Ukawa wamedai wafuasi wake 38 wapo rumande za polisi kwa muda mrefu, huku Chadema ikisema Jumanne ijayo itawasilisha ombi Mahakama Kuu kutaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini aitwe kueleza sababu za kushindwa kuwafikisha watuhumiwa mahakamani.
Jana,
Chadema wametoa taarifa kwenye vyombo vya habari wakisema Jeshi la
Polisi linawashikilia wanachama wake 10 kwa zaidi ya wiki mbili sasa,
wakati CUF ilidai wanachma wake 28 wako kwenye mahabusu za polisi kwa
muda mrefu.
Mwanasheria
mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliwaambia waandishi wa habari kuwa
Jumanne watawasilisha ombi Mahakama Kuu kutaka Mkuu wa Jeshi la Polisi
nchini, Inspekta Jenerali Ernest Mangu aitwe mahakamani kueleza sababu
za kutowafikisha mahakamani watuhumiwa hao.
Lakini,
Mkurugenzi wa Upelelelzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athumani
amepinga madai ya watu kukamatwa kwa sababu za kisiasa pia alivitaka
vyama hivyo kwenda vituo vya polisi kuangalia makosa yaliyotendwa kama
yanahusiana na uanachama wa vyama vyao.
Lissu
amesema watu hao walikamatwa kwa nyakati tofauti katika mikoa
mbalimbali ukiwamo wa Songwe na walisafirishwa hadi Dar es Salaam na
kuwekwa mahabusu katika vituo vya polisi Kanda Maalamu ya Dar es Salaam.
“Ikifika
Jumanne ijayo kama watu hawa 10 hawatapelekwa mahakamani wala polisi
kuwaachia kwa dhamana, tunakwenda kufungua maombi ya kuwaita IGP au DCI
kwa sababu Mahakama Kuu ina mamlaka ya kuamuru mamlaka yoyote ya
Serikali inayoshikilia mtu, kumwita mkuu wa mamlaka kueleza kwanini
inamshikilia mtuhumiwa kwa muda uliozidi kisheria.
“IGP
na wasaidizi wake akiwamo DCI, wataieleza Mahakama Kuu kwanini
wanashikilia watu hao kwa muda mrefu. Kati ya watuhumiwa hao, wawili
wapo kituo cha Kanda Maalumu (Central Police) na nane wapo Oysterbay,” alisema Lissu.
Wanaodaiwa
kushikiliwa Kanda Maalumu waliotajwa na Idara ya Habari ya Chadema ni
Ben Nzogu na Mussa Sikabwe wakati wanaodaiwa kuwa Oysterbay ni Aristotle
Mgasi, Hosia Mbuba na Ignasia Mzenga,
Wengine ni Mdude Nyangali, Shakira Abdallah Makame, Dk David Nicas, Juma Salum na Suleiman Said.
Lissu,
ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki alisema wapo katika hatua za
mwisho za kuandaa hati ya kupeleka Mahakama Kuu endapo watu hao
hawatapewa dhamana na polisi au kupelekwa mahakamani.
Kwa
mujibu wa Lissu, watu hao wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kutoa
na kusambaza katika mitandao ya kijamii maneno yasiyomfaa Rais John
Magufuli, huku wengine wakituhumiwa kwa kosa la studio yao kutengeneza
wimbo wenye uchochezi.
“Hawa
ni watu wadogo sana, ndiyo maana wanafanyiwa hivi. Ingetokea kwangu
mimi au Mbowe (Freeman), mngeona kesho yake tumepelekwa mahakamani.
Jamani mahabusu siyo kuzuri, niulizeni mimi,” amesema Lissu.
Mwanasheria huyo ameongeza, “sheria
inasema mtu anatakiwa ashikiliwe na polisi kwa saa 24 na baada ya hapo
anapelekwa mahakamani isipokuwa akikamatwa siku zisizo za mahakama,
lakini kwao hawa wenzetu ni kinyume na wanazidi kuteseka,” alisema Lissu.
Lissu
alidai alikutana na watuhumiwa hao wakiwa katika mahabusu na alielezwa
mateso wanayoyapata baada ya kupelekwa sehemu fulani ambayo walikwenda
kushughulikiwa na kikosi kazi kinachojumuisha vyombo vya ulinzi.
“Huwa
wanachukuliwa kutoka mahabusu usiku na kupelekwa mikocheni kwenye kituo
cha mateso. Wanavuliwa nguo na wanapigwa hadi kuvuja damu. Wanawekwa
katika vituo vya polisi zaidi ya wiki mbili bila kupelekwa mahakamani
kwa sababu tu ya tuhuma.
“Katiba
ya nchi, Ibara ya 13, ibara ndogo ya sita inapiga marufuku mtu kuteswa,
kudhalilishwa na kuwapa adhabu ya kinyama. Lakini, Tanzania ya leo kuna
sehemu imeandaliwa kwa ajili ya kuwatesa watu,” alisema Lissu.
Mbali
na watu hao 10, Lissu alisema amepata taarifa zisizo rasmi kuwa watu
wengine 73 ambao hawajafahamika kutoka mikoani, nao wanashikiliwa kwa
makosa mbalimbali ikiwamo kutoa maoni ambayo hayampendezi kiongozi wa
nchi.
“Wakifika
hapa Dar, mwenyewe mamlaka ya kuwashughulikia ni Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), siyo mkuu wa upelelezi wala kamanda
wa mkoa husika.
“Sitaacha kusema ukweli, nitaendelea kusema kutokana na mambo mabaya yanayofanyika katika nchi hii,” alisema Lissu.
Katika
hatua nyingine, Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano
na Umma wa CUF, Mbarara Maharagande amesema tatizo kama hilo pia
linawakabili wanachama wa chama hicho, lakini hawatarudi nyuma
kuwapigania.
Amesema
Tanzania Bara wapo wanachama 10 kutoka mikoa ya Tanga na Mtwara ambao
wanashikiliwa na polisi kwa muda mrefu kwa tuhuma za kisiasa, huku Pemba
na Unguja wakiwa 18 wanaotuhumiwa kukata mikarafuu.
“Viongozi
wetu wa ngazi husika bado wanapambana na suala hili. Tutahakikisha
wanapelekwa mahakamani ili sheria ifuate mkondo wake,” alisema Maharagande.
Akizungumzia
madai hayo, DCI Athuman Diwani amesema polisi katika utendaji kazi
inaangalia kosa alilolifanya mhalifu na kwamba hawaangalii kilichofanywa
na mwanachama wa chama fulani.
Alipoulizwa
sababu za kuchelewa kuwapeleka watuhumiwa hao mahakamani, DCI alimtaka
Lissu awasiliane na wapelelezi kujua sababu za kuchelewa kwa kuwa kuna
sababu nyingi za mtuhumiwa kupelekwa mahakamani.
“Mojawapo ya sababu ni mahojiano yanayoyafanyika kati ya mtuhumiwa na polisi kuhusiana na makosa aliyoyatenda,” alisema.
Mkurugenzi huyo aliongeza, “Lakini nimesikia kuwa wanakwenda mahakamani, waache waende kwa sababu ni haki ya kila Mtanzania,” alisema Athuman.
Hata
hivyo, alisema jana kuna watuhumiwa wengi walipelekwa mahakamani, hivyo
huenda watu anaowasema Lissu wakawa ni miongoni mwao.
Pia,
aliwataka viongozi wa CUF kwenda polisi na kueleza kuwa watu
waliokamatwa ni watu wao, ili jeshi hilo liangalie uhusiano wa makosa na
uanachama wao.
Post a Comment Blogger Facebook