Mtu mwenye pumu huwa na mcharuko uvimbe sugu
mwilini kwenye mirija yake ya kupitishia hewa (bronchioles tubes) hali
ambayo husababisha kuvimba kwa kuta za mirija hii na kuwa na ute mzito
hivyo kupungua kwa njia ya kupitishia hewa.
Hali ambayo
humfanya muathirika kushindwa kuvuta na kutoa hewa nje na hivyo kupumua
kwa shida sana. Tatizo hili linaweza kudumu kwa muda mfupi au mrefu
kiasi cha kuhitaji tiba ili kumuwezesha mgonjwa kupata nafuu.
Kutokana
na kuwepo kwa msuguano na uzuiaji wa kupitisha hewa wakati wa kupumua
hewa nje, pumu hujulikana pia kama obstructive lung disease .
Mtu
aliye na pumu huwa na kipindi ambacho hawi na tatizo la pumu mpaka pale
mwili unapochokozwa na kuingia katika hali hiyo. Wakati huo hote cha
maisha yake kinachotokea ni kutulia tu mpaka pale inapotekea uchokozi
mwilini.
Pumu inaweza kugawanywa katika makundi mawili,
iko pumu ya ghafla ijulikanayo kitabibu kama Acute asthma. Wagonjwa
wanaopatwa na kundi hili la pumu huwa na hali ya kawaida katika njia zao
za hewa isiyobadilika wakati wa shambulio na usio wa shambulio.
Kundi
nyingine ni Pumu sugu (Chronic Asthma). Kundi hili la pumu huwa na
tabia ya kuwa na njia nyembamba za kupitisha hewa na kadiri jinsi
mgonjwa anavyoendelea kupata matukio zaidi ya pumu njiaza hewa huzidi
kuwa nyembamba na kusinyaa zaidi.
Aina za pumu
Bila
kujalisha mgonjwa anaingia katika kundi gani, ugonjwa wa pumu unaweza
kugawanywa katika aina kuu nne, ambazo ni inayobadilika, isiyobadilika,
ya mazoezi na inayosababishwa na kazi.
Pumu
inayobadilika (brittle asthma): Kulingana na tabia ya kujirudia rudia
kwa matukio ya ugonjwa huu na madhara yake kwa mgonjwa, aina hii ya pumu
inaweza kugawanywa zaidi katika aina nyingine mbili.
Aina
ya kwanza ya pumu inayobadilika (type 1 brittle asthma) ni pumu yenye
tabia ya kuwa na matukio na mashambulizi ya kubadilika kila mara
japokuwa mgonjwa anaweza kuwa anapata matibabu kadhaa.
Aina
ya pili ya pumu inayobadilika (type 2 brittle asthma) ni pumu ambayo
mgonjwa anatokea kupata shambulizi la ghafla (asthmatic attack) wakati
hapo awali ugonjwa wake uliweza kuthibitiwa kwa matibabu.
Pumu
hatari isiyobadilika (status asthmaticus): Hii ni aina ya pumu iliyo
hatari zaidi kwa mgonjwa. Pamoja na matumizi ya dawa kadhaa, zikiwemo
vitanua njia za hewa (bronchodilators) na vipoza mcharuko mwili
(steroids), mgonjwa wa aina hii ya pumu anaweza asipate nafuu ya haraka
na anaweza kupoteza maisha.
Pumu inayosababishwa na
mazoezi: Hali hii husababishwa na ufanyaji wa kupitiliza wa mazoezi ya
viungo. Kwa kawaida wakati wa kufanya mazoezi mtu hupumua kwa kutumia
pua na kupitia mdomo.
Hata hivyo, wakati mwingine
hutokea hewa aivutayo huingia ndani ikiwa haijapozwa vya kutosha puani
na hivyo kusababisha ongezeko la mtiririko wa damu katika mishipa
inayosambaza damu katika mirija ya kupitisha hewa.
Hali
hii husababisha kuvimba kwa kuta za mirija hiyo na muhusika kupata
shambulizi la pumu. Aina hii ya pumu yaweza kudhibitiwa na dawa.
Inashauriwa
sana kwa watu wenye matatizo kama haya kupasha moto misuli kwa mazoezi
mepesi kabla ya kuanza mazoezi mazito na ya muda mrefu.
Pumu
inayosababishwa na aina ya kazi: Mazingira ya kazi yanaweza kusababisha
kutokea kwa pumu hata kwa baadhi ya wafanyakazi wasio na tatizo hili.
Aina
hii huweza kuwatokea watu wanaofanya kazi kwenye viwanda vya
kutengeneza matairi, vigae, rangi, kemikali mbalimbali, mbolea, chuma,
unga, mbao na nguo.
Pumu husababishwa na nini?
Kuna
mambo kadhaa yanayoweza kusababisha kutokea kwa pumu au yanayohusishwa
na shambulizi lake. Mambo hayo ni pamoja na matatizo ya vinasaba,
maendeleo ya kiuchumi, magonjwa ya mapafu, moshi wa tumbaku, dawa za
kushusha shinikizo la damu, uchafuzi wa mazingira, msongo wa mawazo na
kichanga kuanza kutumia antibiotiki mapema.
Matatizo ya kinasaba yamehusishwa na kutokea kwa karibu asilimia 90 ya ugonjwa wa pumu hususani kipindi cha utoto.
