Dar es Salaam. Mahakama ni
chombo kilichoanzishwa, kwa mujibu wa Katiba na chenye mamlaka kisheria
ya kutoa haki katika jamii kuhusu mashauri mbalimbali ya kijinai, mauaji
au madai ili mkosaji aadhibiwe na asiye na hatia aachiwe.
Katiba
imeruhusu kuanzishwa kwa mahakama katika ngazi mbalimbali kuanzia
mwanzo, wilaya, mkoa, mahakama kuu na rufani. Hata hivyo, uchunguzi
uliofanywa na Mwananchi umebaini kwamba katika baadhi ya mahakama za
mwanzo za jijini Dar es Salaam kuna mitandao ya rushwa inayoshirikisha
wanasheria feki, polisi na mahakimu kukosesha haki.
Mitandao
hiyo inaathiri utoaji hukumu, inachangia kuchelewesha kesi kwa
makusudi, ulaghai katika kuwatoa watuhumiwa waliopo mahabusu, rushwa ili
dhamana itolewe na kulazimishwa kumaliza kesi kabla ya hukumu. Baadhi
ya watu wanaoonekana kuwa wagumu kutoa fedha za kinachoitwa “kusukuma
mwenendo wa kesi” hupewa usumbufu kama vile kulazimishwa kufika asubuhi
mahakamani wakati kesi zao zinasomwa au kusikilizwa jioni au
kuahirishwa.
Mtandao wa dhuluma
Muhidini
Ngulumwa aliyeshitakiwa katika Mahakama ya Mwanzo ya Magomeni, alisema
kuwa ni mwaka wa tatu tangu aliposhitakiwa, lakini kesi yake inatajwa na
hajawahi kupanda kizimbani. Japokuwa kuna wakati huwa anamwona kortini
mlalamikaji wakati wa kusikilizwa kesi huambiwa mlalamikaji huyo ana
udhuru hivyo kesi huarishwa kwa mtindo huo.
Ngulumwa
alisema anashangaa kwa nini mshtaki anakosekana mahakamani zaidi ya mara
tano lakini kesi hiyo haifutwi huku akiendelea kutumia fedha kwa nauli.
“Kuna
Mzee wa Baraza aliwahi kuniambia nikitoa fedha hiyo kesi itamalizika
mapema na hukumu itakuwa upande wangu. Nilipomuuliza kiasi gani
aliniambia Sh500,000, ili agawane na wenzake na Sh200,000 apewe hakimu.
Nilipomjibu sina sijamuona hadi leo na bado napoteza muda huku hatima
yangu nikiwa siielewi, ”alisema Ngulumwa.
Kuruthumu
Majjid alimfikisha Kituo cha Polisi Magomeni aliyekuwa akifanya naye
biashara kwa madai alimdhulumu fedha. Anasema kuwa ilimlazimu kutoa
chochote ili akamatwe na polisi na afikishwe kortini.
Alisema
awali alipoambiwa ili mtuhumiwa akakamatwe lazima atoe fedha, alikataa.
Baadaye alisalimu amri akatoa kiasi cha Sh80,000 lakini akaambiwa
afikishe Sh100,000 na alipotekeleza, ndipo mdaiwa alipokamatwa na
kufikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Magomeni. Hata hivyo, mshitakiwa
yuko nje kwa dhamana.
“Kuanzia hapo amekuwa akiwatambia
watu kuwa ataniyumbisha sana katika kesi hii, na kweli hafiki
mahakamani, huu ni mwezi wa 13 tangu nimshtaki, nasota kutwa nzima, kesi
imesogezwa mbele zaidi ya mara nne, nahisi wanataka nichoke kesi ifutwe
kinyemela, ”alisema.
Katika Mahakama ya
Mbagala-Kizuiani, Abdallah Mjata analalamika kwamba amefungua kesi ya
wizi wa kuaminiana muda mrefu lakini anazungushwa kila siku uchunguzi
haujakamilika. Tofauti na siku nyingine sasa anatakiwa kumaliza kesi
hiyo nje ya mahakama.
“Hapa unaponiona najipanga kuweka
wakili. Kesi niliyofungua inamhusu jamaa niliyempa fedha,
tukaandikishiana, kila kitu ninacho. Kinachofanyika hapa sikielewi kwani
sijawahi kukutana na hakimu wala kesi kutajwa, nikija nakutana na hawa
wanaojifanya wazee wa baraza na kuniomba nimalizane na mtuhumiwa, mimi
sitaki ndiyo maana nasubiri kusonga mbele, ” alisema Mjata.
Mjata
anadai kuwa kinachotembea kortini ni fedha kwamba hiyo ni tabia ya
wanaojifanya watu wa kati ambao wanaharibu sura nzima ya kesi ndiyo
maana anataka kuikomesha kwa kusonga mbele. “Siishii hapa kwa sababu
nina faili, nilifungua kesi hapa,” anasisitiza.
Mzee
mmoja wa baraza mahakamani hapo alikiri kuwapo watu wanaojifanya
washauri wa mahakama wakati si wafanyakazi na hao ndiyo huchafua jina
lao kwa kuwa watu wa kati wanakula fedha ya huku na huku. Alishauri watu
wanaokuwa na kesi wasipende vitu rahisi kwa kuamini misaada
midogomidogo na ahadi hewa ambazo hazitekelezi.
“Watu
wajue kuna matapeli wengi wanaoishi mahakamani, hao wakigundua hilo
wanajiweka kati, hivyo nashauri wahusika kuwa makini, hakuna kitu rahisi
wala cha mkato zaidi ya kufuata sheria, vinginevyo wakikubali
kulaghaiwa kirahisi watapata shida,” alisema mzee huyo ambaye hakutaja
jina lake litajwa gazetini.
