HATIMAYE Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), kimetoa Mwongozo uliokuwa unasubiriwa kwa muda mrefu kuhusu
namna ya kuendesha zoezi la kura ya maoni katika ngazi ya udiwani nchi
nzima. Anaripoti Deusdedit Kahangwa …. (endelea).
Kwa mujibu wa Mratibu wa Kanda Taifa, Mohamed Mtoi, Mwongozo huo unaotaja wajumbe wa vikao vya uteuzi katani pamoja na masharti ya kisheria kuhusiana na zoezi hili, unapaswa kuzingatia na watendaji wote wa Chadema Tanzania nzima.
Kwa mujibu wa Mwongozo huo, Kamati ya
Utendaji ya Kata nidyo yenye jukumu la “kufanya uteuzi wa awali wa
wagombea Udiwani.” Baadaye, uteuzi huo unapaswa kuthibitishwa na “Kamati
ya Utendaji ya Jimbo” husika.
Mwongozo huo unasisitiza kwamba, ni
muhimu masharti ya akidi ya vikao vya uchaguzi kwa mujibu wa Katiba ya
Chadema kuzingatiwa. Kulingana na “Ibara ya 6.2.2 (b) ya Katiba ya Chama
ya mwaka 2006 akidi ya Kikao cha Uchaguzi ni 75%,” inasema mwongozo.
Mbali na kutaja wajumbe wa vikao vya
uteuzi, mwongozo huo umefafanua masharti ya uteuzi kwa mujibun wa Sheria
ya Uchaguzi wa Serikali za mitaa (Udiwani) ya mwaka 1979 (The Local Authorities (Elections) Act 1979).
Kwa mujibu wa sheria hii, chini ya
Kifungu cha 39, mtu anayetaka kugombea Udiwani anapaswa kuwa na vigezo
vifuatavyo: awe raia wa Tanzania, awe ametimiza miaka 21, awe mwanachama
wa Chama cha Siasa, na awe mkazi wa Halmashauri ambapo uchaguzi wa Kata
unafanyika.
Mwongozo huo umewakumbusha watendaji wa Chama kuzingatia masharti ya kifungu cha 40 cha sheria hiyo.
Kulingana na kifungu hicho, mtu atapoteza
sifa za kugombea udiwani ikiwa mtu huyo ana uraia wa nchi nyingine; au
mtu huyo amethibitika kuwa ana matatizo ya akili kwa mujibu wa sheria;
au mtu huyo amehukumiwa hukumu ya kifo au hukumu nyingine jela zaidi ya
miezi sita; au amewekwa kizuizini kwa muda unaozidi miezi sita; au ni
mbia au meneja wa kampuni ambayo imeingia mkataba na Halmashauri husika
ambayo yeye anagombea; au ikiwa amezuiliwa kujiandikisha kuwa mpiga kura
kwa mujibu wa sheria.
Vile vile, mwongozo huo umewakumbusha watendaji hao kuzingatia masharti ya kifungu cha 42(1) cha sheria hii.
Kwa mujibu wa kifungu hiki, mgombea
lazima awe na wadhamini wasiopungua kumi; lazima awasilishe tamko
lililosainiwa na Hakimu kuona kuwa anazo sifa na vigezo vya kuteuliwa
kugombea; na lazima awasilishe tamko la msimamizi wa uchaguzi wadhamini
waliomdhamini ni wapiga kura halali wa Kata anayogombea.
Sababu za kuwasilisha pingamizi dhidi ya
mgombea wa Udiwani, kama zilivyotajwa katika kifungu cha 44 cha sheria
hiyo, zimegusiwa pia.
Kwa mujibu wa mwongozo huo, mgombea
anaweza kuwekewa pingamizi ikiwa taarifa za mgombea zilizopo kwenye fomu
ya kuomba uteuzi hazijitoshelezi kumtambulisha; au ikiwa fomu yake ya
uteuzi haiendani na taratibu za kisheria za uteuzi; au ikiwa kutokana na
yaliyomo kwenye fomu ya uteuzi mgombea anakosa vigezo vya kuteuliwa; au
ikiwa pingamizi dhidi ya mgombea liwasilishwe kabla ya saa kumi siku
inayofuata mara baada ya siku ya uteuzi.
Utaratibu wa Kufanya Vikao vya Kura ya Maoni Katani
Kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na chama, utaratibu wa kufanya vikao vya kura ya maoni ngazi ya madiwani ni kama ifuatavyo:
Kwanza, Katibu wa Kata atachambua fomu za
wagombea na taarifa zao kwa ajili ya kuwasilisha taarifa kwenye kikao
cha Kamati ya Utendaji ya Kata. Pili, Taarifa ya Katibu wa Kata kuhusu
wagombea itawasilishwa kwenye Kamati ya Utendaji ya Kata.
Tatu, Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya
Kata kama walivyoainishwa katika ibara ya 7.3.8 ya Katiba wataipokea
taarifa hiyo. Nne, kama Mwenyekiti wa Kata ni mgombea, basi kikao
kitaazimia kumteua Mwenyekiti mwingine wa muda ambaye si mgombea.
Tano, Katibu wa Kata atawasajili wajumbe wote wa kikao na watasaini karatasi ya mahudhurio.
