Showing posts with label NEWS. Show all posts
Showing posts with label NEWS. Show all posts

Wednesday, September 14, 2016

Serikali yatoa majibu ya hatua iliyofikia kuhusu viwanda ilivyobinafsisah




Serikali inatekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli la kuhakikisha viwanda vilivyobinafsishwa vinafanya kazi linatekelezwa tangu mwezi Novemba mwaka 2015.

Hayo yalibanishwa jana na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Manyoni Mhe. Yahaya Massare lililohusu utekelezaji wa ahadi ya Rais kuvirudisha viwanda vyote vilivyobinafsishwa lakini havifanyi kazi.

Waziri Mwijage alisema kuwa Serikali kupuitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji inaendelea na zoezi la kuchambua mikataba ya mauzo kwa viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo ama havifanyi vizuri au vimesimamisha uzalishaji kabisa.

Waziri alibainisha kuwa timu ya wataalamu toka Wizara ya Viwanda na Ofisi ya Usajili wa Hazina walifuatilia na kufanya tathimini kwa kutembelea kiwanda baada ya kiwanda hatua ambayo inasaidia kutafuta ufumbuzi wa matatizo yaliyopelekea kiwanda kutofanya kazi.

Aidha, Waziri Mwijage alisema kuwa uchambuzi wa mikataba ya viwanda hivyo unafanyika kwa ushirikiano na Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na Wizara za kisekta ikiwemo Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Nishati na Madini, pamoja na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Hata hivyo, Waziri Mwijage alisema kuwa katika kutekeleza ahadi hiyo ya Rais, Serikali imetwaa Kiwanda cha Chai Mponde kilichopo wilaya ya Lushoto mkoani Tanga ambacho mwekezaji amekiuka makubaliano ya mkataba.

Mbali na hayo, akijibu swali la Mbunge wa Tabora Mjini Mhe. Emmanuel Mwakasaka lililohusu mpango wa Serikali kujenga maabara ya kupima ubora na kiwango cha asali inayozalishwa hapa nchini.

Waziri Mwijage alisema kuwa Serikali inaendelea kuhimiza ujenzi wa viwanda nchini ikiwemo viwanda vya asali na kuhakikisha vinakuwa na maabara zinazoweza kupima viwango vya msingi.

Waziri Mwijage aliongeza kuwa kuhusu ujenzi wa maabara mkoani Tabora, Wizara itahakikisha wawekezaji wanaofuatilia ujenzi wa viwanda vya asali wanakuwa na maabara za kupima viwango vya msingi vya msingi na kuiachia TBS kuweka viwango vya kitaifa na kudhibiti viwango hivyo.

Na Beatrice Lyimo, MAELEZO, Dodoma

Rais Magufuli ampa shavu la nguvu aliyekuwa mkurugenzi NSSF Dk Ramadhani Dau


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 14 Septemba, 2016 amemuapisha Dkt. Ramadhani Kitwana Dau kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malaysia.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi, Dkt. Ramadhan Kitwana Dau alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF)

Mhe. Balozi Dkt. Ramadhani Kitwana Dau anajaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Malaysia Dkt. Aziz Ponary Mlima ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Wakati huo huo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli, amewaapisha Makatibu Tawala wa Mikoa mitatu aliowateua mwishoni mwa wiki iliyopita.

Walioapishwa ni  kwanza, Bw. Eliya Mtinangi Ntandu anayekuwa Katibu Tawala wa kwanza wa Mkoa wa Songwe ulioanzishwa rasmi Mwezi Februari 2016.

Pili, Bw. Adoh Stephen Mapunda anayekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara.

Bw. Adoh Stephen Mapunda anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Benedict Richard Ole Kuyan ambaye amestaafu.

Tatu, Bw. Tixon Tuliangine Nzunda anayekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa.

Bw. Tixon Tuliangine Nzunda anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Symthies Emmanuel Pangisa ambaye amestaafu.

Baada ya kuapishwa, Mhe. Balozi Ramadhani Kitwana Dau na Makatibu Tawala wote watatu wamekula Kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda na kushuhudiwa na Rais Magufuli.

