Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi imeliamuru Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC) kutouza au kupiga mnada mali za Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mpaka kesi ya msingi
itakapomalizika.
Shirika
hilo lilizichukua mali mbalimbali za kampuni za Mbowe ambaye pia ni
Mbunge wa Jimbo la Hai, wiki iliyopita kupitia mawakala wa kampuni ya
Fosters Auctioneers katika jengo lililopo makutano ya mitaa ya Mkwepu na
Indira Gandhi (Makunganya) jijini Dar es Salaam.
Hatua
hiyo ya NHC ilitokana na mgogoro wa muda mrefu, wakimtuhumu Mbowe
kushindwa kulipa deni la zaidi ya Sh. 1.3 bilioni, ikiwa jumla ya fedha
za kodi ya kupangishwa kwenye jengo hilo.
Kutokana
na mvutano huo, Mbowe alifungua kesi katika Mahakama Kuu, Kitengo cha
Ardhi, kupinga hatua ya NHC kumuondoa katika jengo hilo, pamoja na
kuchukua mali zake huku wakitangaza kuzipiga mnada baada ya siku 14
tangu kuzichukua.
Jana, Jaji Siyovelwa Mwangasi alitoa
zuio na kuiamuru NHC kutouza wala kupiga mnada mali hizo za Mbowe mpaka
mahakama hiyo itakapotolea uamuzi katika kesi ya msingi.
Katika kesi hiyo namba 722 ya mwaka 2016, Mbowe anawakilishwa na Mawakili Peter Kibatala na Omary Msemo.
Jaji
Mwangasi amesema kuwa, anakubaliana na maombi ya mlalamikaji na kutaka
mali hizo zisiuzwe hadi hapo mahakama itakapofanyia uamuzi kesi ya
msingi.
Hatua
hiyo inakuja baada ya upande wa NHC kupitia mawakili wake Aloyce Sekule
na Miriam Mungula kushindwa kuwasilisha hoja za msingi kueleza, ni
kwanini zuio hilo lisitolewe hadi hapo kesi ya msingi itakapoanza
kusikilizwa.
Awali,
mawakili wa NHC, walidai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza
maombi ya Mbowe kwa kuwa hakuna kesi ya msingi ambayo imefunguliwa,
hivyo maombi hayo yatupiliwe mbali.
Wakili Kibatala alijibu hoja hiyo kwa kusema, hatua ya kuwasilisha maombi hayo inalenga kubaini kama kweli Mbowe anadaiwa kodi ama la.
Kibatala alidai
kuwa mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, hivyo inaweza
ikatoa uamuzi wowote, na ndiyo maana wamewasilisha maombi hayo ili
itolewe amri ya muda ya kuzuia mchakato huo.
Miongoni
mwa hoja za Mbowe alizoziwalisha mahakamani hapo, ni pamoja na hoja
kuwa, yeye (Mbowe) na shirika hilo walikubaliana kwamba atalikarabati na
kulipanua jengo hilo kwa asilimia 100. Makubaliano ambayo yaliingiwa
mwaka 1997.
Amedai
kuwa katika makubaliano hayo yeye na NHC walikubaliana watamiliki jengo
hilo kwa pamoja kwa muda wa miaka 99, huku Mbowe katika mgawanyo wa
mapato akitakiwa kupata asilimia 75 na NHC ikitakiwa kupata asilimia 25.
Pia alieleza
kuwa katika makubaliano hayo, licha ya mwenendo wa kibiashara kutokuwa
mzuri, muda wote alikuwa akilipa asilimia hiyo 25, kwa mujibu wa
makubaliano yao.
Hivyo
kutokana na hatua ya NHC kuvunja mkataba huo kwa kumtoa kwenye jengo na
kuchukua mali zake, anaiomba mahakama iliamuru shirika hilo limlipe
fidia.
Mbowe aliondolewa kwenye jengo husika mnamo Septemba mosi kwa madai ya kushindwa kulipa deni la zaidi ya Sh. bilioni 1.3.
Mawakala
wa NHC walifika katika jengo hilo saa 12:30 asubuhi na wafanyakazi
zaidi ya 50 na kwenda moja kwa moja katika kampuni ya Free media pamoja
na ukumbi wa Bilcanas na kuchukua vifaa mbalimbali ikiwemo, meza, viti
na kompyuta.
Siku
chache baada ya kuondolewa kwa Mbowe katika jengo hilo, Rais John
Magufuli alilisifu shirika hilo kwa hatua hiyo na kulitaka lichukue
hatua kama hizo kwa wadaiwa wengine zikiwemo taasisi za umma
Post a Comment Blogger Facebook