0

Polisi nchini imepiga marufuku vikundi vya ulinzi vya vyama vya kisiasa , vyenye mwelekeo wa kijeshi kufanya kazi za ulinzi hadharani kwa madai kuwa vinaingilia majukumu yao.

Onyo hilo lilitolewa jana na Kamishna wa Polisi–Operesheni na Mfunzo, Paul Chagonja wakati akizungumza na waaandishi wa habari Makao Makuu ya Polisi, Dar es Salaam.

Chagonja alivitaja vikundi hivyo na vyama vyao kwenye mabano kuwa ni Green Guard (CCM), Red Brigade (Chadema) na Blue Guard (CUF), ambavyo hutumiwa na vyama vya siasa hususan katika mikutano yao.

Agizo la Chagonja limekuja ikiwa ni miezi minne baada ya agizo la Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu kupiga marufuku vikundi hivyo vya vyama vya siasa ambavyo vina muonekano na muundo wa vyombo vya usalama, kwani ni kinyume cha katiba na sheria ya nchi.

Alivitaka vyama hivyo kuhakikisha vinafuata muongozo uliotolewa na Ofisi ya Msajili wa vyama hivyo na kama vikienda kinyume jeshi litapambana navyo.

IGP Mangu aliyasema hayo mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Polisi uliokuwa ukijadili namna ya kuondoa vikundi hivyo pamoja na namna ya kuboresha shughuli za uendeshwaji wa vikundi hivyo.

Alisema vikundi hivyo vipo kinyume cha sheria na kwamba kuendelea kuvimiliki kwa kisingizio chochote ni uvunjifu wa Katiba ya nchi na sheria ya vyama siasa, jambo ambalo polisi haliwezi kulivumilia.

“Polisi imejipanga vizuri kuhakikisha mikutano ya kampeni ya vyama vya siasa inafanyika katika hali ya utulivu hadi siku ya uchaguzi,“ alisema Kamishna Chagonja.

Alisema katika kipindi cha kuelekea katika kampeni zinazoanza leo ni muhimu kila mmoja kujiepusha na makosa yanayoweza kupelekea jinai.

Huku akitoa mfano wa makosa hayo ni kubandua picha ya mgombea wa chama fulani kinyume cha sheria.

Kamishna Changonja aliwakumbusha wagombea kwa nafasi zao kuwaelimisha wafauasi wao umuhimu wa kuheshimu sheria ili kudumisha amani, usalama na utulivu katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi.

“Tunatoa tahadhari kwa wananchi pia kuzingatia sheria zinazowaongozwa ikiwamo sheria ya vyama vya uchaguzi na miongozo mbalimbali iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),” alisema Chagonja.

Akizungumza hatua hiyo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuwa askari polisi hawatoshi kulinda mkutano wa watu wengi hivyo wataendelea kuwatumia kulinda wanachama wao.

Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema katika chama chao hakuna kikundi kinachoitwa Green Guard kwani hata Katiba ya chama hicho hakina watu kama hao.

Mkurugenzi wa uchaguzi wa Chama cha CUF, Shaweji Mketo alisisitiza chama chake kuendelea kuwatumia, kwa sababu wapo kikatiba na katiba yao ilipitishwa na Serikali na inatambuliwa na msajili wa vyama vya siasa.

Kwa mujibu wa Mketo, kauli ya Chagonja ni kutaka wavunje katiba ya chama, kwani maamuzi ya kuwatumia yalipitishwa na mkutano mkuu, “Tutawatumia hiyo ya kutukataza haipo, wapo na katiba ya chama iliweka hilo na msajili wa vyama vya siasa akalipitisha hilo, ina maana hakuona tatizo, ”alisema.

Alifafanua kuwa Red Guard hawajawahi kusababisha matatizo zaidi ya kulinda amani, hivyo hawana sababu ya msingi ya kuacha kuwatumia. Mketo alilalama kuwa kila unapofika uchaguzi kunakuwa na kauli za kukatisha tamaa na kutishwa, wao hawaogopi kwa sababu wamefuata sheria.
kutoka
Mpekuzi blog

Post a Comment Blogger

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();
 
Top