Matukio yote yamefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU

Dar es Salaam

14 Septemba, 2016

Edward Lowassa ampongeza Rais Pombe Magufuli


Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa amempongeza Rais Magufuli kwa kuondoa urasimu katika taasisi za serikali na kusema hiyo itasaidia kurejesha utendaji kazi kwa ufanisi.

Lowassa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na mtangazaji wa BBC, John Nene nchi Kenya ambapo alisema urasimu umepungua na hili amejitahiidi lakini kuna mambo baadhi hayako vizuri.

Lowassa hakuwa tayari kusema ni mambo gani haswa hayakua yakienda sawa lakini alimkosoa Rais Magufuli kwa kile alichodaiwa kuwa analeta dalili za udikteta.

Lowassa alikuwa ni mpinzani mkuu wa Rais Magufuli katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 akigombea kupitia CHADEMA na kuungwa mkono na vyama vinavyounda UKAWA.

Amekosoa pia uamuzi wa serikali ya awamu ya tano kupiga marufuku maandamano, mikutano na vikao vya ndani vya vyama siasa huku vyombo vya habari vikifungiwa na wale wote wanamkosoa wakifikishwa mahakamani.

Akielezea Opersheni UKUTA, Lowassa alisema kuwa walipanga kuandamana ili kupinga dalili za udikteta alizoanza kuzionyesha Rais Magufuli.

Mwanamke ashikiliwa kwa kuiba mtoto wa mwezi mmoja


Jeshi la polisi mkoani Morogoro linamshikilia mwanamke mmoja, Anna Luambano (33) mkazi wa Kipawa jijini Dar es Salaam,kwa tuhuma za kuiba mtoto mchanga wa kike mwenye umri wa siku kumi,huko maeneo ya Kilimahewa katika Manispaa ya Morogoro.

Bungeni: Serikali kuanza kuwalipa wazee wa miaka 70 na kuendelea sh 20,000 kila mwezi


#BUNGENI:Serikali ipo mbioni kuanza kuwalipa wazee pensheni bila kujali shughuli waliyokuwa wakifanya siku za nyuma.
Naibu Waziri wa Ajira, Kazi na Vijana Antony Mavunde amesema kwa kuanzia wazee watakuwa wakilipwa shilingi elfu ishirini kwa mwezi na wataanza kulipwa wazee wenye umri wa miaka sabini na kuendelea.

Rais Magufuli amwapisha Dkt Dau pamoja na makatibu tawala wa mikoa mitatu ikulu jijini Dar es Salaam


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 14 Septemba, 2016 amemuapisha Dkt. Ramadhani Kitwana Dau kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malaysia.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi, Dkt. Ramadhan Kitwana Dau alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF)

Mhe. Balozi Dkt. Ramadhani Kitwana Dau anajaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Malaysia Dkt. Aziz Ponary Mlima ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Wakati huo huo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli, amewaapisha Makatibu Tawala wa Mikoa mitatu aliowateua mwishoni mwa wiki iliyopita.

Walioapishwa ni  kwanza, Bw. Eliya Mtinangi Ntandu anayekuwa Katibu Tawala wa kwanza wa Mkoa wa Songwe ulioanzishwa rasmi Mwezi Februari 2016.

Pili, Bw. Adoh Stephen Mapunda anayekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara.

Bw. Adoh Stephen Mapunda anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Benedict Richard Ole Kuyan ambaye amestaafu.

Tatu, Bw. Tixon Tuliangine Nzunda anayekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa.

Bw. Tixon Tuliangine Nzunda anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Symthies Emmanuel Pangisa ambaye amestaafu.

Baada ya kuapishwa, Mhe. Balozi Ramadhani Kitwana Dau na Makatibu Tawala wote watatu wamekula Kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda na kushuhudiwa na Rais Magufuli.

Matukio yote yamefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
14 Septemba, 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Bw. Tixon Nzunda kuwa Katibu Tawala wa mkoa wa Rukwa, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Bw. Eliya Ntandu kuwa Katibu Tawala mkoa wa Songwe, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na Balozi mpya wa Tanzania nchini Malaysia Dkt. Ramadhani Dau mara baada ya tukio la uapisho Ikulu jijini Dar es Salaam.

