Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, January Makamba amemtolea uvivu mshauri wa zamani
wa Siasa wa Rais Jakaya Kikwete, Kingunge Ngombale-Mwiru kwa kuupinga
mchakato wa uteuzi wa mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM na kusema
anakivuruga chama.
Kingunge aliyejitoa kindakindaki kumpigania mbunge
wa Monduli na waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa, amekuwa akitoa
matamko mbalimbali kuhusiana na mchakato huo na zaidi akisema haukutenda
haki hasa baada ya kuenguliwa jina la Lowassa.
Kamati ya Usalama na Maadili, Kamati Kuu na
Halmashauri Kuu ya Taifa, ndizo zilizokuwa na kazi ya kuchuja majina
hadi kupatikana mgombea mmoja, Dk John Magufuli.
Akizungumza jana kwa simu kutoka Bumbuli Tanga,
Makamba (pichani) alisema: “Mzee Kingunge ni mtu mzima, ninamuheshimu
sana, ni mkongwe katika siasa, lakini anakivuruga chama.”
Alisema binafsi hakubaliani na kauli za Kingunge
kupinga uteuzi wa Dk Magufuli kwa sababu makada wote wa chama
waliokuwapo Dodoma, waliamua kumpitisha kwa kuwa walimuona anafaa na
anaweza kukijenga chama.
“Ndani ya chama kuna wazee wenye busara ambao
waliangalia vitu vingi hadi kumteua mgombea kwani unaweza kuwa mtendaji
mzuri lakini ukawa na kasoro nyingi hivyo, unaweza vilevile kuonekana
ukashindwa kukivusha chama kwenye ushindi.
“Mimi ninamuheshimu sana Mzee Kingunge, lakini
siwezi kukubaliana naye anavyokandia mchakato. Mimi ninaamini ulikuwa
sahihi, kila mtu ameridhika na ndiyo maana kura zilipigwa…, tuna imani
naye na anaweza kuongoza tangu zamani,” alisema Makamba.
Makamba alisema, ana imani kwamba atafanya vizuri
hivyo ni bora apewe ushirikiano kama walivyopewa viongozi waliopita ili
kukinusuru Chama cha Mapinduzi na watu waendelee kukiheshimu kama
awali.
Katibu mkuu mstaafu wa chama hicho, Yusuph
Makamba alikaririwa na vyombo vya habari juzi akisema kwamba, watu
wanaoendelea kulalamikia mchakato wa kumpata mgombea urais kwa tiketi ya
CCM, Dk Magufuli wana masilahi binafsi na siyo kwa ajili ya
kukiimarisha chama hicho.
Kauli ya Kingunge
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake
mwanzoni mwa wiki, Katibu huyo wa zamani wa halmashauri kuu ya CCM
alisema, Kamati ya Usalama na Maadili iliteka majukumu ya Kamati Kuu
baada ya kuamua kuchuja majina ya makada waliojitokeza kuwania urais
hadi kufikia watano, akisema jitihada hizo zilifanywa kwa kuvunja kanuni
na zililenga kumuengua Lowassa kuwania kuingia Ikulu.
Kingunge alisema kitendo cha kumuengua Lowassa
kwa kuvunja kanuni kimeacha kasoro kubwa ndani ya chama hicho tawala kwa
sababu taratibu zilikiukwa ili kupata viongozi.
Post a Comment Blogger Facebook