Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyatta amezungumza kwa njia ya simu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kumpa pole kufuatia vifo vya watu na madhara mengine yaliyotokana na tetemeko la ardhi mkoani Kagera.
Tetemeko lililotokea mkoani Kagera Septemba 10, limesababisha vifo vya watu 16, kuacha watu 253 wakiwa na majeraha mbalimbali ya mwili na nyumba zaidi ya 1000 zikiwa zimebomolewa.
Taarifa kutoka kwa msemaji wa Rais Kenyatta alisema kuwa Rais Kenyatta ameahidi kutoa msaada wa mabati, blanketi na magodoro ili kuwasaidia watu wasio na makazi mkoani Kagera.
Msaada huo utasafirishwa kwa ndege na Jeshi la Kenya Jumanne hii Septemba 13 hadi mkoani Kagera ambapo ndipo palipopata madhara.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, jana aliwasili mjini Bukoba kuwatembelea waathirika na kutoa mkono wa pole kwa kaya 16 za waliofikwa na misiba kutokana na tetemeko hilo la ardhi.
Mbowe alitoa shilingi milioni 2.1 kwa ajili ya kaya hizo, mifuko 150 ya sementi kwa familia 15 ambazo zimepoteza makazi ambapo kila kaya ilipata mifuko 10.
Mwenyekiti huyo wa Chadema aliambatana na viongozi wengine wa Chadema mjini humo pamoja na Mbunge wa Bukoba Mjini, Willfredy Rwakatale na Mbunge wa viti maalum (CUF), Saverina Mwijage, walitoa sukari sukari kilo 25 pamoja na mchele kilo 50.
“Ndugu zangu, tukio hili sio la Serikali au chama chochote, ni jambo la kitaifa. Serikali inapaswa kutenga fungu kubwa kwa ajili ya kuisaidia jamii,” Mbowe anakaririwa.
Akiwa katika shule ya Sekondari ya Ihungo iliyobomolewa na tetemeko la ardhi na kusababisha wanafunzi kukosa madarasa ya kusomea, Mbowe ambaye pia alisoma katika shule hiyo alitoa misaada mbalimbali.
Rais John Magufuli alilazimika kuahirisha safari yake ya kuhudhuria kuapishwa kwa Rais wa Zambia, Edgar Lungu kutokana na janga la tetemeko la ardhi, badala yake alimtuma Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kumuwakilisha.
Post a Comment Blogger Facebook