Dar es Salaam. Ni fainali leo pale vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vitakapompitisha mgombea wake urais atakayepambanishwa na yule wa CCM, Dk John Magufuli aliyepitishwa Dodoma juzi.
Fainali hiyo ndani ya Ukawa inatarajiwa
kuhitimisha mvutano uliokuwapo baina ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba ambaye tayari amechukua fomu kuwania urais ndani ya
umoja huo na mgombea anayetajwa na Chadema, Dk Willibrod Slaa. Mwingine
aliyechukua fomu katika umoja huo ni Dk Kahangwa wa NCCR-Mageuzi.
Yeyote atakayeibuka katika mpambano huo na
kutangazwa rasmi leo, atakwenda kushindana katika fainali nyingine dhidi
ya mgombea wa CCM katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25.
Wanaopewa nafasi ni Dk Slaa aliyegombea urais kwa
mara ya kwanza mwaka 2010 na kutoa upinzani mkali kwa Rais Jakaya
Kikwete na Profesa Lipumba ambaye amejaribu bahati yake mara nne, 1995,
2000, 2005 na 2010 na sasa akitaka kujaribu kwa mara ya tano.
Wawili hao wameibua mvutano ndani ya vikao vya
Ukawa na wajumbe wengi walikuwa wanaipa nafasi Chadema kusimamisha
mgombea urais wa Muungano baada ya CUF kupewa nafasi ya kusimamisha
mgombea urais Zanzibar.
Jumamosi iliyopita, kamati ya viongozi ya wakuu wa
vyama vinavyounda umoja huo, NCCR-Mageuzi, Chadema, NLD na CUF
ilikutana asubuhi na jioni kutoa tathmini ya walichokubaliana mbele ya
wabunge wote na viongozi wa vyama hivyo kuwa mgombea wao atatangazwa
leo.
Akitangaza uamuzi huo, Profesa Lipumba aliwaeleza
waandishi wa habari kwamba kuna mambo ya kujadiliana baina ya vyama
hivyo ila hayawezi kuleta matatizo, kwamba wapo pamoja na watatoa majibu
ya pamoja.
Takriban wiki mbili sasa, viongozi wa Ukawa
wamekuwa na mjadala mzito kuhusu kugawana majimbo ambayo mpaka sasa
wamekubaliana kwa asilimia 97 na kushindwa kuafikiana kuhusu urais
kutokana na mvutano kati ya Chadema na CUF.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliliambia
gazeti hili jana kuwa kikao cha leo kipo palepale na kusisitiza kuwa
bado wanaendelea na mazungumzo.
“Watanzania wasubiri kesho (leo) tutawaleleza
kilichoafikiwa. Unajua kwenye siasa saa 24 zinaweza kuwa miezi 24. Siasa
ni siasa na kila kitu kinawezekana katika siasa,” alisema.
“Kama tumeshawaambia watu kesho (leo) ndiyo
tutazungumza, itabaki kuwa hivyo. Leo (jana) hatuwezi kusema chochote.
Unajua tuna vitu vingi tunaendelea kuvikamilisha kwa sasa, tuvute subira
na kila kitu tutakiweka wazi kesho,” alisema Mbowe.
Leo kabla ya kumtaja mgombea wa urais, viongozi wa
Ukawa watakuwa na kikao cha majadiliano ambacho kitatoa mwelekeo wa
umoja huo huku taarifa kutoka ndani ya vyama hivyo zikieleza kuwa
mwafaka bado haujapatikana.
Post a Comment Blogger Facebook