0

SASA ni dhahiri kuwa mawaziri 11 wa Serikali ya Awamu ya Nne inayomaliza muda wake, wametoswa katika mbio za kuwania ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kati yao wakiwemo watatu ambao kura katika majimbo yao zilirudiwa baada ya kulalamikiwa.
Awali katika kura za maoni za kupata wagombea ubunge wa CCM zilizofanyika nchi nzima Agosti mosi mwaka huu, mawaziri tisa waliangushwa katika kinyang’anyiro hicho, akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe (Nachingwea) na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaundentia Kabaka (Tarime Mjini).
Mbali na hao, pia walikuwepo naibu mawaziri saba, akiwemo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim, Pereira Ame Silima (Mambo ya Ndani), Amos Makala (Maji), Kaika Saning’o ole Telele (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi), Dk Makongoro Mahanga (Kazi na Ajira), Adam Malima (Fedha) na Pindi Chana (Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto).
Baada ya kura hizo za maoni, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM iliyokaa wiki hii, ilibaini kuwepo kwa kasoro katika kura za maoni zilizofanyika katika majimbo 11 ambako zililalamikiwa, yakiwemo matatu ya Busega mkoani Shinyanga, Rufiji mkoani Pwani na Mahenge mkoani Iringa ambayo yalikuwa yakiwaniwa na mawaziri watatu.
Rufiji Katika Jimbo la Rufiji wilayani Rufiji mkoani Pwani, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid, alijikuta akipata kura 5,010 na kuangushwa na Mohamed Mchengelwa, aliyejizolea kura 6,002.
Katika kura za maoni za awali, uchaguzi huo uliingia katika utata baada ya kila upande kudai umeshinda, ambapo ilibidi uongozi wa CCM Mkoa uingilie kati, lakini ufumbuzi haukupatikana hadi suala hilo lilipopelekwa CCM Taifa na kuamuru uchaguzi huo ufanyike tena ili kupata mshindi halali. Katika uchaguzi huo wa marudio, jumla ya wagombea nane walijitokeza.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, ambao ulisimamiwa na kamati maalumu kutoka CCM mkoa ili kuhakikisha uchaguzi huo unakwenda vizuri, Msimamizi wa uchaguzi huo, Kombo Kamote ambaye pia ni Katibu wa CCM Wilaya ya Bagamoyo, alimtangaza mshindi huyo na kuamsha shamrashamra kutoka kwa wapenzi wa Mchengelwa.
Hata hivyo, wakati matokeo hayo yakitangazwa Dk Seif hakuwepo ukumbini. Makete Marudio ya kura katika Jimbo la Makete yaliyofanyika juzi, yalishuhudia Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Binilith Mahenge, akiangushwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Profesa Norman Sigalla.
Akitangaza matokeo hayo jana, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Mahenge, Jumanne Kapinga alisema Profesa Sigalla alijizolea kura 8,883 na kufuatiwa na Dk Mahenge aliyepata kura 7,885, Bonike Mhami (124), Fabian Nkinga (74) na Lufunyo Nkinda (42).
Awali katika kura za maoni za mwanzo za Agosti Mosi mwaka huu, Dk Mahenge aliongoza kupata kura 8,534 huku Profesa Sigalla akipata 8,211, Mhami (500), Nkingwa (486) na Nkinda (226).
Kwa kile kilichothibitisha kuwepo kwa udanganyifu wa matokeo ya awali, baadhi ya wana CCM wa jimbo hilo walilazimika kusafiri hadi makao makuu ya CCM ya wilaya ya Mahenge, kupinga matokeo hayo.
Jery Slaa kidedea Ukonga Mbali na mawaziri, katika Jimbo la Ukonga jijini Dar es Salaam, ambako pia kura zilirudiwa, Meya wa Ilala, Jerry Silaa ameshinda baada ya kupata kura 10,955, huku mfanyabiashara maarufu, Ramesh Patel akishika nafasi ya pili kwa kupata kura 6,960.
Silaa pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM. Akitangaza matokeo hayo jana, Katibu Msaidizi wa CCM Wilaya ya Ilala, Anastazia Mwonga alisema kwa matokeo hayo, Slaa amepata ushindi wa asilimia 57.1 ya kura zote, huku Patel akiambulia asilimia 36.3.
Katika matokeo ya awali, Silaa alishinda kwa kupata kura 10,000 huku Patel akishika nafasi ya pili kwa kura 7,356. Namtumbo Vita ‘chali’ tena Katika Jimbo la Namtumbo, kada wa chama hicho Edwin Ngonyani, amembwaga tena mbunge aliyemaliza muda wake, Vita Kawawa baada ya kupata kura 13,573 dhidi ya kura 10,068 alizopata Kawawa huku Balozi mstaafu wa Tanzania, Salome Sijaona akishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 6,015.
Akitangaza matokeo hayo, Mkurugenzi wa muda wa uchaguzi huo, Oscar Msigwa ambaye ni Mjumbe wa NEC ya CCM Wilaya ya Njombe, alimtangaza Ngonyani kuwa ndiye atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi kwa kushindana na vyama vingine vya upinzani.
 Na Habari Leo

Post a Comment Blogger

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();
 
Top