TAMKO
LA MHESHIMIWA UMMY MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO KUHUSU WATOTO WALIOMALIZA ELIMU YA MSINGI
LILILOTOLEWA TAREHE 09/09/2016
Ndugu
Wanahabari, Nitumie fursa hii kupitia kwenu kuongea na watoto wa
Tanzania, wazazi / walezi na jamii kwa ujumla katika kipindi hiki muhimu
ambacho watoto wetu wamemaliza Elimu ya Msingi. Kwa niaba yangu na kwa
niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania napenda kuchukua
nafasi hii kuwapongeza watoto wote waliomaliza mtihani wa Taifa wa
kuhitimu Elimu ya Msingi mwaka huu, Hongereni sana!. Ni jambo la ufahari
kwetu sisi wote kama wazazi/ walezi na Taifa kwa ujumla kwani hii ni
fursa adhimu kwa ustawi na maendeleo ya mtoto na ni moja ya njia ya
kutimizwa kwa haki ya msingi ya mtoto ya kuendelezwa ambayo inamjengea
mtoto msingi imara wa maisha yake ya baadae. Pongezi zangu nyingi kwa
watoto wote wa kike na wa kiume walioweza kufikia hatua hii muhimu kwa
maendeleo na ustawi wao.
Ndugu
Wanahabari, Takwimu zinaonyesha kuwa, wanafunzi 795,761 (wavulana
372,883 sawa na asilimia 46.86 na wasichana 422,878 sawa na asilimia
53.14) wamesajiliwa kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu. Hivyo
ningependa kutumia fursa hii kuwaasa watoto waliomaliza darasa la saba
kutojihusisha na tabia au vitendo vyovyote vinavyo hatarisha afya,
usalama na maendeleo yao, kama vile kujihusisha kwenye masuala ya ngono,
matumizi ya madawa ya kulevya na vileo katika kipindi hiki cha kusubiri
matokeo ya mitihani yao.
Watoto
wetu wa Kike na Kiume wajitambue, na wajue kuwa wao ni hazina ya pekee
katika maendeleo ya nchi yetu. Kipindi hiki wakitumie vizuri kwa kuwa
waadilifu, waaminifu, wenye bidii na kuzingatia kanuni za nidhamu na
tabia njema huku wakijiandaa kwa ajili ya kuendelea na elimu ya
Sekondari. Tukumbuke kuwa Serikali imekusudia kumpa kila mtoto nafasi ya
kupata elimu ya Sekondari. Msingi tayari umeshawekwa na Rais wa Awamu
ya tano, Mheshimiwa John Pombe Magufuli wa kutoa Elimu ya Sekondari
bure. Hivyo tusingefurahi mmojawapo kati ya watoto hawa waliomaliza
elimu ya msingi jana akaikosa nafasi hii kwa sababu zinazoweza
kuzuilika. Nawaasa watoto wote kutumia kipindi hiki kwa kukataa
kurubuniwa, kushawishiwa na kujiingiza katika mambo yenye kuhatarisha
afya, usalama na maendeleo yao.
Ninawataka Wazazi wenzangu, Walezi na jamii kwa ujumla:-
Kutowaozesha
watoto wote wa kike waliohitimu darasa la saba mwaka huu wakati wa
kipindi hiki cha kusubiria matokeo yao, iwe ni kwa sababu yoyote ile au
kwa lengo la kujipatia mali kwa njia ya mahari. Kila Mzazi/Mlezi
anapaswa kutambua umuhimu wa mtoto wake kuendelea kielimu, na kukua
kimwili na kiakili kabla ya kuingia katika ndoa. Ieleweke kuwa Elimu ya
watoto wa kike ni moja ya njia bora za kupunguza umaskini katika mataifa
yanayostawi. Kila mwaka wa elimu kwa mwanamke utaongeza mapato yake ya
baadae kwa asilimia 15, ikilinganishwa na asilimia 11 kwa wanaume.
Aidha, Kila mwaka wa mtoto wa kike kuwa shule humuepusha na maambukizi
ya Virusi vya Ukimwi (VVU) mara 7.
Pia,
uzoefu unaonyesha kuwa, kila mwaka wa kuelimika humsaidia msichana
kufanya maamuzi bora yake na ya familia yake. Benki ya Dunia ilibainisha
ya kwamba kila mwaka wa elimu huzuia vifo 2 vya uzazi katika wanawake
1000 kila mwaka!. Kwa hiyo kumpa mtoto wa kike fursa ya elimu inamsaidia
sio yeye tu kukua kiakili na kimwili lakini pia inamnusuru na ndoa na
mimba za utotoni na kuchangia maendeleo yake, ya familia yake na jamii
kwa ujumla. Ni vyema jamii hasa wazazi na walezi wafahamu kuwa ndoa kwa
wasichana sio njia muafaka ya kutatua changamoto za kifedha za
wazazi/walezi. Bali elimu ndio njia bora ya kutatua changamoto hizo.
Kuwalinda
watoto wote wa kike na wa kiume waliohitimu darasa la saba mwaka huu
dhidi ya vitendo vyote vya Ukatili, hasa kwa watoto wa kike kupewa mimba
au kuwahusisha katika mahusiano ya kimapenzi. Kwa mujibu wa Sheria ya
makosa ya kujamiiana ya mwaka 1998 ambayo imefanyiwa marekebisho na
kuhuishwa kwenye Makosa ya Jinai (Penal Code Cap 16) inaelekeza kuwa ni
kosa la jinai kwa mtu yoyote kumlaghai mtoto wa chini ya miaka 18 kwa
kumpa mimba au kufanya nae mapenzi.
Kifungu
cha 130 (e) cha Sheria hii kinaeleza wazi kuwa “Ni kosa kwa mtu wa
jinsia ya kiume kumbaka msichana au mwanamke; kwa ridhaa au bila ya
ridhaa akiwa chini ya umri wa miaka kumi na nane. Mtu yeyote
atakayetenda kosa la kubaka atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha maisha
au kifungo kisichopungua miaka thelathini. Aidha, Sheria ya Mtoto Namba
21 ya mwaka 2009 Kifungu cha 83 kinaelekeza kuwa ni kosa kumuhusisha
mtoto katika kazi, biashara au mahusiano yoyote yenye mlengo wa kingono
iwe ni kwa malipo au bila malipo.
Mkono
wa Serikali ni mrefu. Tutahakikisha tunawakamata na kuwafikisha
Mahakamani wale wote watakao kwenda kinyume na sheria hizi.
Aidha,
natoa Rai kwa wananchi wote kuendelea kutoa taarifa kwa mamlaka husika
za Serikali za Mtaa, Kijiji, Kata, Wilaya na hata katika Madawati ya
Jinsia na Watoto yaliyopo Polisi, pale watakapobaini mzazi au mlezi au
taasisi anaenda kinyume na jitihada za serikali za kumuendeleza mtoto
kielimu hasa katika kudhibiti ndoa za watoto waliomaliza Elimu ya Msingi
hususan katika kipindi hiki cha kusubiri matokeo yao.
Vunja ukimya toa taarifa kwa maendeleo ya watoto wetu.
Nawatakia kila la kheri watoto wote wa Tanzania katika kipindi hiki cha kusubiri matokeo yao ya mtihani wa Elimu ya msingi.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu wabariki watoto wa Tanzania.
Imetolewa na:-
UMMY A. MWALIMU (MB)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WAZEE NA WATOTO
DODOMA
09/09/2016
Post a Comment Blogger Facebook