Dodoma/Dar. CCM imesema haitarudia makosa ya
mwaka 2010 ya kutengua uamuzi wa wanachama, lakini itahitaji kuwa na
moyo mgumu baada ya makada wengi kukata rufaa kupinga matokeo ya kura za
maoni.
CCM inamalizia hatua ya mwisho ya mchakato wake
wa ndani wa kupata wagombea ubunge na udiwani kwa vikao vya Kamati Kuu
na Halmashauri Kuu vitakavyopitia majina ya makada wote walioshinda
kwenye kura za maoni, ambazo zilitawaliwa na tuhuma za rushwa na
ukiukwaji wa taratibu.
Vikao hivyo huwa vinaweza
kutengua ushindi wa kada kwenye kura za maoni kwa kuangalia rufani
zinazopinga mchakato, tuhuma za rushwa na ukiukwaji wa taratibu.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nnauye alisema wamepokea malalamiko mengi kuhusu ukiukwaji wa kanuni za
uchaguzi katika upigaji wa kura za maoni.
“Kumekuwa na
utamaduni wa kulalamika barabarani wakati mwingine kushawishi wanachama
kulalamika kwenye vyombo vya habari na kwingineko. Utaratibu huu si wa
chama chetu,” alisema Nape.
“Tunashauri taratibu zifuatwe. Katika kufikia hatua hii tunawaomba wanachama wawe watulivu.”
Alisema
wanachama wamejaa mjini Dodoma wakijaribu kushawishi wajumbe kuhusu
rufaa zao, lakini akasema kinachotakiwa kiwasilishwe ni malalamiko yao,
ushahidi wa kutosha katika ngazi husika.”
Nape pia
alisema kumezuka wimbi la matapeli linalowalaghai makada walioshindwa
katika kura za maoni kuwa watoe fedha ili wawasaidie rufaa zao kwenye
vikao hivyo.
Alisema matapeli hao wamesajili namba za
simu za viongozi wa CCM na kwamba yeye ni mmoja wa viongozi
walioathirika na utapeli huo kwa namba yake ya simu ya mkononi kutumika.
“Wanawataka
kutoa fedha ili waweze kuwasaidia na tayari tumeshawanasa baadhi yao na
kuwakabidhi polisi. Wawe makini wasikubali kutapeliwa fedha zao na kama
wana malalamiko wafuate utaratibu uliowekwa,” alisema.
Pamoja
na Nape kutotaja idadi ya rufaa zilizowasilishwa, Mwananchi iliongea na
makada 16 ambao walithibitisha kuwa wanasubiri uamuzi wa vikao hivyo
baada ya kutuma barua zao kupinga matokeo.
Mwananchi
imeshuhudia makada waliobwagwa katika kura hizo, wakiwemo mawaziri
wakiwa kwenye viunga vya jengo la makao makuu ya CCM mjini hapa.
Baadhi
ya makada hao ni mbunge wa Busega, Dk Titus Kamani aliyeangushwa na Dk
Raphael Chegeni. Kamani aliiambia Mwananchi kuwa amekata rufani kupinga
matokeo ya kura za maoni kwa kuwa mchakato ulitawaliwa na rafu nyingi na
anaamini yeye ni mshindi.
Mwingine aliyekuwa mjini
hapa ni Juma Kilimba na David Jairo waliobwagwa Iramba Magharibi,
Asumpta Mshama aliyeangushwa kwenye Jimbo la Nkenge.
Wabunge waliokata rufani
Vigogo
wengine walioangushwa kwenye kura hizo ni Naibu Waziri wa Maji, Amos
Makala (Mvomero), ambaye alisema amelazimika kukata rufaa baada ya
kutoridhishwa na mchakato ulivyoendeshwa, ikiwa ni pamoja na baadhi ya
viongozi wa CCM kutumika kumwangusha.
Alisema kulikuwa
na hujuma wakati wa uchaguzi na baadhi ya viongozi wa chama walitumia
mwanya huo kumjengea mazingira ya ushindi mpinzani wake.
