0
Arusha. Wazee wa kimila wa jamii ya wafugaji wa Kimaasai (Malaigwanan) kutoka Wilaya ya Monduli wamemuomba waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa kubaki na kuendelea kuwa kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa sababu ndicho kilichomlea na anakijua.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Monduli kwa niaba ya Malaigwanan, Mzee Joseph Mesopiro kutoka Kata ya Sepeko wilayani humo alisema viongozi wa mila wanakusudia kutuma ujumbe maalumu kwa Lowassa kumshauri asihame CCM kama baadhi ya watu aliowaita wapambe wanavyomshauri.
“Sote Monduli tumesononeka kwa jinsi vikao vya chama vilivyomtendea mbunge wetu. Bado tunampenda kama ambavyo tunakipenda chama chetu. Tunaamini ataendelea kubaki CCM na kupigania ushindi wa chama katika uchaguzi ujao,” alisema Mzee  Mesopiro
Alizungumza hayo wakati wa hafla ya kuchukua fomu na kuomba kuteuliwa na CCM kugombea ubunge Jimbo la Monduli, mwanasiasa wa siku nyingi Loata Sanare.
Kwa upande wake Laigwanan Julius Laizer kutoka Kata ya Moita, alisema licha ya mizengwe iliyotawala vikao vya uteuzi vya CCM vilivyomalizika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha ufa miongoni mwa viongozi na wanachama, bado anaamini chama hicho kitaendelea kubaki imara hata kama baadhi ya watu watakihama.  “Kama viongozi tuliolelewa na kukuzwa na CCM, tunaamini chama hiki kitaendelea kuwa imara na hatuko tayari kukubali ushawishi wowote wa kututaka tuhamie upinzani,” alisema Laizer.
Mwenyekiti wa CCM, Kata ya Lepurko wilayani Monduli, Njoput Alami alibeza taarifa za kushawishi watu kuhama CCM kwa kisingizio Lowassa kukatwa akiziita ni kelele za wapambe wanaohofia kukosa fursa walizozitarajia iwapo Lowassa angeteuliwa kuwa mgombea wa CCM.
Akizungumzia taarifa za wanaCCM wilayani Monduli kughadhabika na kutishia kukihama chama hicho kutokana na Lowassa kukatwa, Katibu wa CCM Wilaya ya Monduli, Elisante Kimaro alikiri baadhi ya wanachama kuchana kadi na kuchoma bendera za chama hicho, lakini akasema ni idadi ndogo ikilinganishwa na wanachama waliopo wilayani humo.
 “Kuna taarifa za kadi na bendera za CCM kuchomwa moto katika baadhi ya maeneo kama Migungani, Mto wa Mbu, Makuyuni na Nalaarani. Tunaendelea kukusanya taarifa sahihi na kufanya tathmini ya matukio hayo,” alisema Kimaro.


Post a Comment Blogger

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();
 
Top