Dar es Salaam. Janeth Magufuli
bado anasubiri miezi mitatu ya kampeni nzito za kumuwezesha mumewe
kuingia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, lakini walimu na wanafunzi wa
Shule ya Msingi Mbuyuni tayari wanasikitika kumpoteza mwalimu huyo wa
jiografia, historia na Tehama.
Mumewe, Dk John Pombe
Magufuli amepitishwa zaidi ya wiki moja iliyopita kuwa mgombea urais wa
Tanzania kwa tiketi ya CCM, na hivyo atalazimika kupambana vikali na
wagombea wa vyama vingine ili kujihakikishia anaingia Ikulu kuongoza
Serikali ya Awamu ya Tano.
Lakini walimu na wanafunzi
wa shule hiyo wanaona kuwa tayari Dk Magufuli ameshajihakikishia tiketi
ya kuingia Ikulu na walichonacho sasa ni kusononeka kwa kuwa wanampoteza
mmoja wa walimu bora shuleni hapo.
“Kama mumewe
akichaguliwa, nitakosa utu na busara zake. Na unajua? Ni mwalimu wa
mazingira na anajua majukumu yake. Darasa la tano watamkumbuka sana,”
anasema mwalimu mkuu wa shule hiyo, Dorothy Malecela.
“Ni
mwanamke mchapakazi sana na ni mwalimu mzuri, mtu mwenye upendo na
mnyenyekevu. mtu pia mwenye moyo mzuri. Wakati fulani alitoa msaada wa
baiskeli kwa mwanafunzi mlemavu shuleni hapa.”
Alikuwa
akimzungumzia mwanafunzi mlemavu Elisha Lameck, ambaye alikuwa akipata
shida kutoka sehemu moja kwenda nyingine wakati akiwa shuleni hapo.
Mwalimu Malecela anasema licha ya kuwa ni mke wa Waziri Magufuli, ilikuwa kazi kufahamu kama ni mke wa kigogo.
“Hakuwa
na makuu hata kidogo, hata watoto wake walikuwa wakisoma hapa, na
mwingine anasoma shule ya Kata ya Oysterbay,” anaeleza.
“Watoto wao wanasoma shule za kawaida sana. Shule ya kata tofauti na wengine ambao huwapeleka nje ya nchi.”
Malecela alieleza kuwa Mwalimu Magufuli hakuwa mtegeaji kazini.
“Hakuwahi kukosa kipindi na kama akiwa na dharura huwa anamwomba mwalimu mwingine amsaidie kipindi chake,” alisema.
Si mwalimu mkuu pekee ambaye alimmwagia sifa Mama Magufuli.
Ally
Rajab na John Manda, ambao wako naye ofisi moja wanamuelezea Mwalimu
Magufuli kuwa mtu ambaye ilikuwa vigumu kumtambua kuwa ni mke wa waziri,
lakini pia mpole na anayeipenda kazi yake.
Mwalimu
Rajab alisema kuwa wakati mwingine walikuwa wakinunua mihogo na kachori
kwa ajili ya chai asubuhi, na Mwalimu Janeth alikuwa akijumuika kula
pamoja nao.
“Hata wakati mwingine wa safari za mafunzo, huwa anatoa fedha kwa watoto ambao wazazi wao wameshindwa kuwalipia,” alisema.
“Hata wakati mwingine inapotokea walimu kukwaruzana ofisini, amekuwa msuluhishi.”
Baadhi
ya wanafunzi wa shule hiyo, Mabano Mzee, Mariam Mwalami wanafunzi wa
darasa la sita, wanasema kuwa Mwalimu Magufuli alikuwa wa aina yake.
Mzee anasema mke huyo wa Dk Magufuli si mtu wa kuchapa viboko wanafunzi.
“Kama kuna tatizo, anakuelekeza, kama una shida anakusikiliza,” alisema Mzee.
Naye
Mariam anasema kuwa anampenda Mwalimu Magufuli kwa kuwa anajua jinsi ya
kumfundisha mtu na anaelewa, na huwa anajua kama watu wameelewa ama la.
“Baada
ya kufundisha huwa anamwita mwanafunzi na kumuuliza kama ameelewa na
kinachonifurahisha, hata tunapokula makande naye hula,” alisema Mariam.
Stella
Ijumba, mwalimu na rafiki mkubwa wa Janeth Magufuli, anasema aliposikia
Dk Magufuli amepita, alijua hatakuwa tena na mwalimu huyo.
“Niliposikia
mzee kapita, nikamtumia meseji, ‘Hongera rafiki yangu, hayo yote
yamepangwa na Mungu’, japokuwa hakujibu, lakini nilijua tu wengi
watakuwa wamemtumia sasa anashindwa kujibu, alisema mwalimu huyo wa
darasa la nne.
“Nitamkumbuka sana rafiki yangu, alikuwa mpole sana... ninawatakia kila la kheri yeye na mumewe.”
Mwingine
aliyemzungumzia Mwalimu Magufuli ni muuza matunda shuleni hapo, alisema
kuwa atamkosa mteja wake ambaye mara kwa mara hununua matunda kwa ajili
ya kula ama kupeleka nyumbani.
“Huwa napeleka matunda
hata nyumbani kwake huwa ananiagiza, lakini juzi juzi hapa nilipokwenda
nikakuta hali tofauti, kulikuwa na ulinzi mkali, nikashindwa kumuuzia,
nikaondoka,” alisema muuza matunda huyo.
“Baadaye
nikasikia habari za mumewe kuwa ameteuliwa kuwania urais, nikaona sasa
ni ngumu tena kumuona na itakuwa tunamuona kwenye Tv tu.”
Lameck,
ambaye alinunuliwa baiskeli na Janeth alisema: “Ninampenda sana Mwalimu
Magufuli kwani kanisaidia baiskeli hii...mama huwa ananichukua kunileta
shule, lakini hii imenisaidia na itampunguzia mama kazi,” anasema.
Anasema
kuwa kaka yake, Eliya sasa ndiye anayemsindikiza kutoka na kwenda shule
na mama yao amebaki nyumbani akiendelea na shughuli nyingine.
Iwapo
Dk Magufuli atachaguliwa kuliongoza Taifa Oktoba 25, Shule ya Mbuyuni
itakuwa imeweka historia ya aina yake kwa kutoa wake wawili wa marais.
Salma
Kikwete, mke wa Rais anayemaliza muda wake, pia alifundisha shule hiyo
katika kipindi chake cha miaka 20 ya utumishi serikalini.
Lakini
kingine kitu kingine cha aina yake ni kwamba iwapo Dk Magufuli atakuwa
Rais, maana yake mkewe ataingia kwenye kundi la wake za marais wawili wa
nchi zilizo kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao majina yao ni
Janeth.
Mke wa Rais wa Uganda ni Janet Kataaha Museveni wakati mke wa Rais Paul Kagame wa Rwanda anaitwa Jeannette Kagame.
Post a Comment Blogger Facebook