Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, amesema
mgombea urais wa chama hicho, Dk. John Magufuli, ni chaguo la Mungu.
Akizungumza na wazee, wanawake, vijana na wanachama wa CCM Mkoa wa
Dar es Salaam jana, alisema jina la Dk. Magufuli lilijitokeza katika
hatua zote za uteuzi ikiwamo vikao vya wazee na hata katika Mkutano Mkuu
alichaguliwa na maelfu, jambo linaloonyesha anakubalika kwa wote.
Alisema Mungu ametoa hukumu yake kwa mtu wake na Watanzania ndiyo wataamua katika sanduku la kura.
“Magufuli ni mgombea wa sampuli nyingine, ni mzalendo anapenda
watu, nchi yake kwa dhati, asiyejikweza hana makuu, anamwamini Mungu,
anatambua CCM imemfikisha alipo leo, ni kada mzoefu… sifa yake nyingine
anapenda kuona matokeo ya kazi anayoifanya na aliyopewa kuifanya,”
alisema.
Kikwete ambaye ni Rais wa Awamu ya nne, alimwagia sifa Dk. Magufuli
kuwa ni mmoja wa watumishi wa umma ambaye hakusita kutangaza Ilani ya
chama chake na chama kwa ujumla, hivyo ni kada wa uhakika, mzoefu ndani
ya CCM anayestahili kuunda serikali ya awamu ya tano.
“Wapo maafisa wa serikali wanaona haya kusema wanatekeleza ilani ya
CCM, lakini Magufuli katika kazi zake zote alisema anatekeleza Ilani ya
CCM na anatambua yupo alipo kwa sababu ya chama na siyo kwa ujanja na
fedha zake kwa kuwa hana fedha,” alibainisha.
UTEUZI WAKE WAKIPA SIFA CHAMA
Kikwete alisema uteuzi wa Magufuli unakipa sifa chama kuwa
hakinunuliki kwa kuwa hakuwahi kujivuna kwa fedha wala mali, kwani ndani
ya siasa mtu anaweza kuwalipa wachache kwa tamaa na njaa zao, lakini
huwezi kununua chama.
“Nawaambia watalipa wachache, lakini hawatawanunua Watanzania wataamua,” alisema na kuongeza:
“Sifa nyingine ni Mungu ametaka Magufuli awe rais, kwani aliwahi
kuja Ikulu kuzungumza nami masuala ya makandarasi, nikamuuliza naona
wenzako wanachukua fomu wewe huchukui?”
“Aliniuliza kwani na mimi natosha? Nilimwambia wana-CCM ndiyo wataamua kama unatosha au la,” alisema.
Alisema Dk. Magufuli ni kada aliyechukua fomu kimya kimya bila kuita waandishi wa habari.
“Alichukua fomu bila mbwembwe, alitembea kutafuta wadhamini bila
wapambe na alirudisha bila mbwembwe na mgombea wa namna hiyo anakifaa
chama na Watanzania,” alisema
Alisema mgombea huyo hana mbwembwe kwani alipoulizwa kama ana
kikosi cha kazi, alisema anaweza kufanyakazi na yeyote na kukiachia
chama kupanga timu ya ushindi ya makada 32.
Aidha, alimmimina sifa Dk. Magufuli kuwa hakubali kushindwa katika
jambo lolote, mbunifu, anachukia wazembe, wababaishaji wala rushwa na
kwamba atapendwa na kila Mtanzania anayechukia mambo hayo.
MAGUFULI: NINATOSHA PANDE ZOTE
Kwa upande wake, Dk. Magufuli alisema anatosha pande zote, mbele,
katikati, nyuma, kulia kushoto na ubavuni, na yupo tayari kupeperusha
bendera ya CCM na kuongoza serikali ya awamu ya tano.
“Mwalimu alipotaka kwenda kupigana vita na Idd Amini, alianzia Dar
es Salaam, marais wote waliopita walipoaanza safari ya kwenda Ikulu
walianzia hapa, nimekuja kwenu wazee wa Dar es Salaam, vijana na
kinamama kuomba baraka, nasaha, busara na dua zenu kabla ya kuanza
safari yangu. Jumapili nitaongea mengi leo (jana) ni hayo tu,” alisema.
Alisema yuko tayari kupeperusha bendera ya CCM bila kigugumizi,
kinyongo, uchovu na manunguniko hadi kuhakikisha serikali ya awamu ya
tano inaingia Ikulu.
“Wana CCM tushikamane kura za maoni za urais, ubunge na udiwani
zimekwisha, jukumu letu liwe kuhakikisha tunafanya kampeni uvungu kwa
uvungu, kitanda kwa kitanda, chumba kwa chumba na nyumba kwa nyumba
kuhakikisha CCM inaunda serikali ijayo, ni chama kikubwa kimehimili
mengi na kina uwezo wa kuendelea kutawala,” alibainisha na kuongeza:
“Nawathibitishia natosha na ninatosha kweli kweli, mbele, katikati,
nyuma na ubavuni, wanatosha mgombea mwenza, madiwani na wabunge.”
Shida za wana-Dar es Salaam na Watanzania nazifahamu…uzoefu wa miaka 20 serikalini unanitosha, sikuwahi kushindwa mahali.”
Mgombea Mwenza, Samia Suluhu, alisema ni mama wa watoto wanne,
hivyo matatizo ya Watanzania anayajua kama mama anayeijua familia yake
na kuwataka kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono CCM.
SOURCE:NIPASHE
Post a Comment Blogger Facebook