Banza Stone enzi za Uhai wake
Banza Stone (wa kwanza kulia) akiwa na Bendi ya Muziki Ya Twanga Pepeta
Mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi, Banza Stone amefariki dunia leo hii Ijumaa. Ramadhani Masanja amefikwa na umauti kutokana na kuandamwa muda mrefu na magonjwa.
Shabani Ally Masanja ambae ni kaka wa Banza amethibitisha kutokea kifo cha Banza Stone nyumbani Sinza na msiba uko Sinza njia panda ya Lion. Banza Stone alikuwa anaugua ugonjwa wa fungus ya kichwa na kifua.
Banza Stone aliyezaliwa mwaka 1972 na kufanikiwa kumaliza elimu ya msingi katika shule ya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam mwaka 1987, alianza taratibu kujihusisha na masuala ya muziki akiwa angali mdogo.
Banza alianza muziki miaka 25 iliyopita, mara tu baada ya kumaliza elimu yake ya msingi kwa kujihusisha na muziki wa Hip Hop, enzi hizo walikuwa wakisikiliza katika redio. Wakati huo alikuwa na wenzake kama kina K One na Scoz Man.
Wazazi wake waliweka pingamizi baada ya kuonekana muziki huo kuwa wa kihuni na mwaka 1990 akaamua kuanza mchakato mpya wa kuwa mcheza dansi, alicheza dansi kwenye maharusi na kufanikiwa kupata fedha kidogo. Banza aliamua kwenda shule kusomea masuala ya mziki kwenye chuo cha utamaduni cha Korea, Korea Cultural Music Centre mwaka 1990 mpaka 1991.
Baada ya kuhitimu cheti alianza kuimba katika bendi mbalimbali ikiwamo The Heart Strings, Twiga Band, Achigo Band kama mpiga ngoma, Afri-Swez na bendi nyingine ndogo ndogo. Alikuwa akidumu katika bendi kwa miezi kadhaa, kabla ya kuhamia katika bendi nyingine mpaka alipoingia katika bendi ya The African Stars, Twanga Pepeta na kuijenga bendi hiyo barabara.
Alijiunga na chuo cha Sanaa Bagamoyo mwaka 2000 ambapo alipata mafunzo kwa miaka miwili, alipomaliza alitoka Twanga Pepeta na kwenda Tanzania One Theatre (TOT) na huko alijulikana zaidi kwa jina la Mwalimu wa Walimu japo hakukaa sana na kuamua kuanzisha bendi yake iliyokuwa ikiitwa Bambino Sound ambayo ilidumu kwa miezi kadhaa tu lakini ilivunjika kutokana na kutokuwa na uongozi mzuri na akarudi African stars Band na baadae kuhamia Extra Bongo.
Katika kipindi cha miaka 24 tangu aanze muziki wa dansi rasmi haikuwa rahisi kwake kupata mafanikio, kwani alizunguka sana mpaka kuifikia bendi ya The African Stars Twanga Pepeta mwaka 1995. Banza Stone alipitia zaidi ya bendi tisa ikiwemo Rufita Band. Mwaka juzi msanii wa muziki wa kizazi kipya, Hamisi Ramadhani H-Baba aliamua kumshirikisha Banza kurekodi wimbo wake mpya wa Sina Raha.
Banza Stone amewahi kutamba na nyimbo kadhaa zikiwemo: Mtaji wa Maskini, Kumekucha, Elimu ya Mjinga, Angurumapo Simba Mcheza Nani na Falsafa ya Maisha. Amewahi pia kuimba vibao kadhaa vya taarabu ukiwamo Kuzaliwa Mjini na ule wa Play Boy.
Post a Comment Blogger Facebook