Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa
la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amekana kumtolea lugha chafu
Askofu wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wakati
akisomewa maelezo ya awali katika Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam
jana.
Akisomewa maelezo na Wakili wa Serikali, Joseph
Maugo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilfred Dyansobera, Gwajima alikana
kutoa lugha chafu ila alikubali kuwa yeye ni askofu wa Kanisa la Ufufuo
na Uzima, majina yake na kwamba aliitwa polisi Machi 27, 2015 kwa ajili
ya kuhojiwa .
Maugo alidai upande wa mashtaka utawaita mashahidi saba kutoa ushahidi dhidi ya Gwajima pamoja na kuwasilisha vielelezo vitano.
Wakili wa Gwajima, Peter Kibatala aliomba kupewa maelezo ya mlalamikaji katika kesi hiyo.
Hakimu
Dyansobera aliuagiza upande wa mashtaka kuwapatia maelezo ya
mlalamikaji na kwamba kesi itaanza kusikilizwa kwa mashahidi upande wa
mashtaka kutoa maelezo yao Agosti 10, mwaka huu.
Ilidaiwa
kuwa kati ya Machi 16 na 25, mwaka huu kwenye Viwanja vya Tanganyika
Packers, Kawe, Gwajima alitoa lugha chafu dhidi ya Pengo.
Akisoma maelezo ya awali, Maugo alidai kati ya Machi 16 na 25, Gwajima alitoa maneno machafu kwa Pengo.
Hata hivyo, Gwajima aliyakana maelezo hayo na kukubali maelezo yake binafsi ya kuitwa polisi.
Katika
kesi inayomkabili Askofu Gwajima na wenzake watatu, Maugo alisema nayo
ilikuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali, lakini
mshtakiwa mmoja hakuwapo mahakamani kutokana na kusumbuliwa na maradhi.
Alidai
kwa mujibu wa sheria, mshtakiwa anatakiwa kuwapo mahakamani, hivyo
aliomba ipangwe tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali,
ambapo itasikilizwa Oktoba 8, mwaka huu.
Katika kesi hiyo, Gwajima anakabiliwa na shtaka la kushindwa kuhifadhi silaha na risasi anazomiliki kihalali.
Kwa
upande wa washtakiwa wenzake, akiwamo mlinzi wake, George Mzava,
Yekonia Bihagaze na Mchungaji Georgey Milulu, wao wanakabiliwa na
mashtaka mawili ya kukutwa wakimiliki bastola aina ya Berretta pamoja na
risasi 20 kinyume cha sheria.
Wanadaiwa kuwa Machi 29,
mwaka huu katika Hospitali ya TMJ, Mikocheni A walikutwa wakimiliki
bastola hiyo yenye namba CAT 5802 bila ya kuwa na kibali kutoka mamlaka
husika.
Pia wanadaiwa kuwa siku hiyo, washtakiwa hao
pia walikutwa wakimiliki isivyo halali risasi tatu za bastola pamoja na
risasi 17 za bunduki aina ya Shotgun. Washtakiwa wako nje kwa dhamana.
Post a Comment Blogger Facebook