Mwanamke mmoja aitwaye
Halima Abdan anasema ameliwa zaidi ya Sh1.2milioni huku akiwa
hajafanikiwa kumtoa ndugu yake aliyepo mahabusu Segerea.
Halima
aliangukia kwenye mikono ya askari ambaye hajawahi kukutana naye bali
huzungumza naye kwenye simu baada ya kuunganishwa na mzee wa baraza
akidai kuwa atamsaidia kumtoa ndugu yake aliyeko mahabusu kwa mwaka wa
pili sasa.
Mara ya kwanza alitaka apewe Sh800,000 kwa
madai kuwa siku atakapopelekwa kortini kwa ajili ya kusikilizwa kesi
yake angeachiwa lakini ikashindikana. Mara ya pili alitaka apewe
Sh300,000 ili agawane na askari wa Segerea na Sh100,000 kwa ajili ya
kuwapa baadhi ya watu hapa mahakamani ili atoke lakini ilishindikana
pia.
Halima anasema, ndugu yake hakufanya kosa ili
alikumbwa na kesi hiyo kwa kuwa mtu aliyemdhamini amekimbia, hivyo
akakamatwa na ameshakaa ndani karibu mwaka na nusu.
“Nikimtazama
alivyokonda anapokuja mahakamani na tunapokwenda kumwona Segerea,
natamani nifanye kitu chochote kumtoa. Niliwahi kukutana na hakimu mmoja
akaniambia atanisaidia lakini naye amekula fedha na kila tukimpigia
simu haipatikani tena na wala hatumuoni tena,” alisema.
Mtu
mwingine aliyedakwa na mtandao wa kitapeli mahakamani ni Laizer Kaanan
ambaye anasema ndugu yake amewekwa mahabusu Keko zaidi ya mwaka mmoja u
na wanapotaka kumtoa “wanavunwa” fedha tu na wajanja wakiwamo mahakimu
wa Mahakama ya Mwanzo ya Kariakoo.
“Nimekuja nimwone,
akishushwa tu naondoka najua kesi yake haitatajwa, kila siku ni
hivyohivyo. Nimetoa karibu Sh600, 000, kila siku natajiwa fedha na mtu
hatoki, nimechoka naona kuna watu wananifanya mrija wa kufyonza, akitoka
sawa asipotoka basi, taratibu zote za dhamana nimekamilisha wamekaa
nazo wao, badala ya kuzifanyia kazi wananifanya mtaji wa kuchumia, sitoi
tena,” Kanaan alisema kwa masikitiko mahakamani hapo.
Katika
Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, kuna watu wa makamo huwa na makabrasha
yenye nyaraka, ambao inadaiwa wanatumiwa na mahakimu na polisi
kushawishi wenye mashauri watoe fedha kwa madai ya kufanikishiwa mambo
yao.
“Wapo wengi; mahakimu na polisi wanashirikiana na
matapeli hao; wengine wanafanikiwa kuwatoa jamaa zao mahabusu, kufuta
kesi na kuwakandamiza wenye haki. Mtandao huo upo sana hapa,”anasema
mzee mmoja maarufu eneo hilo ambaye jina lake limehifadhiwa.
Claudiana
Mbazigwa anasema kuwa ameliwa na wajanja kiasi cha Sh1.4 milioni kwa
ajili ya kutaka ndugu yake aliyeko mahabusu ya Segerea atoke.
“Sasa
karibu tunafilisika maana alipokuwa mahabusu Msimbazi wanaojifanya watu
wa msaada walitaka tutoe Sh300,000, nikatoa. Lakini mpaka sasa ikiwa
imepita zaidi ya miezi mitatu. Kila akiletwa hapa mahakamani tunaitwa
kwa ajili ya kumwona angalau kwa mbali pamoja na kuonana na hao wanaodai
kutusaidia kumtoa ambao tulifahamiana nao tangu akiwa Msimbazi. Hadi
huku wanatutisha ili tutoe fedha, siku zinakwenda hakuna
kinachofanyika,” anasema Mbazigwa.
Kisa cha kusikitisha
zaidi kimempata Abdallah Mpondela aliyetoka Lindi kuja kushughulikia
kesi ya ndugu yake na ikiwezekana kumtoa mahabusu. Baada ya kukamilisha
taratibu zote za dhamana na kutoa Sh500,000 bado hajafanikiwa kumtoa.
“Kila
nikija nakutana na wazee ambao hunieleza hali ya kesi na kunitaka nitoe
fedha zaidi, labda tutafanikiwa kumtoa, nimeshatumia 980,000, hajatoka
na leo alikuja hapa mahakamani..... kesi yake haijatajwa, sijui kwa
nini. Hao wazee wamesema niwasubiri na sasa wamesema niwakute kwenye
mgahawa wa Falcon ndiyo naenda kuutafuta,” alisema Mpondela.
Msajili wa Mahakama Kuu
Mahakimu
wafawidhi wa mahakama hizo hawakupatikana na waliokuwa wanakaimu
walidai hawana mamlaka ya kusemea jambo hilo zito. Lakini Msajili wa
Mahakama Kuu Tanzania, John Kahyoza anasema anayetakiwa kupinga rushwa
ni mtoa rushwa, hivyo watumie njia mbalimbali za kupinga ikiwamo
kuwasiliana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ili
kupata fedha kwa ajili ya kuwakamata wahusika.
Alisema
kwa upande wao kama wasimamizi wa mahakama wana upelelezi maalumu wenye
lengo la kuwafuatilia mahakimu wanaojihusisha na rushwa na wamewahi
kuwakamata mara kadhaa na kuwachukulia hatua.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah amesema kuwa wanajitahidi kupambana na rushwa lakini wanapata tatizo la ushahidi.
Post a Comment Blogger Facebook