0

Ni kweli inauma mno kutelekezwa na mzazi. Mimi ambaye baba na mama yangu walinilea kwa umoja wao pamoja na umaskini wetu, huwa nawaza ingekuwaje baba au mama asingekuwa karibu yangu? Malezi ya mzazi mmoja au wote wasingekuwepo. Inaumiza sana!

Hiyo ndiyo sababu naweza kuhisi kile ambacho kinamuumiza mtoto aliyetelekezwa. Mimi ni baba, najua ni kiasi gani mtoto wangu ananihitaji kwa ukaribu. Upendo wangu kwake umekuwa zawadi yake muhimu kutoka kwangu kuliko kitu chochote. Hivyo basi, najua atapitia machungu kiasi gani kama nikimtelekeza.

Chukua hii; Kwa hali yoyote ile, mzazi hana leseni ya kumtelekeza mtoto wake. Changamoto zije na ziondoke, hakikisha unabaki umemganda mwanao. Kosa la kumtelekeza mtoto linafanana na la kuua. Huyo ni mtoto wako, unamkimbia, unataka alelewe na nani?

Mwanamuziki Aboubakar Shaban Katwila ‘Q Chilla’ katika nyimbo zake Aseme na Si Ulinizaa, alionesha wazi kuumizwa na alivyokataliwa na baba yake, Shaban Katwila, tangu akiwa mimba.

Baba mcheza soka maarufu Tanzania, mtoto anaishi kwa shida, akisaidiwa na wasamaria wema, wakati huo mama mzazi alishafariki dunia. Q Chilla akaokotwa! Ukitafakari vizuri unaweza kuhisi Q Chilla aliumia kiasi gani.

Baada ya vilio vingi, mzee Katwila alitumia njia mbalimbali kutengeneza suluhu na mwanaye. Wakasameheana na kudumisha upendo kama mtu na mzazi wake. Tangu hapo, Q Chilla alipitia vipindi vingi vibaya, baba yake akawa msaada wake.

Mara ya mwisho nilipozungumza na Q Chilla, alikiri kuwa yupo kwenye kipindi kizuri sana cha maelewano na baba yake na kwamba alikuwa mmoja wa watu waliompigania aweze kuacha matumizi ya dawa za kulevya baada ya kutopea.

Chukua hii; Watu hufanya makosa lakini ni haohao hugeuka watu wazuri. Anaweza kukutenda leo lakini kesho akakufaa. Ni mwongozo wa wahenga kuwa hupaswi kutupa jongoo na mti wake.

Isisahaulike migogoro ya kimapenzi husababisha maumivu mengi kwa watoto, vilevile uchonganishi kati ya mtoto na mzazi mmoja. Mama akibaki na mtoto baada ya kutofautiana na baba yake, anaweza kumjaza mtoto sumu kuwa baba yake alimsusa, hakumjali.

Hutokea kwa akina baba ambao hulea watoto bila mama zao, nao hutema sumu yenye uchonganishi kati ya mtoto na mama yake. Ni vizuri sana mtoto anapopevuka ayapime matukio ya nyuma kwa kutumia akili ya kikubwa. Anaweza kupata majibu ambayo ni mazuri mno kwa maisha yake.

Kwanza mzazi ambaye anamtelekeza mtoto wake ni mtu ambaye anastahili mno kuhurumiwa, maana hawezi kuwa sawasawa. Binadam aliyekamiliki kiakili anatambua kuwa mtoto ni sehemu ya maisha yake, hatathubutu kumtelekeza.

Stadi wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul Juma ‘Diamond Platnumz’ ana machungu yake. Alishapata kueleza kuwa baba yake, Abdul Juma hakuwa na muda naye kipindi anakua, hivyo jukumu la malezi na ukuaji wake, lilisimamiwa na mama yake, Sanura Kassim ‘Sandra Khan’.

Malezi ya Diamond yalijaa machozi na jasho, mama yake akihangaika huku na huko kuhakikisha mtoto wake anapata mahitaji muhimu, japokuwa haikuwezekana kupata yote. Kwamba wakati huo wa mateso, baba yake aliendekeza utoto wa mjini, akashindwa kuzingatia kuwa yeye ni baba.

Diamond naye ameamua kutoa adhabu kali kwa baba yake. Hamshirikishi kwenye mafanikio yake. Wengi tu wanakula matunda ya kazi yake ya muziki ambayo imempa umaarufu mkubwa barani Afrika na kwingineko duniani, baba mtu haambulii chochote.

Baba Diamond anapigika, anaumwa anakosa mpaka msaada wa matibabu, wakati huo Diamond anatapanya fedha kwa watu wengine. Inawezekana anafanya hivyo kutokana na hasira kali alizonazo, ila zimezidi kipimo.

Leo hii Diamond hana ubavu wa kumfuta baba yake kwenye mzunguko wa maisha yake, isipokuwa atabaki kuwa baba yake anayemchukia. Na je, hizo chuki hazifiki mahali zikaisha?

Kuna adhabu kubwa ambayo Diamond anashindwa kuitumia, na yenyewe ni kuwa chanya kwa baba yake. Angekuwa anamjali na kumpa huduma nyingi muhimu, angekuwa anamsuta kwa vitendo, kwamba yeye alimtelekeza kisha anamhudumia.

Uamuzi wa Diamond kutomjali baba yake ni kisasi. Na ni mwendelezo wa damu mbaya ambayo mara nyingi huhama kutoka kwa mzazi mmoja kwenda kwa mwingine.

Leo hii Diamond ni baba, yupo vizuri na mwanaye kwa sababu hakuna mgogoro kati yake na mama wa mtoto wake ambaye pia anatarajia kumzalia mtoto wa pili. Mama ni raia wa Uganda, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, mtoto aliyepo ni wa kike, Latiffah, wanatarajia wa kiume.

Inaweza kutokea baadaye Diamond akagombana na Zari kisha akawa mbali na watoto wake kwa sababu ni wadogo. Mama akatumia nafasi yake kuwajaza sumu watoto wake kuwa baba yao aliwatelekeza. Nao wakikua wakamchukia baba yao. Diamond anatakiwa ayapime hayo.

Huu ni wakati mzuri mno kwa Diamond kukata mnyororo wa chuki kati yake na baba yake. Kutosikia kilio cha baba yake ambaye anaumwa ugonjwa mkubwa (kansa), ni roho ngumu mno. Ni roho ngumu mithili ya ile ya Jenerali Idd Amin Dada wa Uganda.

Diamond anayo nafasi ya kumhudumia baba yake kama ambavyo mtu anaweza kujitolea kwa ajili ya raia wengine wenye matatizo wanaomgusa. Kiusamaria wema tu. Ajitolee tu!

Namkumbusha kuwa alimnunulia gari aliyekuwa mkongwe wa muziki nchini, marehemu Marehemu Muhidin Maalim Gurumo, baba yake akiwa anaishi katikati ya dhiki kubwa. Vilevile amekuwa akinukuliwa kutoa misaada mbalimbali, baba yake anateseka. Misaada sharti ianze nyumbani.

Hiyo chuki mpaka lini Diamond? Mbona hujakana kutumia jina lake? Unaitwa Nasibu Abdul Juma, huyo Abdul Juma unamwacha anataabika kwa sababu ya visirani vya nyakati za giza. Tafadhali Diamond usiwe na roho ya Idd Amin, haikufai. Zipo baraka nyingi utaongezewa baada ya suluhu yako na baba yako.

Post a Comment Blogger

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();
 
Top