0

Mtunzi: Enea Faidy
Ilipoishia sehemu ya pili ( kama hukuisoma bofya hapa)
...Baada ya kukamilisha yote hayo Madam Mbeshi akasogeza kiti chake karibu na meza kisha akaketi halafu akaanza kusogeza vitu vilivyokuwepo mezani pale lakini ghafla akakutana na karatasi chafuchafu mezani kwake lakini ilikuwa na maandishi.

Akashtuka kidogo halafu akaichukua ili aisome vizuri. Mwalimu Mbeshi hakutaka kuamini kile alichokiona, akataharuki kwa hofu na mshangao....

 Sehemu ya tatu
...Mwalimu Mbeshi aliposoma ujumbe ule kutoka kwenye ile karatasi chafuchafu alizidi kuchanganyikiwa sana, mapigo ya moyo yalimwenda kasi kama gari iliyokata breki ikiwa mlimani. akarudia tena na tena ujumbe ule uliosomeka "POLE SANA MWALIMU KWA MASWAHIBU YALIYOKUKUTA SHULENI KWAKO.. MIMI DOREEN MBWANA NIMEFANYA YOTE HAYO! PIA MUDA WA KIFO CHAKO U KARIBU KWANI UMESOMA UJUMBE WA MWANAFUNZI MCHAWI"

Jasho jembamba lilimtiririka mwanamama yule bila kuelewa afanye nini. Akataka kulitupa chini karatasi lile lakini ghafla akaona karatasi lile limebadilika ghafla, sio karatasi tena bali kitu kama ngozi ya binadamu iliyooza sana huku ikitoa harufu mbaya ikiwa imeambatana na funza wengi wakitembea tembea. 
Madam Mbeshi alihisi kinyaa sana huku woga ukiwa umemtawala kupita kiasi kwani katika maisha yake hakuwahi kushuhudia mauzauza ya namna ile hats Mara moja. Alitamani akimbie lakini miguu ilikuwa imeganda kama msumari kwenye sumaku. 
Mbeshi alihangaika sana na wale funza mkononi mwake kwani walizidi kumpanda mwilini kwa kasi na kumtia ghasia. Machozi yalimtoka mwalimu mbeshi lakini kila tone lililodondoka lilikuwa damu. 
Hofu ikamzidia sana, hakuwa na tumaini la kusalimika tena kwani kwa hatua aliyofikia ilitisha sana. Na yote hayo yalisababishwa na binti Doreen Mbwana.

Ghafla mlango wa ofisi ya mwalimu Mbeshi uligongwa lakini Mbeshi hakuwa hata na uwezo wa kuzungumza chochote. Mlango uligongwa sana lakini Mbeshi hakuweza kuufungua ingawa alitamani yule aliyegonga mlango aingie ili iwe ahueni kwake lakini ilishindikana. 
Kila aliponyanyua kinywa ulimi ulikuwa mzito na hakuweza kuzungumza chochote ikambidi atulie kimya akiugulia mateso yake yalimzonga ndani ya muda mfupi tu.

"Masikini Mimi  inamaana ndo nakufa? masikini familia yangu ambayo Mimi ndio tegemezi! ee Mungu nisaidie!" aliwaza Mbeshi huku machozi ya damu yakizidi kutiririka.
                                    
 *******
Walimu hawakujua lolote linaloendelea ofisini kwa mkuu wa shule hivyo waliendelea na ratiba za shule kama kawaida.
Wanafunzi walienda mstarini, wakajipanga vizuri kwa mistari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha NNE.

Mwalimu John ambaye alikuwa zamu kwa wiki ile alikuwa amesimama mbele kwaajili ya matangazo lakini ghafla akasikia wanafunzi wachache wakimzomea. 

Moyo wake ukamlipuka akautazama msitu ule wa watu lakini macho yake yakatua moja kwa moja kwa wanafunzi wa kidato cha NNE, akamwona Dorice na nyuma yake alikuwa amesimama Doreen akiwa anacheka sana kwa sauti ya dharau na kiburi. Hasira za mwalimu John zikampanda akaumanisha meno yake kwa ghadhabu

"Doreen! hebu njoo mbele haraka sana!" alisema mwalimu John kwa sauti kali iliyojaa ghadhabu lakini bila aibu Doreen aliachia sonyo Kali iliyowafanya wanafunzi wote wamgeukie yeye na kumwangalia kwa mshangao.
"We mtoto! unanisonya Mimi? una adabu kweli?"
"Kwanini nisikudharau wakati we mwenyewe umejidharau?" alisema Doreen kwa kujiamini sana.
"Ati nini?"alishangaa mwalim John kwani hakutegemea kama Doreen angekuwa jeuri kiasi kile.
"We unavokuja kazini hivo unategemea nini?"
"Vipi" alishtuka Mwalimu John.
"Unakuja kazini bila kuvaa suruali ili iweje!?"
"Una wazimu wewe nani hajavaa suruali?"

"Jiangalie huko chini kama umevaa suruali;" alisema Doreen na kumfanya Mwalimu John ajiangalie vizuri akagundua kweli alikuwa hajavaa suruali. 


Alishtuka kupita kiasi wanafunzi wote wakamtazama Mwalimu John kwa mshangao kwani kweli alikuwa hajavaa suruali. Baadhi ya wanafunzi walicheka, lakini baadhi walimhuzunikia wakiamini kuna mchezo kachezewa na si bure.

Mwalimu John akakimbia mstarini pale Kama mwendawazimu na kwenda ofisini lakini kila alipojaribu kuvuta kumbukumbu zake alikumbuka kuwa alipotoka nyumbani alikuwa amevaa suruali tena suruali yake mpya ya kadeti.

 "Sasa imeenda wapi?? mnh hapana kuna MTU kanichezea lazima nimweendee Malawi hata Nigeria ntafika Ila siwezi kumwacha" aliwaza Mwalimu John na wakati huo waiimu wenzake waliamua kwenda nyumbani na kumletea suruali nyingine ili aweze kuondoka Nayo.
 
********
Baada ya wanafunzi kuingia darasani kwao. Doreen aliamua kumuita Dorice nje kwani alikuwa na mazungumzo nae mazito sana.Dorice alionekana kuogopa kwani wito ule haukuwa wa kawaida, akasimama kwa hofu akimtazama Doreen 

"vipi mbona unaogopa, unaogopa nini?" alisema Doreen.
"siogopi kitu!"alijibu Dorice
"basi nisogelee"
Dorice akamsogelea Doreen kwa hatua chache.
"Jana ulikuwa na nani pale kwenye mti usiku?" aliuliza Doreen huku akiuchezesha mguu wake wa kulia chini na mkono mmoja akiwa kaushika kiunoni.
"hukuniona au?" aliuliza Dorice kwa mshangao.
"jibu swali!"
"OK! nilikuwa na Eddy"
"nani yako Eddy?"
"Doreen unanitisha ujue?"
"kha! nakutisha nina mapembe hapa? nijibu swali langu"
"Eddy mpenzi wangu!"
"nimekupata sasa... tangu lini Eddy mpenzi wako hujui kama ni mume wangu mtarajiwa?"
"Ati nini....... Eddy ni. .."
 
Itaendelea .....

Post a Comment Blogger

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();
 
Top