HAKUNA mwanzo usiyokuwa
na mwisho! Huu ni usemi pekee ambao umejidhihirisha kwa Mkurugenzi wa
Endless Fame Production na mbunge mtarajiwa wa Viti Maalum mkoani
Singida kwa leseni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wema Isaac Sepetu baada
ya kumwangukia aliyekuwa shostito wake, Kajala Masanja ‘Kay’.
MWISHO WA MATUSI?
Wema na Kajala wamekuwa na bifu zito
lililokuwa likichukua sura mpya kila kukicha kufuatia wawili hao
kutokusameheana, kutukanana na kukashifiana ambapo Wema alifikia hatua
ya kumwita mwenzake ‘bogasi’ na yeye (Kajala) akamwita chizi.
Tukio la Wema kujishusha na kutoa kauli
ya kusema yuko tayari kumsamehe Kajala aliitoa mbele ya mwandishi wetu,
Julai 15, mwaka huu ndani ya Ofisi za gazeti hili, Bamaga-Mwenge jijini
Dar.
WEMA AFUNGUKA
Wema alifunguka hayo baada ya kuulizwa
hatima ya bifu lake na Kajala ambapo alisema kwa sasa yupo tayari
kabisa kumsamehe Kajala ambapo aliapa kwamba hata ikitokea wakutane
popote hawezi kumuonyeshea kinyongo cha aina yoyote.
Alisema pamoja na kushindwa kukutana na Kajala kwa muda mrefu lakini nafsi yake imeshamsamehe na imemuongoza kufanya hivyo.
Wema alisema kuwa kila jambo lina mwisho
wake, hivyo amekaa chini na kufikia uamuzi huo ambao anaamini kabisa
hapa duniani hakuna mtu asiyekuwa na moyo wa huruma.
Aliongeza kuwa pamoja na yote
yaliyotokea awali, hana budi kuyapuuzia kwa sasa, hivyo yuko tayari
kukutana na kukaa na Kajala kwani moyoni hana kinyongo chochote.
SINA TATIZO NA KAJALA
“Kiukweli kabisa nimeshamsamehe Kajala, sina tatizo naye, hivyo muda wowote akinihitaji kwa lolote sina kinyongo kabisa.
“Nimefikiria kwa kina, nikaona sina
sababu ya kuendelea kuwa na chuki naye na kupitia hilo namuomba Mungu
aendelee kuniongoza ili nifute kabisa hilo wazo la chuki moyoni.
“Nipo radhi kukutana naye mahali popote
pale endapo atanihitaji au mimi nitakapomuhitaji nitamtafuta,”
alifunguka staa huyo na kuongeza:
KUTOKA MOYONI
“Najua itakuwa ngumu sana kwa watu
kuniamini kwa sababu hapo nyuma kulikuwa na mambo mengi kati yetu,
naendelea kuwatoa wasiwasi kwa kuwaambia tena kuwa tayari moyo wangu
umeshamsamehe Kajala na nimejishusha kwa kila hali kwake.
“Nipo radhi kukutana naye mahali popote tukaongee ili wale wanaohisi sijamsamehe waamini hilo.”
Baada ya paparazi wetu kuhakikishiwa
taarifa hiyo na Wema kwa kauli za kumsamehe zaidi ya mara moja huku
akionyesha unyenyekevu na kujishusha kwa asilimia mia, alimtafuta Kajala
ili kujua moyoni mwake ana nini juu ya Wema.
KAJALA ROHO KWATU
“Kwanza nashukuru kusikia hivyo, binafsi
sina tatizo na hilo, kikubwa namshukuru maana nimekuwa nikimuomba Wema
kupitia sehemu mbalimbali ili tumalize tofauti zetu lakini alikuwa
akikataa, ila kama mwenyewe anasema yupo tayari tuyamalize, kwangu ni
furaha.
“Nimekuwa nikipigania hilo kila kukicha,
sasa naamini Mungu atakuwa amesikia kilio changu kwa mara nyingine,
napenda kusema sina tatizo lolote katika hilo,” alisema Kajala.
WEMA ACHUKUA FOMU YA UBUNGE
Msamaha huo umekuja siku moja kabla ya
Wema kuchukua fomu ya kuwania Ubunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida
Mjini kupitia CCM ambapo juzi Julai 15, mwaka huu alichukua fomu na
anatarajia kuirejesha kesho Jumapili.
Post a Comment Blogger Facebook