Askofu
wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amejitokeza leo na
kujibu tuhuma zilizotolewa dhidi yake na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa wiki moja
iliyopita.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Askofu Gwajima
amekanusha tuhuma za kuwa alimwambia Dk Slaa kuwa wapo maaskofu ambao
walihongwa na mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa na kuitwa mshenga wa
mgombea huyo.
Askofu
huyo amesema kuwa hajawahi kumwambia Dk Slaa kuwa maaskofu wa
Kikatoliki wamehongwa na Lowassa ili wamchague hivyo aliyoyasema Dk Slaa
ni kuwachafua viongozi hao wa dini.
Wakati
Dk Slaa anatangaza kustaafu siasa Septemba Mosi, alimwita kiongozi huyo
wa Kiroho kuwa ni mshenga wa Edward Lowassa kwa Chadema na kusema kuwa
askofu huyo alimwambia kuwa wapo maaskofu 30 wa Katoliki wamehongwa na
Edward Lowassa.
Licha
ya kukanusha tuhuma hizo, Akofu Gwajima amesema kuwa kuna watu
wanawatumia Dk Slaa na mchumba wake, Josephine, na kuwaonya waache
kutumika.
Pia Askofu Gwajima ametoa tuhuma kwa Usalama wa Taifa kuwa wanatumika pamoja na Dk Slaa.
“Mimi
najua wapo Usalama wa Taifa ambao wanamlinda Dk Slaa lakini nawaomba
sana Usalama wa Taifa walinde nchi ikae kwa amani, wasijiingize kwenye
siasa au kulinda kikundi flani’’ alisisitiza Gwajima.
Aidha
askofu huyo amesema kuwa kama Dk Slaa atajitokeza kumjibu kwenye vyombo
vya habari, na yeye atajitokeza kuelezea mambo aliyoyafanya Dk Slaa
Afrika ya Kusini akiwa na vijana wa Usalama wa Taifa siku chache kabla
ya kutangaza kuachana na siasa.
Kiongozi huyo wa Kiroho amewataka wananchi waangalie ni mtu yupi anayefaa na wasije wakagawanywa na harakati zinazoendelea.
CHANZO: MWANANCHI
Post a Comment Blogger Facebook