Jina la James Lembeli siyo jipya kwenye medani
za siasa. Huyu ni moja ya wanasiasa waliopata umaarufu mkubwa katika
kipindi cha ndani ya miaka 10 alichokaa bungeni akiwakilisha Jimbo la
Kahama kwa tiketi ya CCM.
Kwa takriban wiki moja, jina
hilo limeteka vyombo vya habari baada ya kukacha kugombea ubunge kupitia
chama hicho tawala kilichomlea tangu akiwa kijana kabla ya juzi kuhamia
Chadema, kisha kutangaza kuwania ubunge katika Jimbo la Kahama Mjini.
Mwanasiasa
huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira hadi hapo Agosti 20, alichaguliwa kuwa Mbunge wa Kahama mwaka
2005 na kutetea kiti hicho mwaka 2010.
Lembeli ni moja
ya wabunge wa CCM watakaokumbukwa katika Bunge la tisa na 10 kwa
michango yake mingi ya kujenga na hata kuikosoa Serikali yake moja kwa
moja katika masuala mbalimbali yaliyoonekana bayana kuathiri wananchi.
Ni moja ya wabunge ambao walionekana waziwazi kuichukia rushwa na ufisadi na ndiyo sababu ya misingi aliyoitaja kumkimbiza CCM.
Kwa
nafasi yake hiyo ya kuongoza kamati inayojihusisha na masuala ya ardhi,
maliasili na mazingira, Lembeli alionekana kuwa mkali kwa Serikali hasa
katika migogoro ya ardhi, ujangili wa wanyamapori na usafirishaji wa
magogo.
Ikumbukwe kuwa mwaka 2013 alikuwa injini kuu ya
uchunguzi wa sakata la uvunjifu wa haki za binadamu la Operesheni
Tokomeza Ujangili uliofanywa na kamati yake na kuitikisa Serikali ya
Rais Jakaya Kikwete.
Matokeo ya uchunguzi huo
yalisababisha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel
Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai
Nahodha, Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk Mathayo David
Mathayo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki
kujiuzulu.
Mbali na safari yake ijayo ya ubunge wa
kutegemea ridhaa ya Chadema, hatua ya Lembeli kuhamia katika chama hicho
cha upinzani huenda ikaongeza harakati zake za kupambana na ufisadi na
kuleta maendeleo.
Post a Comment Blogger Facebook