa, wakiwemo Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani na Naibu Waziri Nishati na Madini, Charles Kitwanga.
Vikundi vya burudani vya ngoma za jadi vikiwemo vya utamaduni vya Bujora, Ritungu vya jijini hapa na sungusungu kutoka Kijiji cha Malembwe wilayani Kwimba, navyo vilishiriki mapokezi hayo.
Msafara wa Dk Magufuli ukiongozwa na pikipiki zaidi ya 150 ulianza safari kwenda mjini kati ya saa nane mchana, ambapo maelfu ya wananchi waliojipanga katika maeneo mbalimbali katika barabara hiyo wakiwemo akina mama, watoto na vijana, wakijitokeza kumlaki na kumpungia kwa khanga za CCM na matawi ya miti.
Maeneo hayo ni pamoja na Ilemela, Butuja, Sabasaba, Iloganzala, Pasiansi, Nyamanoro, Ghana na Mission ambapo alilazimika kusimama kwa muda katika baadhi ya maeneo hayo na kusalimia wananchi baada ya kumzuia wakimtaka awasalimie.
Kote huko wananchi walikuwa wakimshangilia kwa makofi, vigelegele na vifijo wakimuita ‘Jembe’ huku baadhi wakipaza sauti na kumwambia “Wewe ndiye Rais wetu, wengine wanajisumbua.”
Nape
Akimtambulisha mgombea huyo na msafara alioambatana nao kabla ya kusaini kitabu cha wageni cha Chama, Nape alisema CCM imemaliza kazi, Ukawa mwaka huu wataisoma namba.
Alisema mchakato wa CCM ulifanywa kwa kufuata taratibu na ukamalizika salama, wanaoendelea kusema sema wakiwemo wazee ni kutaka kuvuruga Chama, wakiendelea CCM itawajibu na kushughulika nao.
Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati akisalimia, Dk Magufuli alisema atawatumikia Watanzania wote bila ubaguzi na kuahidi kuwa, hatakiangusha Chama Cha Mapinduzi, wana CCM na Watanzania wote iwapo atachaguliwa

Post a Comment Blogger

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();
 
Top