BAADA ya vuta nikuvute katika
vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kuhusu
kukubaliwa au kutokubaliwa kwa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Ngoyai
Lowassa kujiunga na umoja huo ili kuongeza nguvu ya kisiasa, hatimaye
mwanasiasa huyo maarufu nchini amekubaliwa na tayari amejiunga rasmi
Ukawa akiwa mwanachama halisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), imefahamika.
Taarifa rasmi kutoka Ukawa na kwa
msemaji wa Lowassa ambaye hakutaka jina lake litajwe, imeeleza kuwa
uamuzi huo ulifikiwa baada ya majadiliano ya kina katika Mkutano Mkuu wa
Ukawa uliofanyika mapema wiki hii huku ajenda kubwa ikiwa ni kumpokea
Lowassa ili kuimarisha kambi ya upinzani ikiwa ni pamoja na kumsimamisha
kama mgombea urais wa umoja huo.
Taarifa rasmi zilizolifikia gazeti hili
zimeeleza kuwa Lowassa anatarajiwa kutangazwa rasmi Jumapili hii hivyo
maadalizi ya mkutano mkubwa wa aina yake yanaendelea. Chanzo chetu
kutoka katika mkutano huo kilisema kwa moyo mmoja, wenyeviti wa vyama
vyote vinavyounda umoja huo, yaani Freeman Mbowe (Chadema), Profesa
Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia
(NCCRMageuzi) na Emmanuel Makaidi (NLD), wameridhia kuungana na Lowassa
katika safari yao ya kuking’oa CCM madarakani huku wakiamini kuwa
wakimsimamisha kuwa mgombea wa Ukawa watafanikisha azma ya vyama vya
upinzani kuingia ikulu.
“Katika kikao chetu tulijadili mikakati
kadhaa ya kuchukua dola lakini kubwa zaidi lilikuwa ni jinsi ya kuungana
na Lowassa ili kutimiza azma hiyo, ikizingatiwa kwamba hivi sasa
anaungwa mkono na Watanzania wengi na hasa jinsi ambavyo hawakuridhishwa
na mchakato wa kumuengua kuwania urais kwa tiketi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), hivyo tuna uhakika kwa mkakati huu lazima tuking’oe CCM
madarakani,” alisema mjumbe mmoja wa Mkutano Mkuu (jina limehifadhiwa).
TUNDU LISSU AFUNGUKA
Akizungumzia suala hilo, Mnadhimu Mkuu wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu,
aliliambia gazeti hili kuwa majadiliano kuhusu Lowassa yalikuwa ya
lazima kwa kuwa katika muungano wa vyama kila kiongozi ana mtazamo wake
hivyo, kila jambo la muhimu lazima lifanyike kwa majadiliano ili kufikia
mwafaka kwani lengo ni kuhakikisha kwamba kunakuwapo na mkakati wa
pamoja kuhakikisha kuwa CCM kinag’olewa madarakani ili makada wa chama
hicho waelewe kuwa sasa Watanzania wanahitaji mabadiliko na si maneno
matupu ya majukwaani.
LIPUMBA NAYE ANENA
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa
Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba alisema kwamba Ukawa hivi sasa
wamejipanga kimkakati kuhakikisha wanachukua dola na kuongeza kwamba
waliokuwa wakieneza propaganda kuwa anawakwamisha wataendelea kuumbuka
kwa kuwa vyama vyote vinavyounda Ukawa ni kitu kimoja.
Aliongeza kwamba, kamwe umoja huo
hauwezi kusambaratika kwani ajenda kuu ni kuindoa CCM madarakani na
kuongeza kwamba, mambo mengine kama mgawanyo wa ruzuku yatafuata baadaye
kwani yanazungumzika katika ngazi ya uongozi.
MSIMAMO WA LOWASSA
Msemaji wa Lowassa ambaye kawa sasa
ndiye gumzo la taifa ukiachana na Dk. John Magufuli aliyepitishwa na CCM
kuwania kiti cha urais amelihakikishia gazeti hili kuwa Lowassa ameamua
kuingia Ukawa ili kuendeleza siasa za kistaarabu kutimiza azma yake ya
Safari ya Matumaini kama ambavyo amekuwa akiwaahidi Watanzania.
Alisema ameamua kuungana na Ukawa kwa
kuwa anaamini kuwa lengo la vyama vyote vya siasa ni kuhakikisha
vinatimiza malengo yao ya kuwahudumia wananchi, hivyo inapotokea katika
chama kimojawapo, bado kuna nafasi ya kutumia vyama vingine kutimiza
malengo ya kisiasa. Msemaji huyo aliongeza kwamba baada ya kuenguliwa
alikuwa na kazi ngumu ya kubaini nini cha kufanya ili kutimiza azma yake
ya kisiasa, ndiyo maana alikaa kimya ili kuepusha mivutano kati yake na
CCM lakini hakuwa amekata tama kuhusu jinsi anavyoweza kuwakomboa
Watanzania kutoka katika dimbwi la umaskini, jambo ambalo alikuwa
akiwaeleza katika safari yake ya kusaka wadhamini nchi nzima.
MKAKATI WA KAMPENI
Msemaji huyo alisema kuwa akiwa katika
Ukawa, Lowassa ameandaa mkakati kabambe wa uhamasishaji wananchi ili
watambue kwamba azma ya kuwakomboa ipo palepale na kuongeza kuwa ana
uhakika watamuunga mkono kwani anatambua kwamba wapo pamoja naye katika
safari ya matumaini.
Alisema kwamba kazi iliyo mbele yake ni
kuhakikisha kuwa anaisuka upya ‘Team Lowassa’ na atakuwa makini na
baadhi ya watu waliomsaliti ili wasiharibu mkakati wake na kuongeza
kwamba watazunguka nchi nzima kufanya kampeni za kistaarabu,
zisizokashfu wanasiasa wengine ili wananchi wapime ni kiongozi gani
anafaa kati ya yeye na wengine.
TATHMINI YA USHINDI
Chanzo chetu ndani ya Ukawa kilieleza
kwamba, tathmini iliyofanywa hadi sasa inawapa uhakika wa kuchukua dola
kwani katika maeneo mengi, Lowassa anaungwa mkono zaidi kuliko mgombea
mwingine yeyote yule. Kilisema kuwa katikamaeneo mengi CCM haikubaliki
kutokana na kuendesha siasa za kibabe na mizengwe, jambo ambalo limekuwa
likiwakera wananchi kwani kinachotokea ni kwamba wanachaguliwa viongozi
badala ya wao kuchagua viongozi wanaowataka.
Kilisema Lowassa ana nguvu zaidi katika
Mikoa ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa, Kusini, Nyanda za Juu Kusini na
Zanzibar hivyo CCM kama inataka kushindana naye ijipange vyema.
ZITTO AJUMUISHWA
Katika mkakati huo wa ushindi, inaelezwa
kwamba, umoja huo utamjumuisha kundini Kiongozi Mkuu wa Chama cha
ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye chama chake nacho kitaongeza nguvu ya
ushindi.
Lowassa alikuwa mgombea urais kwa tiketi
ya CCM kati ya wagombea 38 ambao walichukua fomu lakini jina lake
lilikatwa katika kikao cha Kamati ya Maadili na Usalama ya CCM, jambo
ambalo lilizua sintofahamu miongoni mwa wanasiasa wengi waliokuwa
wakimuunga mkono, hatua ambayo ilisababisha mtikisiko wa kisiasa nchini.
Post a Comment Blogger Facebook