0
Mjumbe wa Iliyokuwa Tume ya Mabadiliko yakutoka gazeti la mwananchi

Dar es Salaam. Mjumbe wa Iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole amesema yupo tayari kufanya kampeni za kumpinga mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa kwa madai kuwa ana doa linalomzuia kuwania nafasi hiyo.
Polepole ameibuka kuwa maarufu tangu kumalizika kwa Bunge la Katiba, akishiriki kwenye midahalo kadhaa kuhusu mchakato wa kuandika Katiba mpya, akitofautiana na msimamo wa CCM wa kubadilisha Rasimu ya Katiba.
Akizungumza na Mwananchi jana, Polepole alisema Lowassa anayeungwa mkono na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ana tuhuma za ufisadi na ni mmoja wa makada wa CCM walioipinga Rasimu ya Katiba.
Polepole alisema msingi wa kuzaliwa kwa Ukawa ni kutaka Katiba mpya yenye maoni ya wananchi, hivyo Chadema kumpokea Lowassa ni sawa na kukiuka misingi hiyo.
“Nimeshirikiana na Ukawa na viongozi wao kama Watanzania kuhakikisha Taifa letu linapata Katiba mpya na inayotokana na maoni ya wananchi. CCM ambao walikuwa ndiyo wana mkakati na wenye maamuzi ya mwisho katika kukwamisha maoni ya wananchi. Watu hao (wa CCM) hawastahili kupewa uongozi iwe ndani ya CCM au hata ndani ya Ukawa,” alisema.
“Hawana dhamira njema na Taifa letu, watuhumiwa mengine nitaelewa, lakini kwenye la Katiba nilikuwepo na ninajua mchango wao wa kutukwamisha. Niliweka maoni yangu kwamba CCM ikiwachagua hao nitapiga kampeni ya kuwakataa. Hawakupita CCM na mmoja wapo ni Lowassa.”
Alisema amepoteza imani na Ukawa kwa kukubali kuikiuka misingi ambayo awali waliisimamia.
“Nina haki ya kutokubaliana na msimamo wa Ukawa na ikibidi nitasimama na kupiga kampeni ya kumkataa mgombea wao wa urais,” alisema.
Katika Bunge la Katiba, wajumbe kutoka CCM walilazimisha kuondolewa kwa baadhi ya mapendekezo kwenye Rasimu ya Katiba, ikiwa ni pamoja na pendekezo la kutaka muundo wa Muungano uwe wa serikali tatu.

Post a Comment Blogger

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();
 
Top