BAADA ya mchuano wa kuwania uteuzi wa kugombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM uliomalizika kwa Dk John Magufuli kuibuka mshindi, kwa wiki moja kuanzia leo joto la siasa linatarajiwa kuhamia kwa makada wa chama hicho wanaowania kuteuliwa kuwania ubunge na udiwani kote nchini.
Chama hicho tawala, kinatarajiwa kuanza kutoa fomu za ubunge, udiwani na wagombea wa Ujumbe katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Kutokana na kufunguliwa kwa pazia hilo, wananchi wenye sifa za uongozi wamehamasishwa kujitokeza.
Kwa mujibu wa ratiba ya mchakato wa uteuzi ndani ya CCM, fomu hizo zitakazogharimu Sh 100,000 kwa wagombea wa ubunge na Sh 10,000 kwa upande wa madiwani, zitatolewa hadi Julai 19, mwaka huu.
Kwa upande wa Dodoma Mjini, akizungumza na gazeti hili jana Katibu wa CCM wilaya hiyo, Albert Mgumba alisema mkoa wa Dodoma umejipanga vizuri katika kuhakikisha zoezi hilo linakwenda vizuri.
Alisema fomu zitakazotolewa kuanzia leo ni zile za Udiwani na Udiwani Viti Maalumu huku zile za Ubunge zikiwa na za Ubunge wa Jimbo na Ubunge Viti Maalumu. Alitoa wito kwa wana CCM kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu ili kutimiza haki yao ya kuchaguliwa.
“Tunahimiza wanawake kwa vijana kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu,” alisema.
Alisema CCM mkoa wa Dodoma imefanya uhamasishaji wa kutosha kuanzia vikao vya ndani na hata vikao vya nje kwenye mikutano ya hadhara ambapo wananchi wamehamasishwa kujitokeza kuchukua fomu.
Mgumba alisema baada ya kumalizika kwa zoezi la uchukuaji fomu, Julai 20, mwaka huu kampeni matawini zitaanza na kumalizika Julai 31, mwaka huu. Alisema kura za maoni kwenye matawi zitafanyika Agosti Mosi mwaka huu.
Post a Comment Blogger Facebook