Sita, Katibu wa Kata ataandaa karatasi za
kupigia kura ya maoni zikiwa na majina ya wagombea wote, kila jina la
mgombea likiwa na kisanduku cha kumwezesha mpiga kura kuweka tiki mbele
ya jina la mgombea.
Saba, Katibu Kata ataandaa fomu za
matokeo zikiwa na nafasi kwa ajili ya wagombea na mawakala wao kusaini
baada ya uchaguzi, ili baadaye aweze kuwasilisha fomu hizo kwa Katibu wa
Jimbo wa Jimbo/Wilaya.
Nane, Katibu wa Kata ataandaa muhtasari
wa kikao cha uteuzi wa mgombea udiwani na kuhakikisha unasainiwa na
Mwenyekiti na Katibu wa kikao. Tisa, Katibu wa Kata atawasilisha taarifa
ya uteuzi kwa Katibu wa Jimbo/Wilaya kwa ajili ya hatua zaidi.
Na kumi, Kamati ya Utendaji ya Jimbo/Wilaya itapokea, kujadili na kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea udiwani.
Nyaraka zinazohitajika wakati wa uteuzi wa wagombea udiwani
Kulingana na mwongozo uliotolewa na chama, mchakato wa uteuzi wa wagombea udiwani utaongozwa na nyaraka zifuatazo:
Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa1979; Kanuni za Uchaguzi za Mwaka 2010; Mwongozo wa Tume kwa vyama
vya siasa na wagombea wa Udiwani, Ubunge na Urais; Maadili ya Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2015; Katiba ya Chama ya Mwaka 2006 Toleo la mwaka 2014;
Mwongozo wa Chama Dhidi ya Rushwa; na Kanuni za Uchaguzi wa Kiserikali
na ndani ya Chama kama zilivyorekebishwa mwaka 2012.
Nyaraka nyingine ni Fomu za kuomba uteuzi
za wagombea wa Udiwani; Fomu za mahudhurio ya wajumbe kikao cha
uteuzi/mapendekezo; Karatasi za Kura na majina ya wagombea; Karatasi za
taarifa ya Matokeo; na Muhtasari wa kikao cha uchaguzi utakaoandaliwa na
Katibu wa Kata na Jimbo/Wilaya.
Utaratibu wa kura za maoni udiwani viti maalum.
Vigezo vya uteuzi wa Wagombea Udiwani
Viti Maalum navyo vimetajwa katika mwongozo huu. Kwa mujibu wa mwongozo
huu, vigezo vya jumla vya uteuzi wa madiwani viti maalum ni ka
aifuatavyo:
Kwanza, ni lazima mgombea awe mwanachama
wa CHADEMA; lazima awe mwanachama wa BAWACHA; na lazima awe amejaza
fomu zitakazoandaliwa na BAWACHA Makao Makuu kwa ajili ya kuwatambua
wagombea.
Kwa mujibu wa mwongozo huo, kutakuwa na kamati ya kupitia, kuchambua na kuchuja majina ya wagombea udiwani viti maalum.
Kamati hiyo ya mchujo itaundwa na ngazi
mbili. Katika ngazi ya kwanza kutakuwepo na Sekretariati ya BAWACHA
Wilaya/Jimbo. Na katika ngazi ya pili kutakuwepo na Kamati ya Utendaji
ya Wilaya/Jimbo. Kamati hii itapewa vigezo kutoka ngazi ya Taifa na kila
kigezo kitakuwa na alama zake kwa ajili ya kuiwezesha kamati kuwapata
wagombea walio bora.
Mwongozo huo unafafanua kwamba, idadi ya
Viti Maalum katika Halmashauri husika itategemea maelekezo
yatakayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa Halmashauri husika.
Lakini, “kama Tume watachelewa kutoa
idadi ya Viti Maalum katika Halmashauri husika, Mkutano Mkuu wa BAWACHA
ngazi ya Wilaya utachagua Madiwani wa Viti Maalum kulingana na Kata
zilizopo,” unasema mwongozo.
Mwongozo huo, unaonyesha mtiririko ufuatao katika mchakato wa kuwapata wagombea wa udiwani wa viti maalum:
Kwanza, Katibu wa BAWACHA wa Jimbo
atachambua fomu za wagombea waliojitokeza. Pili, taarifa ya uchambuzi wa
Katibu wa BAWACHA Jimbo itawasilishwa kwenye kamati ya uchuchaji ya
Jimbo/Wilaya.
Tatu, taarifa ya Kamati ya Uchujaji ya
Jimbo/Wilaya itawasilishwa kwenye Mkutano Mkuu wa BAWACHA Wilaya kwa
ajili ya kupiga kura.
Nne, Katibu wa BAWACHA wa Jimbo
atawasilisha taarifa ya matokeo ya Mkutano wa Mkuu wa BAWACHA wa
Jimbo/Wilaya uliofanya uchaguzi wa madiwani wa Viti Maalum kwenye Kikao
cha Kamati ya Utendaji ya Jimbo/Wilaya, kwa ajili ya uthibitisho.
Tano, Katibu wa Jimbo/Wilaya ataandika
barua ya kuwasilisha matokeo ya uteuzi wa Viti Maalum kwa Mratibu wa
Kanda kwa ajili ya kuyawasilisha kwenye ofisi ya Katibu Mkuu. Na sita,
Katibu Mkuu atawasilisha majina ya Viti Maalum kwenye Tume ya Taifa ya
Uchaguzi
Post a Comment Blogger Facebook