Tuesday, September 13, 2016

Waziri mkuu Kassim Majaliwa awataka Watanzania kudumisha amani



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini zote kutumia nyumba za ibada kuwahamasisha waumini wao umuhimu wa kulinda na kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.

Amesema Serikali itahakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa nchini ili Watanzania wawe na uhakika wa kuendelea kufanya kazi zao za kuwaingizia kipato na kuwaletea tija.

Waziri Mkuu ametoa wito huo jana(Jumatatu, Septemba 12, 2016) wakati akizungumza na waumini wa dini ya kiislam mara baada ya kumaliza kuswali sala ya Eid El Haji kwenye viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke Dar es Salaam.

“Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote nchini. Wito wangu kwa viongozi wa dini msisitize waumini juu ya utunzaji wa amani pamoja na kukemea vitendo viovu ili Taifa lizidi kusonga mbele,” amesema.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amewasisitiza wananchi kuendelea kuwaombea mahujaji waliopo mjini Makka na Madina nchini Saudi Arabia wakiendelea na ibada ya hijja warudi salama.

Pia Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kuwasaidia kwa hali na mali watu waliokumbwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera ambako jumla ya watu 16 walifariki na wengine 253 kujeruhiwa.

Pia maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1264 zikipata nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma

Awali akisoma hutuba ya Eid viwanjani hapo Sheikh Nurdin Kishki alisema dini ya Uislamu ni dini ya amani hivyo amewaomba waislamu kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani yakiwemo mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Sheikh Kishki amesema ni muhimu watu kulinda amani kwani ikitoweka ni vigumu kuirudisha, alitolea mfano wanachi wa nchi za Libya na Misri ambazo hadi sasa zimeshindwa kuirudisha.

Amesema mtu yeyote anayejihusisha na vitendo vya uwamwagaji wa damu, kudhulumu mali za watu pamoja na kuwavunjia heshima wenzake atakuwa ameangamia, hivyo amewataka Watanzania hususan wakazi wa Temeke kujiepusha navyo.

“Temeke sasa inaongoza kwa matukio ya mauaji, wanaua hadi walinzi. Askari wameuawa bila hatia, jambo hili linasikitisha sana. Watu waliokuwa wanafanya kazi ya kulinda raia na mali zao wanauawa bila ya hatia! Ameongea kwa masikitiko na kuwaomba Watanzania wajiepuszhe na vitendo hivyo.

Katika hatua nyingine Sheikh Kishki ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuonyesha dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo hivyo amewaomba wananchi wawe mstari wa mbele kutoa ushirikiano ili taifa liweze kusomba mbele.

“Ndugu zangu tumepewa heshima kubwa leo kuswali Eid na Mheshimiwa Waziri Mkuu tena amekuja hapa kwenye viwanja hivi vya Mwembe Yanga, hii inaonyesha ukaribu wa viongozi wetu wakuu kwa wananchi wao hususan wa hali ya chini,” amesema.

Majambazi yavamia magari ya mnadani na kumuua dereva mmoja kwa Risasi


Majambazi wapatao 10 juzi usiku walivamia magari mawili yaliyobeba wafanyabiashara waliokuwa wakitokea mnadani na kumuua kwa risasi, dereva aliyegoma kuwapa fedha na simu.

Dereva huyo, Chrispin Inyangwe (40) alipigwa risasi ya mgongoni alipojaribu kupambana nao.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana eneo la katikati ya vijiji vya Miula na Kalundi vilivyopo Kata ya Kipande wilayani Nkasi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema wafanyabiashara hao walikuwa wakitokea mnadani na walipofika eneo hilo walikuta mawe yamepangwa barabarani kuzuia magari.

Alisema baada ya kuona mawe hayo, magari hayo yalilazimika kusimama na ndipo majambazi hao waliokuwa na silaha za moto, mapanga na marungu walipoibuka na kufyatua risasi hewani na baadaye kutaka wafanyabiashara hao wasalimishe fedha na simu zao za mkononi.

Kamanda huyo alisema baadhi ya wafanyabiashara walisalimisha fedha na simu zao, na waliokataa walishambuliwa.