Mbunge
mwingine, Said Nkumba (Sikonge) alisema amekata rufani ili haki
itendeke kwa kamati husika, baada ya kubaini kuwepo kwa njama za
makusudi za kumwangusha hasa baada ya uongozi wa wilaya kuamuru upigaji
wa kura urudiwe katika maeneo ambayo alionekana ameshinda. Madai kama
hayo yalitolewa na Gregory Teu (Mpwawa) ambaye alikata rufaa akisema
haki haikutendeka na kulikuwa na mchezo mchafu. Mbunge wa Dodoma Mjini,
Dk David Mlole alisema ikiwa Kamati Kuu ya CCM itashindwa kuitendea haki
rufaa yake, ataachana na masuala ya siasa.
Naye mbunge
wa Morogoro Kusini –Mashariki, Dk Lucy Nkya alisema iwapo rufaa yake
haitashinda, atakubaliana na matokeo na hatahama chama kwa sababu ya
kushindwa katika kura za maoni.
Mshama alidai kuwa
amehujumiwa katika mambo mengi yaliyojitokeza kwenye mchakato huo,
ikiwamo baadhi ya washindani wake kupotosha kwenye vyombo vya habari
kuhusu siku ya kura ya maoni.
“Jambo hilo liliwafanya
baadhi ya wapigakura wangu kutojitokeza, hivyo kunifanya nikose kura
zao. Nimefanya mambo mengi katika jimbo hili ambalo watu wake wanapenda
elimu walinifurahia. Siamini kama wamenikataa, hizi ni hujuma,” alisema
Mshama.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dk Titus Kamani alisema anavyojua ni kwamba yeye ndiye mshindi.
“Hivi
wewe unaongea nini? Mimi najua nimeshinda sasa unasemaje nikuambie plan
B yangu wakati nimeshinda mimi. Siwezi kushindwa na wala sijasikia
kwamba nimeshindwa,’’ alisema Dk Kamani
Naye Nyambari Nyangwine, mbunge wa Tarime, alisema alisema mambo hayakuwa mazuri kwenye matokeo ya kura za maoni.
“Mimi siwezi kuhama chama kwani kutumikia wanaume wawili ni kazi kubwa. Unajua naamini Kamati Kuu itatenda haki tu,’’ alisema
Ally
Kibona Mbunge wa Ileje alisema anaiomba CCM iwe makini na rafu ambazo
zinachezwa ndani ya chama hicho hususan kipindi cha uchaguzi ikiwemo
kuanza kampeni kabla ya muda wake.
Mbunge wa Jimbo la
Mbinga Mashariki mkoani Ruvuma, Gaudance Kayombo alisema kwamba yeye
alishakata rufaa baada ya kutokubaliana na matokeo hayo ila hafikirii
kukihama chama tawala.
Wakubali matokeo
Wakati
makada hao wakisubiri kwa hamu uamuzi wa vikao vya juu vya chama,
baadhi ya vigogo walioshindwa wamesema wamekubaliana na matokeo na
hawana mpango wa kukata rufaa.
Wabunge hao ni pamoja na
Dastan Mkapa (Nanyumbu), Dk Muhammed Seif Khatibu (Uzini), Mathias
Chikawe (Nachingwea), Gaudensia Kabaka, Adam Malima (Mkuranga) na Salehe
Pamba (Pangani).
Vikao vya uteuzi
Nape
alisema jana kuwa vikao vya Taifa vya chama hicho vilianza jana na
sektarieti itakaaa kwa siku mbili, ikifuatiwa na Kamati Kuu ya Taifa na
Halmashauri Kuu itakayokutana Jumatano na Alhamisi.
“Kwa nafasi ya ubunge na uwakilishi tunategemea kufanya uteuzi Agosti 8 (Alhamisi),”alisema Nape.
Post a Comment Blogger Facebook