Dar es Salaam. Wakati wa hali ya sintofahamu
ikiwa imetawala uteuzi wa mgombea atakayeungwa mkono na vyama vinne vya
upinzani, imebainika kuwa mzozo unaochelewesha suala hilo ni mgombea
ambaye Chadema haijamuweka bayana.
Katibu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ndiye ambaye
anapewa nafasi kubwa ya kupitishwa kugombea urais kwa tiketi ya Ukawa
mbele ya mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na kada wa
NCCR-Mageuzi, Dk George Kahangwa, lakini hadi sasa vyama hivyo bado
vinasita kumtangaza mteule wake.
Profesa Lipumba alikuwa amewaahidi waandishi wa
habari wiki iliyopita kuwa mgombea ambaye ataungwa mkono na vyama hivyo
vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD angetangazwa Julai 14, lakini siku
hiyo hakuna aliyetangazwa.
Badala yake viongozi wa Chadema, NLD na NCCR ndio
waliofika Hoteli ya Coloseum jijini Dar es Salaam ambako Profesa Lipumba
aliahidi kuwa ndiko jina la mgombea huyo lingetajwa, wakati viongozi wa
CUF hawakuonekana na baadaye jioni wakasema kuwa walikuwa na kikao cha
ndani ya chama cha kutafuta ufumbuzi wa mambo ambayo walikuwa
hawajakubaliana.
Vyama hivyo vitatu vikaeleza baadaye kuwa jina
hilo litatangazwa ndani ya siku saba kuanzia Julai 14, lakini siku
iliyofuata CUF ilisema suala la kuachia chama kingine jukumu la
kusimamisha mgombea urais litawasilishwa kwenye kikao cha Baraza Kuu la
chama hicho ambacho kitafanyika Julai 25, jambo ambalo lilikubaliwa na
vyama hivyo vitatu.
Matamko hayo yamefanya suala la mgombea urais wa
Ukawa kugubikwa na giza nene, lakini kwa siku tatu Mwananchi imefuatilia
na kubaini kuwa mgombea ambaye yuko na hajatajwa rasmi kwa vyama hivyo
vinne ndiye anayechelewesha mchakato huo na amesababisha kuwapo na
hatari ya umoja huo kuparaganyika.
Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka ndani ya
vikao vya Ukawa vilivyoanza kufanyika takribani wiki mbili jijini Dar es
Salaam, zinaeleza kuwa licha ya viongozi wa vyama hivyo kumpata mgombea
wao wa urais katika kikao cha Julai 14 mwaka huu, walikwama kumtangaza
kutokana na CUF kutokuwapo kikaoni ikielezwa kuwa wanapinga maendeleo ya
mchakato huo.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa msimamo huo wa CUF
umetokana na utata ulioibuka katika kikao cha Ukawa cha Julai 11 na 14,
baada ya wagombea wawili kati ya watatu, kukubali mmoja wao agombee
urais, lakini chama chake kikasema kuwa kinachotakiwa ni Ukawa kutangaza
jina la chama kitakachotoa mgombea na si jina la mgombea.
Tayari Profesa Lipumba ameshachukua fomu za
kuwania urais kwa tiketi ya CUF, wakati Dk Kahangwa amechukua fomu
kuwania urais kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, huku mchakato wa Chadema ukiwa
haujaanza.
Habari hizo zinaeleza kuwa awali kulikuwa na
mvutano mkali kati ya Profesa Lipumba na Dk Slaa na kwamba katika kikao
cha Julai 11, Lipumba ambaye ni mwenyekiti wa CUF alikubali kumuachia Dk
Slaa agombee urais kupitia Ukawa, lakini inaonekana hata ndani ya
Chadema bado hawajaafikiana kuhusu jina la mgombea.
Hata hivyo, chama hicho kimeeleza kuwa jina la mgombea urais limeshapatikana na linasubiri muda muafaka.
“Tutamtangaza mgombea urais wa Ukawa ndani ya wiki
moja kama tulivyosema awali,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa
Chadema-Bara, John Mnyika jana.
Post a Comment Blogger Facebook