Uvutaji wa sigara au tumbaku kipindi cha ujauzito pia unahusishwa na kusababisha pumu kwa mtoto atakayezaliwa.
Ugonjwa
wa pumu umeonekana sana kwenye nchi zilizoendelea kiuchumi
ikilinganishwa na nchi zenye maendeleo na hali duni ya kiuchumi. Sababu
bado hazijawa wazi.
Magonjwa ya mapafu kama bronchitis,
vyanzo vya mzio kama vile vumbi, vinyesi vya wanyama na baadhi ya
vyakula, vinaweza kuchoche tatizo hilo.
Uchafuzi wa
mazingira kama moshi na baadhi ya harufu kali, Baadhi ya kemikali kwenye
maeneo ya kazi hasa kwenye viwanda kama vya rangi, chuma, sementi na
vigae.
Baadhi ya wagonjwa wanaotumia dawa za kushusha
shinikizo la damu zilizo katika jamii ya beta-blockers kama vile
propanolol wapo katika hatari ya kupata shambulio la ugonjwa wa pumu.
Magonjwa
kwenye mfumo wa kupumua yasabishwayo na baadhi ya virusi na bakteria
kama vile rhinovirus, Chlamydia pneumonia au Bordetella pertusis.
Matumizi
ya mapema sana ya baadhi ya dawa hasa antibiotiki kwa watoto yanaweza
kubadilisha mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya magonjwa na hivyo kumfanya
mtoto kuwa katika hatari ya kupata pumu.
Ongezeko la msongo wa mawazo huweza kusababisha pumu na matatizo katika mfumo wa upumuaji.
Upasuaji
wakati wa kujifungua (caesarian section), Tafiti kadhaa zimeonyesha
kuwa kujifungua kwa njia ya upasuaji huongeza uwezekano wa kupata pumu
kwa vile njia hiyo yaweza kuathiri mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya
maradhi.
Vihatarishi vya ugonjwa wa pumu
Uwezekano
wa kupata ugonjwa wa pumu huongezeka iwapo mtu atakuwa na magonjwa ya
mzio kama vile magonjwa ya ngozi (eczema) au homa isababishwayo na aina
fulani ya vumbi, vumbi la maua au chavua, matumizi ya asprini na
maambukizi ya ugonjwa wa virusi.
Vile vile kama anaishi
sehemu zenye baridi au hewa yenye unyevu na vumbi, matatizo katika njia
yake ya chakula ikiwamo uchokozi wa kujaa tindikali na gesi tumboni.
Dalili za ugonjwa wa pumu
Dalili
za ugonjwa wa pumu ni pamoja na kuishiwa na pumzi, kupumua kwa shida
huku pumzi zikikata, kutoa sauti kama mtu anayepiga miluzi wakati wa
kupumua (wheezing), kukohoa sana hasa nyakati za usiku au asubuhi.
Kikohozi huambatana na kutoa makohozi mazito, yasiyo na rangi au yenye
rangi ya njano.
Kubana kwa kifua kwa mtu aliyepata
shambulizi kubwa la pumu na atashindwa kuzungumza na pia kuwa na hali
kama ya kuchanganyikiwa huku.
Matibabu ya Pumu
Kwa
ujumla matibabu ya pumu hujumuisha kuepuka visababishi/ vianzisha mzio
vya ugonjwa huu na matumizi ya madawa kwa walio na hali mbaya.
Kwa
wagojwa wanaopata ugonjwa huu kwa sababu ya msongo wa mawazo hupewa
ushauri nasaha kwa ajili ya kusaidia kutatua matatizo yanayowakabili.
Vilevile
inashauriwa kwa wenye tatizo hili kuwa na dawa karibu muda wote kwa
ajili ya matumizi pindi shambulizi litakapotokea. Vilevile inashauriwa
kuepuka mazingira na hali za baridi ambazo huweza kuchochea kutokea kwa
shambulio la ugonjwa huu.
Matibabu ya kutumia dawa
hujumuisha matumizi ya dawa za kusaidia kupunguza na kuondoa makohozi
(expectorants) na dawa zinazosaidia kutanua mirija ya hewa
(bronchodilators).
Zipo dawa pia pia za kuondoa
mcharuko mwili na zile za kuzuia mzio Hata hivyo, kuna matibabu ya ziada
kulingana na hali ya mgonjwa pamoja na kundi na aina ya pumu
inayomuathiri.
Kwa wagonjwa wenye pumu ya ghafla na
wenye hali mbaya matibabu hujumuisha matumizi ya dawa za kutanua mirija
ya hewa, (bronchodilators) pamoja na kuongezewa hewa ya oksijeni.
Vilevile
dawa za kutuliza mcharuko mwili (steroids) pamoja na dawa za kutuliza
kukakamaa kwa misuli ya mwili (intravenous muscle relaxants). Kwa
wagonjwa wenye pumu sugu, jambo la muhimu ni kuepuka visababishi na
matumizi ya dawa zinazosaidia kutanua mirija ya hewa.
Ni
vema pia kuepuka matumizi ya dawa za jamii ya beta-blockers kwa
wagonjwa wenye shinikizo la damu na ambao pia wana pumu. Dawa hizi
huleta uchokozi na mgonjwa hupata kikohozi na kubanwa.
Post a Comment Blogger Facebook