Inasemekana kwamba Inyangwe ambaye alikuwa dereva wa gari aina ya Mitsubishi Canter alikaidi kutoa fedha na kutaka kupambana nao, ndipo watu hao waliokuwa na bunduki aina ya SMG walipomfyatulia risasi iliyompata mgongoni na kufariki dunia papo hapo.

Kitendo hicho kiliwafanya wafanyabiashara wengine waliokuwa wakikataa kutoa fedha, kuzisalimisha sambamba na simu zao, ndipo majambazi hao walipowaachia na kukimbia.

Watu 19 waliojeruhiwa walipelekwa Hospitali ya Mkoa mjini Sumbawanga. Kamanda Kyando alisema majeruhi 12 waliruhusiwa kurejea nyumbani na wengine saba wanaendelea na matibabu na kwamba polisi wanaeendelea na msako wa watu hao.

Rais Kenyatta, Mbowe watoa msaada kwa waathirika wa tetemeko la ardhi kagera



Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyatta amezungumza kwa njia ya simu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kumpa pole kufuatia vifo vya watu na madhara mengine yaliyotokana na tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

Tetemeko lililotokea mkoani Kagera Septemba 10, limesababisha vifo vya watu 16, kuacha watu 253 wakiwa na majeraha mbalimbali ya mwili na nyumba zaidi ya 1000 zikiwa zimebomolewa.

Taarifa kutoka kwa msemaji wa Rais Kenyatta alisema kuwa Rais Kenyatta ameahidi kutoa msaada wa mabati, blanketi na magodoro ili kuwasaidia watu wasio na makazi mkoani Kagera.

Msaada huo utasafirishwa kwa ndege na Jeshi la Kenya Jumanne  hii Septemba 13  hadi mkoani Kagera ambapo ndipo palipopata madhara.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, jana aliwasili mjini Bukoba kuwatembelea waathirika na kutoa mkono wa pole kwa kaya 16 za waliofikwa na misiba kutokana na tetemeko hilo la ardhi.

Mbowe alitoa shilingi milioni 2.1 kwa ajili ya kaya hizo, mifuko 150 ya sementi kwa familia 15 ambazo zimepoteza makazi ambapo kila kaya ilipata mifuko 10.

Mwenyekiti huyo wa Chadema aliambatana na viongozi wengine wa  Chadema mjini humo pamoja na Mbunge wa Bukoba Mjini, Willfredy Rwakatale na Mbunge wa viti maalum (CUF), Saverina Mwijage, walitoa sukari sukari kilo 25 pamoja na mchele kilo 50.

“Ndugu zangu, tukio hili sio la Serikali au chama chochote, ni jambo la kitaifa. Serikali inapaswa kutenga fungu kubwa kwa ajili ya kuisaidia jamii,” Mbowe anakaririwa.

Akiwa katika shule ya Sekondari ya Ihungo iliyobomolewa na tetemeko la ardhi na kusababisha wanafunzi kukosa madarasa ya kusomea, Mbowe ambaye pia alisoma katika shule hiyo alitoa misaada mbalimbali.

Rais John Magufuli alilazimika kuahirisha safari yake ya kuhudhuria kuapishwa kwa Rais wa Zambia, Edgar Lungu kutokana na janga la tetemeko la ardhi, badala yake alimtuma Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kumuwakilisha.

Wakurugenzi wapya 13 waapishwa , watakiwa kufuatilia maagizo ya viongozi


Wakurugenzi wapya 13 wa halmashauri wameapa kulinda maadili na kukabidhiwa majukumu ya kufuatilia maagizo ya Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, kwenye maeneo yao na kutoa mrejesho wa hatua za utekelezaji wake. 

Kiapo hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angela Kairuki aliyewataka kutilia mkazo ufuatiliaji wa maagizo na kupambana na tatizo la watumishi hewa ambao idadi yao imefikia 17,102 waliogundulika katika kipindi cha kuanzia Machi mpaka sasa. 

Wakurugenzi hao walioteuliwa hivi karibuni na Rais, John Magufuli waliapishwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene katika ukumbi wa Tamisemi mjiniDodoma.

