0

Dodoma. Ukumbi wa Bunge juzi uligeuka uwanja wa malumbano na mipasho huku misemo ikichukua nafasi kubwa kutoka kwa wabunge wa chama tawala CCM na upinzani.
Malumbano hayo yalizuka baada ya Bunge kukaa na kujadili Mwelekeo wa Mpango wa Taifa, lakini ghafla wabunge walianza kurushiana maneno wakituhumiana kuwa majipu yanayotakiwa kutumbuliwa.

Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti, Mary Mwanjelwa, malumbano yalianza kwa Mbunge wa Viti Maalumu, Jesca Kishoa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe jambo lililoamsha mjadala mzito.

Kishoa alianza kumtaja Dk Mwakyembe kuwa ni jipu linalohitaji kutumbuliwa na Rais na kuwa nafasi aliyonayo hakustahili.

Kishoa alitaja sababu ya kumwita Dk Mwakyembe si msafi kwamba alitumia zaidi ya Sh238 bilioni kwa ajili ya kununulia mabehewa ambayo yalithibitika kuwa ni mabovu.

Kitendo hicho kiliamsha hasira za Dk Mwakyembe na kusimama kisha kukana Serikali kutumia kiasi hicho huku akisisitiza ikithibitika kuwa ni kweli yuko tayari kujiuzulu wadhifa huo.

Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Jenista Mhagama alisimama mara kadhaa kutaka Kishoa afute kauli lakini upinzani ulimtetea mbunge huyo.

Hata hivyo, Mwanjelwa aliwataka kuendelea na mjadala ili akaangalie kwanza kumbukumbu za Bunge kuhusu maneno yaliyotamkwa na baadhi ya wabunge.     

Post a Comment Blogger

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();
 
Top