Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi, (NEC) Jaji Damian Lubuva amesema mgombea urais mteule wa CCM,
Dk John Magufuli hapigi kampeni bali kinachofanyika ni utambulisho wa
mgombea wao kwa wananchi.
Kauli ya Lubuva imekuja ikiwa ni siku chache baada
ya Chama cha ACT-Wazalendo kuandikia barua NEC, ikilalamika kuwa Dk
Magufuli ameanza kampeni kabla ya wakati.
Alisema NEC imepokea barua ya malalamiko ya
ACT-Wazalendo inayolalamika kuwa Magufuli ameanza kampeni kabla ya muda
na pia kulalamika kualikwa kwa mteule huyo wa CCM kuwa mgeni rasmi
kwenye ufunguzi wa Michuano ya Kombe la Kagame, inayoanza leo kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Tume ina maadili yake, kwa mfano eti tumzuie
asiende kwenye mechi , sisi tumzuie kama nani, huu si wakati wetu,
wakati wetu ukifika tutakunjua makucha yetu” alisema.
Alisema NEC haihusiki hata na yale yanayotokea
Dodoma, bali itaanza kazi yake ifikapo Agosti 21 mara baada ya uteuzi
rasmi wa wagombea.
Akizungumzia zaidi ziara hizo, Jaji Lubuva alisema
tume hiyo haina kauli juu ya ziara ya Magufuli, bali akifanyacho ni
mchakato tu wa ratiba ya chama chake.
Jaji Lubuva alisema kwa upande wa Sheria na
Katiba, Nec itaanza kuchukua hatua kwa wale watakaokiuka kanuni kuanzia
Agosti 22, pindi kipyenga cha kampeni kitakapoanza hadi Oktoba 24
kitakapomalizika.
“Katika kipindi hicho, tume inakuwa na nguvu ya
kuwashughulikia wagombea, kwa sasa kinachotokea ni mambo ya vyama, sisi
kwenye tume hatuna msingi wa kushughulikia hayo,” alisema.
Wakati Jaji Lubuva akisema hayo, Chama Cha Kijamii
(CCK) wameamua kutumia wanasheria ili kuandaa mipango ya kumwekea
pingamizi Dk Magufuli, kuwa anakiuka Sheria ya Uchaguzi kwa kufanya
kampeni kabla ya wakati.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa CCK Renatus
Muhabi, alisema Tume ya Uchaguzi (NEC) huenda nayo ikashtakiwa kwa
kushindwa kuwajibika licha ya kuwa ndiyo msimamizi wa Sheria ya
Uchaguzi.
“Tumeshampa kazi mwanasheria, Aloys Rugazia kuandaa pingamizi baada ya kutoridhishwa na majibu ya Jaji Lubuva.
“ Majibu yake Jaji Lubuva ni wazi yanaonyesha kuwa
anaiogopa CCM, maana ndiyo iliyompa hiyo nafasi, hapo unaweza kuona kwa
nini tumekuwa tunalilia tume huru, yeye anapodai hahusiki na kufuatilia
mambo anayofanya mgombea huyo, eti hadi pale atakapochukua fomu ya NEC,
huu siyo utawala bora ni ukiukwaji mkubwa,” alisema.
Post a Comment Blogger Facebook