 Akizungumza mara baada ya kiapo hicho, waziri Kairuki aliwataka wakurugenzi hao kutekeleza matamko yote yanayotolewa na viongozi wa ngazi za juu serikalini, kwa kutoa mrejesho wa utekelezaji wake. 

Kairuki aliwataka kufanya kazi kwa bidii ili wawatumikie wananchi wanaowaongoza. 

Alisema katika ziara nyingi alizozifanya, amekuta wakurugenzi hawafuatilii matamko yanayotolewa na viongozi wa ngazi za juu serikalini katika maeneo yao. 

“Hata kwa wale ambao wanayafuatilia huwa hawatoi mrejesho wa hatua zilizofikiwa katika kutekeleza matamko hayo, hivyo ninawaomba mkayatekeleze maagizo na kurudisha mrejesho kwa kiwango kinachotakiwa,” alisema Kairuki. 

Pia, aliwataka wakurugenzi hao kwenda kusimamia fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali hadi senti ya mwisho, ili kuhakikisha inatekelezwa kwa asilimia 100. 

Alisema kuna baadhi ya miradi ya maendeleo, inatekelezwa kwa fedha za Serikali na wakati huo huo inatumia fedha za wafadhili. 

Waziri Kairuki aliwataka wakurugenzi hao kuhakikisha kuwa miradi yote inayotumia fedha za Serikali inasimamiwa ipasavyo. 

“Utakuta mradi mmoja unafadhiliwa na pia unatumia fedha za Serikali, kwa hiyo wafadhili wakija kukagua wanaonyeshwa jengo likiwa limekamilika na Serikali nayo ikija kukagua inaonyeshwa jengo hilohilo. Nataka mkasimamie fedha zote za Serikali kwenye mamlaka zenu,” alisema Kairuki. 

 Alisema kuna baadhi ya maeneo ambako fedha za Tasaf (mpango wa kunusuru kaya maskini), zimetumika kujengea maabara na kununulia madawati kinyume na malengo yaliyokusudiwa. 

Pia, aliwataka kuhakikisha kuwa hatua kali za kinidhamu zinachukuliwa kwa wakati kwa watumishi waliosimamishwa kazi katika kipindi cha miezi sita na si zaidi ya hapo. 

Alisema mtumishi aliyechukuliwa hatua za kinidhamu ikiwamo kufukuzwa au kusimamishwa kazi, mchakato wake wote ufanyike ndani ya miezi sita. 

Aliwataka pia wakurugenzi hao kufuata maadili ya viongozi wa umma, kwani wakikiuka watafikishwa kwenye baraza la maadili ya viongozi wa umma ambalo kwa sasa limeongezewa meno. 

Waziri Kairuki aliwataka wakurugenzi hao kusimamia suala la rasilimali watu, kwani utafiti ulionyesha kuwa asilimia 80 hadi 90 ya watumishi wa umma ni watoro.

Alisema katika baadhi ya maeneo kuna wakaguzi na waratibu wa elimu wa kata, lakini hawatembelei shule zao kuona kama walimu wanahudhuria shuleni au la. 

Kadhalika, aliwataka wakurugenzi hao kuachana na tabia ya kuwatumia viongozi wa Serikali walioko chini yao, kama vile watendaji wa kata, vijiji na wenyeviti wa vijiji kuwalimia mashamba yao.

Alisema watakaobainika kufanya vitendo hivyo, watachukuliwa hatua kali za kinidhamu. 

Waziri Simbachawene aliwataka wakurugenzi hao kwenda kuchapa kazi bila kumwonea yeyote. Aliwaambia kuwa kukusanya  mapato kiwe ni kipaumbele chao cha kwanza, kwani kipimo cha mamlaka yoyote kujitegemea ni uwezo wake wa kukusanya mapato. 

Aliwataka wakurugenzi hao kuhakikisha kuwa wanawatembelea watumishi wao wote ili kujua penye upungufu, idadi yao na hata ikiwezekana kuwajua kwa majina yao. 

