Dar es Salaam. Pamoja na kupata
ushindi wa mabao 3-0 jana, Yanga iliweka rekodi mbaya ya kukosa penalti
mbili ndani ya dakika 10 za mchezo huo dhidi ya Djibouti Telecom kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hata hivyo,
mshambuliaji Malimi Busungu aliyeibuka mchezaji bora wa mechi hiyo na
kuzawadiwa king’amuzi aliiokoa timu yake baada ya kuifungia mabao mabao
mawili, dakika ya 26, akiunganisha krosi ya beki Mghana Joseph Zuttah na
kuongeza la pili dakika 65, akiunganisha krosi ya kinda aliyeng’ara
Geofrey Mwashiuya.
Chipukizi huyo aliyeingia uwanjani
kipindi cha pili akitokea benchi alifunga bao la tatu kwa juhudi binafsi
baada ya kuwatoka mabeki wa Telecom na kupiga shuti lililogonga mwamba,
kisha kumgonga mgongoni kipa Nzokira Jeef na kuingia wavuni na kuiweka
Yanga katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa robo fainali ya mashindano ya
Kombe la Kagame.
Yanga iliingia kwenye mchezo huo ikiwa
na kumbukumbu ya kufungwa mabao 2-1 na Gor Mahia ya Kenya Jumamosi
kwenye mechi ya ufunguzi pamoja na kukosa penalti iliyopigwa na nahodha
Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kadi nyekundu ya mshambuliaji wake, Donald
Ngoma.
Jinamizi la kukosa penalti liliendelea kuiandama
timu hiyo baada ya washambuliaji wake vinara wa ufungaji msimu
uliopita, Amissi Tambwe na Simon Msuva kukosa penalti ndani ya dakika
10, huku Cannavaro akijiweka kando wakati wa upigaji wa penalti hizo.
Tambwe
alikosa penalti yake dakika 39, baada ya Msuva kuangushwa ndani ya eneo
la 18 na beki wa Telecom, Warsama Ibrahim aliyepewa kadi ya njano kwa
kitendo hicho.
Wakati mashabiki wakishangaa, Tambwe
kukosa penalti hiyo katika dakika 45, Yanga ilipata penalti ya pili
iliyopigwa na Msuva iliyoshia mikononi mwa kipa wa Telecom, Jeef na
kuwafanya mabingwa hao mara tano wa Kagame kwenda mapumziko wakiwa mbele
kwa bao 1-0.
Kutokana na kukosa penalti hizo, kocha
Hans Pluijm aliwapumzisha Msuva na Tambwe na kuwaingiza Mwashiuya na
Kpah Sherman wakati Telecom ilimtoa Said Elmi na kumwingiza Warsama
Said.
Kipindi cha pili Telecom iliyovaa jezi nyekundu
na kushangiliwa kwa nguvu na mashabiki wanaodhaniwa kuwa wa Simba
ilianza kucheza kwa kujiamini kulinganisha na dakika 45 za kwanza
ambacho Yanga ilitegeneza nafasi nyingi, lakini washambuliaji wake
walikosa umakini.
Yanga iliyocheza mfumo wa 4-3-3,
ilitawala vizuri katikati ya uwanja baada ya kuingia kwa Mwashiuya na
Sherman waliokuwa na maelewano mazuri na viungo wa Salum Telela, Deus
Kaseke.
Kwa matokeo hayo, Yanga inahitaji ushindi dhidi
ya KMKM ya Zanzibar ili kujihakikishia kucheza hatua ya robo fainali ya
mashindano hayo.
Katika mchezo wa mapema, wawakilishi
wa Zanzibar, KMKM walijiweka katika mazingira magumu ya kufuzu kwa robo
fainali baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Al- Kahrtoum
ya Sudan kwenye uwanja huo.
Mshambuliaji Salah Bilal
alifungia Al- Khartoum bao la kuongoza, dakika ya 7, likiwa ni bao lake
la tatu katika mashindano hayo ya mwaka huu na kumfikia kiungo
mshambuliaji wa Gor Mahia, Michael Olunga mwenye idadi hiyo.
KMKM
ilisawazisha bao hilo kipindi cha pili kupitia kwa Simon Mateo dakika
ya 58, akitumia mpira mrefu uliopigwa na kipa wake ulioshindwa kuolewa
na mabeki wa Al Khartoum uliompa mwanya mfungaji kufunga bao hilo ambalo
ni la pili kwake.
Al- Khrtoum iljihakikishia pointi
tatu muhimu na nafasi kwenye robo fainali baada ya kupata bao la pili,
dakika 84, lililofungwa na Anthony Agay.
Katika mchezo wa Kundi C, uliochezwa Uwanja wa Karume, KCCA ya Ugand imeziduka kwa kuichapa Adama City ya Ethiopia kwa bao 1-0.
Post a Comment Blogger Facebook