0
Katika maisha kuna watu ambao wamefanikiwa sana na kuna ambao wanasukuma tu maisha siku ziende. Na ukiangalia hawa ambao wamefanikiwa sana kuna ambao walianzia chini kabisa, hawakuwa na elimu kubwa, hawakurithi mali na pia hawakupata watu wa kuwapa mitaji au kuwasaidia. Ila kwa hatua fulani wameweza kufikia mafanikio makubwa sana.
Inawezekana wewe ni mmoja wa watu ambao bado hujafikia mafanikio makubwa unayotazamia. Huenda umejaribu sana ila unaona kama bahati haiku upande wako. Huenda pia unaona kwa elimu ndogo uliyopata hutaweza kufikia mafanikio makubwa. Au kwa kuwa wazazi wako walikuwa masikini hivyo na wewe utaishia kuwa masikini.
Sasa leo nataka nikuambie kwamba yote hayo unayofikiria yanakukwamisha wewe kufikia mafanikio ni ya uongo. Nakuhakikishia unaweza kufikia mafanikio makubwa kama utazijua hatua muhimu za kukufikisha kwenye mafanikio na ukazitumia ipasavyo.
Leo utazijua hatua hizo kwenye makala hii, na kazi yako itakuwa ni kuanza kuzitumia hatua hizi mapema iwezekanavyo ili uweze kubadili maisha yako.
1. Amua ni nini unataka kwenye maisha yako
Hii ndio hatua ya kwanza na muhimu sana ili kuweza kufikia mafanikio makubwa. Cha kushangaza ni kwamba karibu asilimia 90 ya watu hawajui ni nini wanachotaka kwenye maisha yao. Hebu nikuulize ni nini hasa unachotaka kwenye maisha yako? Ukinijibu unataka kuwa na hela nyingi au kuwa tu na mafanikio makubwa basi hujui unachotaka. Unatakiwa ujue ni nini hasa unachotaka kwenye maisha yako. Kama ni fedha, sema ni kiwango gani cha fedha unachotaka na kwa muda gani. Kama unataka kufikia mafanikio makubwa ni lazima ujue mafanikio makubwa kwako wewe ni nini.
Kaa chini sasa na uandike kwenye kitabu chako cha malengo ni kitu gani unachotaka kwenye maisha yako. Kujua unakoelekea ndio mwanzo mzuri wa safari yako.
2. Jua ni gharama gani unatakiwa kulipa ili kufikia mafanikio unayotarajia
Kuna baadhi ya watu wanajua kabisa ni nini wanataka kwenye maisha yao na wamekuwa wakitamani sana kufikia kile wanachotaka. Lakini siku zinakwenda bila ya kuweza kufikia kile wanachotaka. Hii inatokana na watu hao kutojua gharama wanayotakiwa kulipa ili kufikia mafanikio wanayotarajia. Sikiliza utaendelea kuwa hivyo ulivyo kama utaendelea kuishi maisha unayoishi sasa. Na ili uweze kufikia mafanikio makubwa ni lazima uanze kubadilisha mfumo wako wa maisha wa sasa.
Katika kila jambo zuri unalotaka, kuna gharama utahitajika kulipa ili uweze kupata jambo hilo. Kama unataka kuongeza kipato zaidi ya unachopata sasa utahitajika kufanya kazi zaidi na kwa maarifa zaidi. Utahitaji kupunguza matumizi yasiyo ya msingi na pia utahitaji kupunguza muda unaopoteza kwenye mambo yasiyo ya msingi.
Jua ni gharama gani utakayotakiwa kulipa ili kufikia mafanikio makubwa na jipange kulipa gharama hiyo. Kama unafikiri unaweza kufikia mafanikio makubwa kwa kuendelea kuishi unavyoishi sasa unajidanganya. Gharama kubwa utakayotakiwa kulipa kwenye kila hatua kubwa unayotaka kupiga kwenye maisha yako ni kufanya kazi kwa bidii na maarifa.
3. Weka milango na mipango ya muda mfupi na muda mrefu
Baada ya kujua unataka nini kwenye maisha yako na kukubali kulipa gharama ya kupata unachotaka, sasa unahitaji kuwa na malengo na mipango. Ni vigumu sana kufanya jambo kubwa kwenye maisha yako kama huna malengo na mipango. Unahitaji kuwa na malengo ya muda mrefu, mwaka mmoja, miaka miwili, miaka mitano na hata miaka kumi. Malengo haya yaendane na kile unachotaka kwenye maisha yako ili ufikie mafanikio makubwa.
Pia unahitaji malengo ya muda mfupi, miezi sita, miezi mitatu, mwezi, wiki na hata siku. Kila siku hakikisha umeipanga kufanya kitu ambacho kitakusogeza kufikia malengo yako makubwa. Malengo yoyote unayopanga hakikisha unayaandika kwenye kitabu chako cha malengo. Malengo na mipango yako ndio yatakuwa muongozo kwenye maisha yako.
4. Kuwa mwaminifu
Katika safari yako ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa, uaminifu ni nguzo muhimu sana. Ukikosa uaminifu utapoteza kila kitu ambacho umekuwa unakijenga kwa bidii na maarifa. Kuna picha ambayo imejengwa na jamii yetu kwamba watu waliofanikiwa ni wezi, wanadhulumu au wanatapeli. Ukweli ni kwamba watu wanaofanikiwa kwa njia hizo, mafanikio yao hayadumu kwa muda mrefu. Utakuwa shahidi yangu kwamba umewahi kuona watu wengi ambao ni wezi na maisha yao yanaishia wapi. Au wanaofanya biashara haramu mwisho wao unakuwa nini.
Usidanganyike hata kidogo kujihusisha na kazi au biashara yoyote ambayo ni kinyume na sheria au kinyume na imani au kisimamo yako binafsi. Uaminifu unalipa, jinsi unavyokuwa muaminifu ndivyo watu wengi wanavyokuamini na ndivyo itakavyokuwa rahisi wewe kufikia mafanikio makubwa.
5. Kuwa mvumilivu
Huu ndio ukweli ambao watu wengi hawapendi kuusikia. Hakuna kitu kwamba utalala masikini uamke tajiri, hakuna na ikitokea hivyo utajiri huo utapotea haraka kama moshi unavyopotea. Unahitaji muda ili kuweza kufikia mafanikio unayotarajia. Na katika muda huo utashindwa mara nyingi sana. Kama utakosa uvumilivu utaona muda huo ni mrefu sana na pia utakata tama kutokana na kushindwa. Na ukishakata tamaa ndio mwisho wa safari yako ya kufikia mafanikio makubwa. Uvumilivu ndio tofauti kubwa kati ya watu waliofanikiwa na ambao wanasukuma tu maisha yaende. Unahitaji kuwa mvumilivu sana na kuendelea kujifunza kutokana na makosa unayofanya.
Fuata hatua hizi tano na zifanyie kazi kila siku. Kama utazifuata kweli baada ya muda utaona mabadiliko makubwa kwenye maisha yako. Uwezo wa kufikia mafanikio makubwa unao, ni wewe tu kuanza kuutumia ili kufikia mafanikio hayo.

Post a Comment Blogger

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();
 
Top