JESHI la polisi mkoa wa Dodoma limetoa
taarifa kwamba raia mwenye asili ya kiasia,Amit Kevalramani,aliyekamatwa
na fedha zaidi ya milioni 70 zilikuwa ni fedha zake mwenyewe.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa
Polisi mkoa wa Dodoma, David Misime amesema baada ya uchunguzi
uliofanywa na jeshi la polisi walibaini kuwa fedha hizo zilikuwa zake.
“Napenda kutoa taarifa fupi kuhusu tukio lililotokea tarehe 11/07/2015 majira ya saa10:00 asubuhi katika Hoteli ya St. Gasper hapa mjini Dodoma, kuwa wananchi walitoa taarifa majira ya saa 10:00 kwamba kuna mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia amekamatwa na wananchi akiwa na fedha nyingi na kuna vurugu kubwa.
“Baada ya kupata taarifa hizo Jeshi la Polisi Mkoani hapa lilifika eneo la tukio ili kuona kama taarifa hizo ni za kweli.
“Askali walithibitisha kuwa ni kweli
walimkuta mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia ambaye alijulikana kwa jina
la Amit Kevalramani mwenye umri wa miaka 31, Mhindi, Mfanyabiashara,
Mkazi wa Dar es Salaam akiwa na fedha kiasi cha Tsh. 722,500,000.
“Alipohojiwa alisema kuwa tarehe 10/07/2015 alifika Dodoma kwa ajili ya ununuzi wa mazao ya nafaka”alieleza kamanda Misime.
Misime amesema mtuhumiwa huyo alifika
Dodoma 10 Julai mawaka huu majira ya asubuhi na alifikia katika Hoteli
ya St. Gasper na 11 Julai 2015 aliamua kurudisha fedha benki kutokana na
kuona mkusanyiko wa watu wengi wasioeleweka na wenye viashiria vya
vurugu.
Amesema akiwa katika harakati ya
kurejesha fedha hizo benki, ndipo kundi la watu waliokuwa katika eneo la
Hoteli ya St. Gasper walimtilia mashaka na kumzuia asiondoke na ndipo
taarifa zilitolewa polisi.
Kwa mujibu wa maelezo ya Misime amesema
mashaka ya watu hao yalitokana na vuguvugu za kisiasa/mchakato wa
uchaguzi kati ya makundi mbalimbali kuwa kuna watu wanahonga wajumbe.
Amesema taarifa hizo ndizo hata polisi
walizopokea kabla ya kufanya uchunguzi lakini baada ya uchunguzi wa kina
jeshi hilo lilijiridhisha kuwa taarifa hizo hazikuwa za kweli.
“ Katika tukio hili na uchunguzi
tulioufanya tumebaini kuwa hakuna kosa la jinai lililothibitika licha ya
kukutwa na kiasi hicho cha fedha, tuhuma za rushwa ambazo ndiyo
zilikuwa msingi wa ukamataji wa mtu huyo hazikuthibitika, kwa kuwa
hakuna aliyeona akizigawa fedha hizo wala hakuna aliyedai kushawishiwa
au kugawiwa fedha hizo.
“Aidha imethibitika fedha hizo ni mali
yake halali na kwa kuwa hakuna ushahidi mwingine uliyo thibitisha
vinginevyo amerejeshewa fedha zake” alisema Misime
Wakati huo huo Misime amesema 10 Julai
2015 majira ya saa saa 3 usiku eneo la Railway Dodoma tulifanikiwa
kuwakamata raia wa Burundi kwa kosa la kuishi nchini bila kibali.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Hererimana
Methode(21), Hatungimana Alexis, (20),Niyongabo Justin,( 20),Nteturuye
Onesphore (21), Bikorimana Levis, (21) ambao wote ni Wakazi wa Mabanda
Burundi kwa kosa la kuingia nchini na kuishi nchini bila kibali.
Amesema watuhumiwa hao a walikuwa
wanasafiri na treni kuelekea Dar es Salaam na walipofika Dodoma Askari
wanaosindikiza treni waliwashtukia na walipowakamata na kuwahoji
walijieleza kuwa ni raia wa Burundi.
Kutokana na tukio hilo Misime amesema
anawaomba wananchi wa mkoa wa Dodoma na nje ya Dodoma kutoa ushirikiano
pale wanapoona watu ambao siyo raia.
Amesema wasikubali kuwakaribisha
wasiwakaribishe bali watoe taarifa kwa vyombo vya dola waweze kuhojiwa
kwani hata kama waliingia Nchini na kuhifadhiwa katika makambi yaliyopo
Nchini hawaruhusiwikutoka kwenda mbali na kambi zao bila kuwa na
kibali maalum.
Post a Comment Blogger Facebook