Wakurugenzi walioapishwa jana ni Godwin Kunambi (Dodoma) Elias Ntiruhungwa (Tarime), Mwantumu Dau (Bukoba) na Frank Bahati (Ukerewe) Wengine ni Hudson Kamonga (Mbulu), Mwailwa Pangani (Nsimbo), Godfrey Sanga (Mkalama), Yusufu Semuguruka (Ulanga), Bakari Mohamed (Nachingwea), Juma Mnweke (Kibondo), Butamo Ndalahwa (Moshi), Waziri Mourice (Karatu) na Fatma Latu (Bagamoyo). 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. George Simbachawene.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Angella Kairuki akiongea Wakurugenzi wapya mara baada ya kuapishwa jana mjini Dodoma. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. George Simbachawene. Kushoto kwa Simbachawene ni  Mkurugenzi mteule wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilimanjaro Bi. Butamo Nuru Ndalahwa

Serikali yasema waliosoma shahada za sayansi watapewa mafunzo ya muda mfupi ya ualimu ili kukabiliana na upungufu wa walimu

u

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma

Serikali imeanza kupanga walimu wa sayansi moja kwa moja katika shule badala ya Halmashauri kama ilivyokuwa awali ili kuleta uwiano sawa wa walimu katika shule mbalimbali nchini.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Suleman Jaffo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Muleba Prof. Anna Tibaijuka lililohusu mkakati wa Serikali katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa walimu.
Naibu Waziri Jaffo amesema kuwaSerikali imeandaa mkakati wa kuwaajiri wahitimu wa shahada za sayansi ambazo siyo za ualimu baada ya kuwapa mafunzo ya muda mfupi kuhusu mbinu za ufundishaji na maadili ya ualimu ili kukabiliana na changamoto ya walimu wa sayansi nchini.
Naibu Waziri Jaffo amesema kuwa tayari kibali kimeombwa katika Ofisi ya Rais Utumishi kwa ajili ya utekelezaji huo, ambapo Serikali imepanga kuajiri walimu wastaafu wenye uwezo wa kufundisha waliokuwa wanafundisha masomo ya sayansi kwa mkataba ili kupunguza pengo lililopo.
Aidha, Naibu Waziri Jaffo amebainisha kuwa Serikali inafanya tathimini ya mahitaji ya walimu wa masomo ya sanaa kwa kila Halmashauri ili kubaini maeneo yenye ziada na yenye upungufu ili kusawazisha.
“Mpango wa Serikali uliopo ni kuwahamasisha walimu wa ziada wa masomo ya sanaa kwenda kufundisha katika shule za msingi ndani ya Halmashauri husika, ambapo kabla ya kuanza utekelezaji wa mabadiliko haya Serikali itatoa waraka maalumu kwenda katika Halmashauri zote nchini” amefafanua Naibu Waziri huyo.
Akizungumzia kuhusu utaratibu wa mafunzo ya walimu Mhe. Jaffo amesema kuwa Halmashauri moja haiwezi kuwa na mfumo wa peke yake wa kuandaa walimu hali ambayo iltakuwa ni vigumu kuthibiti ubora wa mafunzo hayo kwa walimu.
Hata hivyo amesema kuwa Serikali itaendelea kuongeza udahili wa walimu wa sayansi katika vyuo vya ualimu kadri watakavyojitokeza ili kukidhi mahitaji yaliyopo

Wanafunzi wawacharaza viboko walimu wao., mmoja ang'olewa meno matano mwingine ngeu kichwani


Waziri wa Elimu, Prof Joyce Ndalichako

Wawanafunzi wa Kidato cha Sita Shule ya Sekondari Usevya wilayani Mlele Mkoa wa Katavi, wanadaiwa kuwashambulia kwa kuwacharaza viboko walimu wao wawili miongoni mwao akiwemo Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Makonda Ng’oka “Membele'‘ (34) ambaye ameng’olewa meno matano kwa kipigo hicho.

Walimu hao wawili wamedai kuwa hawako tayari kuendelea kufundisha katika shule hiyo huku wakisisitiza kuwa ni fedheha kwao kucharazwa viboko na wanafunzi wao wenyewe ambapo Mwalimu Gabriel Kambona aliachwa na ngeu kichwani.

