Dar es Salaam. Kauli ya Rais wa Awamu ya tatu,
Benjamin Mkapa ya kutaka wajumbe wa Halmashauri Kuu kupiga kura na wale
wasioafiki watoke, ndiyo inaelezwa kuwa ilimaliza mzozo ulioibuka baada
ya jina la Edward Lowassa kuenguliwa mapema.
Kikao hicho kilichofanyika Julai 10 kilionekana
kuelekea kukumbwa na mtafaruku baada ya wajumbe kumpokea Rais Jakaya
Kikwete kwa wimbo wa kuonyesha kuwa wana imani na waziri huyo mkuu wa
zamani ambaye jina lake halikuwamo miongoni mwa makada watano
waliopitishwa na Kamati Kuu ya CCM.
Habari ambazo Mwananchi imezipata kutoka kwa
wajumbe wa Halmashauri Kuu zinasema kuwa baada ya mapumziko ya chakula
cha mchana, ulizuka mjadala mkubwa kuhusu kuenguliwa kwa Lowassa, ambaye
alionekana kuwa alikuwa akiongoza mbio za urais ndani ya chama hicho.
Habari hizo zinasema wakati wa mjadala huo ndipo
wajumbe wa Baraza la Ushauri la Viongozi walipoingilia na kuanza kutoa
ushauri mmoja baada ya mwingine kabla ya Mkapa kuzungumza na baadaye
kusema “twendeni tukapige kura, asiyetaka atoke”, ndipo hali ya ukimwa
ilipotanda na kufuatiwa na kazi ya kupiga kura iliyoashiria kuwa amani
imerejea.
Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa kikao hicho chenye
wajumbe takriba 400 kutulizwa na kufikia hatua ya kupigia kura majina
matano ili kupata matatu ambayo yalipelekwa kwenye Mkutano Mkuu.
Habari ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa
wajumbe waliokuwa wakimtaka Lowassa walikuwa wakihoji sababu za mbunge
huyo wa Monduli kuenguliwa huku jina la Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe likiachwa.
Alikuwa mwenyekiti wa baraza hilo, Ali Hassan
Mwinyi aliyeanza kwa kuwaeleza wajumbe historia ya changamoto
zilizokipata chama hicho, aliyoyaona mwaka 1995 wakati kulipokuwa na
wagombea 17, lakini walioingia kwenye mchujo walikuwa 15, wakiwemo
Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na Cleopa Msuya.
Mwinyi aliwashauri wajumbe kuwa kama wanampenda
mtu, wawe na kiasi na kama wanamchukia mtu, wawe na kiasi pia na kwamba
wasifanye mambo hayo kwa kupitiliza kwani matokeo yatapokuwa tofauti na
walivyotarajia wao ndiyo wataathirika zaidi kuliko muhusika.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa mwingine aliyetoa
nasaha zake alikuwa Waziri Mkuu wa zamani, John Samuel Malecela, ambaye
aliimbia kwenye mbio hizo mwaka 2005 wakati walipojitokeza makada 11
kuwania kuteuliwa na CCM.
Malecela, ambaye wakati huo alikuwa na wadhifa wa
makamu mwenyekiti wa CCM Bara, Malecela aliwaeleza wajumbe hasa
walikuwa na mapenzi na Lowassa kwamba hata yeye wakati huo alikuwa na
kundi kubwa la watu waliokuwa wanamuunga mkono kutoka Kanda ya Ziwa.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa, Malecela aliwaambia
wajumbe wa NEC kwamba wafuasi wake walikuwa wakilia kwa uchungu kutokana
na jina lake kukatwa, walimshauri mengi ikiwemo ya kuhama chama,
lakini aliwaambia “chama kwanza mtu baadaye”, kwa maana huo ndiyo
ulikuwa uamuzi wa chama na unapaswa kuheshimiwa.
Wakati huo, baada ya Rais Kikwete kutangazwa kuwa
ndiye ambaye angepeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2005, alikwenda kumpa mkono wa hongera na kuahidi kumuunga mkono.
Post a Comment Blogger Facebook