0
MGOMBEA urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli, amewahakikishia wana-CCM na Watanzaia kwa ujumla kuwa mwaka huu, chama kitapata ushindi wa Tsunami na si wa kishindo wala kimbunga.

Dk Magufuli alisema hayo nje ya ofisi ya chama hicho mkoani Mtwara juzi alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama hicho ambapo alisisitiza kuwa wapinzani watapiga kelele sana, wataongea sana lakini ushindi kwa CCM ni lazima na upo pale pale.

Alisema ushindi huo unatokana na matawi yaliyoanguka ndani ya chama na kuhama na kwamba watu hao wameiacha CCM ikiwa safi na salama zaidi.

Alisema watu hao walikuwa wakitumia fedha nyingi kurubuni watu wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM ambapo chama kiliwakata na kukimbilia vyama vingine vya upinzani.

Aliwataka wana-CCM wasikatishwe tamaa na watu wa aina hiyo na badala yake washikamane, wawe kitu kimoja na kwamba mwaka huu, chama kitafanya kampeni za kisayansi.

Aidha, Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba alisema ni kazi rahisi kumnadi Dk Magufuli kutokana na vigezo na sifa alizonazo.

Mwigulu, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, alisema walioshindwa kwenye mchakato wa kura za maoni na kuhama ndani ya chama, hivi sasa wanahaha kutafuta urais wenyewe ambapo wanatoa mpaka hela ili kutafuta uongozi, lakini wataumbuka mapema.

Akizungumza na mamia ya wana-CCM waliojitokeza kumpokea katika hiyo ofisi ya chama ambapo alifika kwa ajili ya kuwasalimia na kuwashukuru kwa kumchagua kuwa mgombea na kumdhamini, Dk Magufuli aliwataka makada hao na Wtanzania kwa ujumla kutoyumba kwa kuwa Watanzania walio wengi bado wanakipenda Chama.

“Ushindi wa mwaka huu wala si wa kimbunga ni wa Tsunami, watapiga kelele sana, watakuja na propaganda nyingi sana, lakini ushindi wa CCM ni lazima. Ni lazima tupate ushindi wa rais, wabunge, wawakilishi na madiwani,” alisema.

Alisema walikuwa watu 42, wakati wakiomba kuteuliwa na chama hivi sasa, CCM ina kundi moja tu la ushindi.

“Hako ka tawi kamoja ndio kakameguka kwenda uko mbali, mti ambao unataka upate mbao zake nzuri matawi kudondoka chini ni vizuri ili upate mbao safi.

 “Lakini baada ya kudondoka hilo ni jambo la kawaida kwa chama kikubwa kama CCM.

"Hata ukiangalia tangu enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere wapo waliotoka wako akina Kambona walitoka na wengine walifukuzwa na wengine walijua watafukuzwa wakakimbia wenyewe kabla ya kufukuzwa kama hao,” alisema.

Alisema iwapo atachaguliwa kuongoza dola atapenda awe mtumishi wa watu, asiyekuwa na majivuno ili aweze kuwatumikia wananchi na atimize matarajio yao.

 Dk Magufuli alisema wakati wa kampeni ukifika zitafanyika za kistaarabu na kisayansi na kwamba zitakuwa za shina kwa shina, tawi kwa tawi, kata kwa kata, jimbo kwa jimbo, wilaya, mkoa na taifa.

Aliwataka wana-CCM wasimame imara kwani wananchi wengi wanakipenda Chama.

 Dk Magufuli akizungumzia uzoefu wake ndani ya CCM, alisema alikuwa mbunge katika kipindi chake cha miaka 20, ambapo vipindi viwli alipita bila kupingwa na alikuwa waziri kwa miaka 20 katika wizara mbalimbali.

Alisema anaifahamu vizuri Mtwara, Tanzania, CCM na kero za Watanzania anazifahamu vya kutosha hivyo akipewa nafasi watashudia wenyewe kasi ya utendaji kwa maendeleo ya taifa.

 “Nilichaguliwa na mkutano mkuu kutoka kila kona ya nchi kwa asilimia 87, wale walionichagua waliwakishia Watanzania wote. Niwahakikishie kuwa mwaka huu, tutashinda zaidi,” alisema.

Aliwataka wana-CCM katika umoja wao kutulia na kutoyumbishwa na maneno ya porojo kwa kuwa chama kinajiuliza kwa kile walichofanya kwa wananchi na si maneno matamu bila vitendo.

“Chama nakifahamu, shida za wana-CCM nazifahamu, matarajio yao nayafahamu, shida za wananchi nazifahamu hivyo kama nitachaguliwa nitawatumikia kwa uadilifu mkubwa ili kuwaletea maendeleo,” alisema.

Post a Comment Blogger

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();
 
Top