Wakati
mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli,
akitarajiwa kuzindua kampeni zake kesho jijini Dar es Salaam, mgombea
kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa amekwama
kuzindua kampeni zake kama ilivyotangazwa awali.
Ukawa
unaoundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), National
Convention for Construction and Reform – Mageuzi (NCCR-Mageuzi), Chama
cha Wananchi (CUF) na National League for Democracy (NLD) umeahirisha
uzinduzi kutokana na kukosa mahali patakapotosha ‘mafuriko’ ya watu
watakaohudhuria.
Lowassa
alitarajiwa kufungua pazia kwa kuzindua kampeni zake kwenye Uwanja Mkuu
wa Taifa jijini Dar es Salaam, lakini serikali imekataza uwanja huo
kutumika kwa kampeni za vyama vya siasa.
Mkurugenzi
wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene, akiongea na waandishi wa
habari Jumatano wiki hii, alisema serikali imefikia hatua hiyo kwa vile
kusudio la ujenzi wa uwanja huo ni shughuli za michezo pekee na si
vinginevyo.
Kampeni
zinazoanza kesho pia zitahusisha wagombea urais kupitia vyama vingine
vya siasa vikiwamo ambavyo wagombe wake hawapewi nafasi kubwa ya kuibua
ushindani kama itakavyokuwa ama kukaribia kwa CCM na Ukawa.
Pia kuanza kwa kampeni hizi kutawahusisha wagombea ubunge na udiwani watakaoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Afisa
Habari wa Chadema iliyo mshirika katika Ukawa, Tumaini Makene, amesema
kuwa, Lowassa anayewania Urais akiwa na mgombea mwenza Juma Duni Haji,
ameahirisha kuzindua kampeni zake mpaka itakapotangazwa baadaye.
Alisema
kuahirishwa kwa uzinduzi huo kunalengo la kutoa fursa kwa Ukawa
kujiweka sawa hasa katika kupata uwanja wenye uwezo wa kuwajumuisha watu
wengi na nafasi za kuegesha magari.
“Mgombea
wetu hatazindua kampeni leo wala kesho, waache hao wengine waanze sisi
tunajipanga kupata eneo zuri litakalotosha kwa idadi kubwa ya watu
tunaowatarajia ikiwamo na maegesho ya magari,” alisema.
Makene
alisema kutokana na uzeofu uliojionyesha wakati mgombea wao akitafuta
wadhamini ama kutambulishwa mikoani, wanaamini kuwa mkutano wao
utahudhuriwa na watu wengi, hivyo ni muhimu wakatafuta eneo kubwa la
kutosha watu wengi na maegesho ya vyombo vya usafiri.
Wakati
ikitarajiwa kuzindua kampeni zake kesho, CCM imeshatangaza kamati ya
watu 32 kwa ajili ya kutafuta ushindi, ikiongozwa na Katibu Mkuu wa
chama hicho, Abdulrahaman Kinana.
Kamati
hiyo ilitangazwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye,
Jumanne wiki hii ambaye alimuita Kinana kama mwanaharakati wa kivita
anayefahamu medani za ushindi.
Uchaguzi
wa mwaka huu ambao unatarajiwa kuwa na changamoto kubwa hasa kutokana
na mgombea anayeungwa mkono na Ukawa (Lowassa) akitokea CCM, kuonyesha
upinzani mkubwa dhidi ya CCM alichokuwa mwanachama wake tangu mwaka
1977.
Licha
ya kuwa mwanachana, Lowassa ameshika nafasi tofauti ndani ya CCM na
serikalini ikiwamo Uwaziri Mkuu aliojiuzulu mwaka 2008.
Lowassa
alikuwa pia katika timu ya kampeni za mwaka 2005 ambapo Rais Jakaya
Kikwete aliwania nafasi hiyo kwa mara ya kwanza na kupata ushindi wa
kishindo.
Hata
hivyo, Julai 29, mwaka huu, Lowassa aliamua kujiunga na Chadema ikiwa
ni siku chache baada ya jina lake kukatwa katika hatua za awali za
kuwachuja watia nia waliotaka kuwania Urais kupitia CCM.
Jumla
ya makada 42 wa CCM walijitokeza kwenye kinyang’anyiro cha kumtafuta
mgombea urais ambapo 38 walirejesha fomu na Magufuli aliibuka kuwa
mshindi atakayegombea Urais katika ‘kumrithi’ Rais Kikwete.
Macho
na masikio ya wapiga kura wengi kuanzia kesho yataelekezwa kwenye
uzinduzi wa kampeni hizo kusikia sera za vyama hivyo vikubwa
vinavyoshindana kumpata Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Post a Comment Blogger Facebook