Mei mwaka huu, Ng’oka “Membele” alifikishwa katika Mahakama ya Mkoa wa Katavi kwa tuhuma za kumlawiti mwanafunzi wake akidaiwa kutenda kosa hilo kati ya Novemba 2015 na Aprili mwaka huu.

Ilisemekana kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa Makamu Mkuu huyo wa shule hiyo kulifuatia wanafunzi wa kiume wanaosoma Kidato cha Tano sasa wako Kidato cha Sita katika shule hiyo kumkataa na kutishia kuandamana kupinga vitendo vyake vya kuwalawiti wanafunzi wake.

Wanafunzi hao walidai kuwa mwalimu huyo amekuwa akiwalawiti baadhi yao ikiwa ni adhabu mbadala wanapobainika kufanya makosa shuleni hapo.

Hata hivyo, baada ya kutopatikana ushahidi wa kumtia hatiani Ng’oka, Julai 27, mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Mpanda ilimwachia huru.

Mwalimu Ng’oka aliripoti kwenye kituo chake cha kazi shuleni Usevya Agosti Mosi mwaka huu ambako kurejea kwake shuleni hapo kunadaiwa kuamsha hasira kwa baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Sita wakidai hawapo tayari kumwona mwalimu huyo na familia yake shuleni hapo.

Akizungumza na wanahabari jana mjini hapa, Ng’oka alidai kuwa hayuko tayari kuendelea kufundisha kwenye shule hiyo akihofia usalama wake na kutokana na kipigo alichokipata cha kushambuliwa na baadhi ya wanafunzi wake wa kidato cha tano na cha sita wakati akiwa nyumbani kwake na familia yake.

 Akisimulia mkasa huo, alisema Agosti 12, mwaka huu usiku alikuwa nyumbani kwake shuleni hapo pamoja na familia yake pamoja na mwalimu mwenzake, Gabriel Kambona aliyekuwa amemtembelea.

“Ghafla, saa mbili usiku nikiwa maliwatoni nikioga lilitokea kundi la wanafunzi wa kidato cha tano na sita wakiwa na silaha za jadi kama vile fimbo, marungu, mawe na matofali na kuanza kuishambulia familia yangu pamoja na mwalimu Kambona,”alieleza na kuongeza kuwa alilazimika ‘kuchomoka’ bafuni baada ya kusikia mayowe yaliyokuwa yakipigwa na familia yake wakiomba msaada. Alipofika sebuleni alishuhudia wanafunzi hao wakiishambulia familia yake kwa kuwacharaza viboko.

“Ndipo walinigeukia na kuanza kunishambulia kwa kunipiga kwa marungu na fimbo hadi nikapoteza fahamu nilizinduka nikiwa nimelazwa kwenye Kituo cha Afya Usevya na kubaini kuwa nimepoteza meno yangu matano huku nikiwa nimejeruhiwa vibaya kichwani. Baadaye nilihamishiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ambako nililazwa wiki moja na nusu kwa matibabu na sasa nimepewa rufaa niende Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar kwa matibabu zaidi,”alieleza.

Alidai kuwa uhasama baina yake na wanafunzi hao umedumu kwa muda mrefu, lakini anashangaa uongozi wa Halmashauri ya Mpimbwe na Wilaya ya Mlele umeshindwa kumpangia kituo kingine cha kazi na kuchukua hatua yoyote kwa wanafunzi hao licha ya kupeleka majina yao kwa kuwa anawafahamu wote waliohusika.

Mwalimu Kambona alidai kuwa hayuko tayari kuendelea kufundisha kwenye shule hiyo kwamba kitendo cha kupigwa na wanafunzi wake kimemfedhehesha.

Kwa mujibu wa mwalimu huyo, walimu wa shule hiyo waliketi baada ya kutokea kwa tukio hilo, na walifikia maamuzi kuwa wanafunzi wote waliobainika kushiriki kuwashambulia walimu wao wasimamishwe shule akidai kuwa uongozi wa Halmashauri ya Mpimbwe na Wilaya ya Mlele ulipinga.

“Nimeandika barua ya kuomba uhamisho kwani nia aibu kwangu kuendelea kufundisha wanafunzi ambao wamenishambulia na kunitoa ngeo kichwani ….. siku hiyo ya tukio niliibiwa simu mbili za kiganjani lakini jana nimefanikiwa kuikamata simu moja kwa mwanafunzi wa kidato cha tano anayeitwa , Alex Maiko Makona na tayari amemfikisha katika Kituo cha Polisi cha Usevya,” alidai.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Katavi, Gregori Mshota alisema tayari chama chake kimeanza kuwasiliana na uongozi wa Halmashauri ya Mpimbwe na uongozi wa Wilaya ya Mlele ili kuhakikisha mwalimu huyo anakuwa salama.

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Katavi, Ernest Hinju alidai kuwa suala hilo lipo ofisini kwake na wameanza kulitafutia ufumbuzi. “Jambo hili linahitaji ushirikishwaji wa vyombo mbalimbali ikiwemo Bodi ya Shule ya Sekondari ya Usevya,” alieleza.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa katika ziara mkoani Katavi mwezi uliopita, mke wa mwalimu Ng’oka alitinga kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini Maji Moto akiwa na bango lenye malalamiko ya kutishiwa usalama wa maisha wa familia yake, na Waziri Mkuu alimwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa kushughulikia malalamiko hayo.

Waziri mkuu Kassim Majaliwa apokea zaidi ya sh. bil. 1.4 kwaajili ya maafa ya tetemeko Kagera




WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea michango wa zaidi ya sh. bilioni 1.4 kutoka kwa mabalozi wa nchi za nje nchini Tanzania na Jumuia ya Wafanyabiashara wa Kitanzania kwa ajili ya kusaidia wananchi waliothirika na tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera.

Tetemeko hilo lilitokea Jumamosi, 10 Septemba, 2016 na kusababisha vifo vya watu 17 hadi leo na wengine 253 kujeruhiwa. Pia limesababisha maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,264 zikipata nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.

Akizungumza katika hafla ya uchangishaji fedha kwa ajili ya kusaidia wahanga hao jana Jumanne, 13 Septemba, 2016 Waziri Mkuu aliwashukuru kwa michango yao ya fedha na vifaa vya ujenzi ikiwemo mifuko 2,800 ya saruji. Amesema tetemeko hilo ni kubwa na halijawahi kutokea nchini.

Alisema tetemeko hilo limesababisha Serikali kuzifunga shule zake mbili za sekondari za Nyakato na Ihungo kati ya nne zilizoathirika vibaya na tetemeko hilo.

“Serikali itajitahidi kuhakikisha inarejesha miundombini iliyoharibiwa na tetemeko hilo katika kipindi kifupi ili wanafunzi na wananchi wengine waweze kuendelea na shughuli zao za kawaida,” alisema.

Waziri Mkuu alisema katika kuhakikisha suala hilo linashughulikiwa haraka tayari Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Muhagama yuko mkoani Kagera akiongoza kitengo cha maafa kufanya thamnili kujua athari zilizosababishwa na tetemeko hilo.

Mawaziri wengine walioko mkoani Kagera wakiendelea kufanya tathmini hiyo ni pamoja na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako.

Alisema Kamati ya Maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Kamati ya Maafa ya mkoa wa Kagera imefungua akaunti maalumu katika benki ya CRDB kwa ajili ya kupokea michango kutoka kwa watu mbalimbali. Namba za akaunti hiyo ya Kamati ya Maafa ya Kagera ni CRDB 0152225617300.

Pia Waziri Mkuu aliwapongeza na kuwashukuru waheshimiwa Wabunge kwa kuamua kutoa posho zao za kikao cha jana kwa ajili ya kuchangia wahanga wa tetemeko hilo na kuwaomba wananchi wengine kujitokeza na kutoa michango yao.

Wakati huo huo viongozi wa makampuni ya mafuta ya GBP, Oil Com na Moil wameahidi kujenga shule mbili za Nyakato na Ihungo ambazo sehemu kubwa ya miundombinu yake imeharibika vibaya. Shule hizo zitajengwa katika kipindi cha siku 30.

Hafla hiyo iliyoongozwa na Waziri Mkuu ilihudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Suzan Kolimba na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi, Dk. Aziz Mlima.

Post Labels